Na CHRISTIAN BWAYA,
UTAMBULISHO ni hitaji la msingi kwa kila mwanadamu aliyekamilika. Tunajisikia vizuri kujua sisi ni nani na tumetoka wapi. Unapojikuta kwenye mazingira ambayo huna uhakika na utambulisho wako, thamani yako inapungua. Huwezi kuwa na ujasiri katika mazingira haya.
Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 imelitambua hili. Imempa mtoto haki ya kupata utambulisho kwa jina, uraia, uzazi na ukoo. Jambo hili limekuwa sehemu ya utamaduni wetu kwa muda mrefu. Wazee wetu walihakikisha tunaufahamu ukoo wetu kwa vizazi kadhaa. Lengo lilikuwa ni kumjengea mtoto utambulisho unaoeleweka.
Katika makala haya tunaangalia haki nyingine muhimu kwa mtoto ambayo ni malezi.
Malezi ya familia
Sheria hii imempa mtoto haki ya kuishi na wazazi au walezi wake katika mazingira ya familia. Familia ni mkusanyiko wa baba na mama, watoto (wa kuzaliwa na kuasili), wakiwamo ndugu wengine kama babu, bibi, wajomba, shangazi, binamu, wapwa wanaoweza kuishi na mtoto.
Kuishi katika familia ni hitaji muhimu la kila mwanadamu. Maisha ya kifamilia yanamhakikishia mtoto uangalizi mzuri unaomsaidia mtoto kukua vyema kimwili, kiroho, kiakili, kimaadili na kijamii.
Unapotengwa na familia, kwa kawaida, unaweza kuathirika kisaikolojia. Sheria hii imelitambua hili na kufanya iwe kosa kwa mtu yeyote kumnyima mtoto haki ya kuishi na familia yake.
Hata hivyo, yanaweza kuwapo mazingira yanayohalalisha mtoto kutengwa na familia yake. Kubwa ni ikiwa mahakama itajiridhisha kuwa mazingira ya familia anayoishi mtoto yanahatarisha usalama na ustawi wake.
Mfano wa mazingira yasiyo salama kwa mtoto ni yale yanayoweza kuleta hatari kwa mtoto; yanayoweza kumfanya mtoto akadhalilishwa na hata pale inaponekana kumtoa nyumbani inaweza kuwa salama zaidi kwa mtoto.
Fikiria mazingira ambayo mtoto analelewa na wazazi wenye matatizo ya kiakili; walevi kupindukia; wazazi wenye tabia ya ugomvi na matumizi ya nguvu kupita kiasi hali inayoweza kumuathiri mtoto kiakili, kimaadili, kihisia au kimwili.
Ikithibitika kuwa nyumbani anakoishi mtoto kuna hatari ya namna hiyo, inaweza kuamuliwa kuwa mtoto ahamishiwe kwingine. Uamuzi wa kumtenga mtoto na wazazi wake unapochukuliwa, utahakikisha kuwa mtoto anapelekwa kwenye mazingira yenye kumhakikishia usalama wake.
Ubora wa malezi
Sheria haijaishia kumhakikishia mtoto malezi ya familia. Imeainisha aina za huduma anazostahili mtoto kutoka kwa wazazi /walezi wake. Izingatiwe kuwa mzazi, kwa mujibu wa sheria hii ni mwanamume au mwanamke aliyemzaa mtoto, au mtu mwingine aliyepewa haki ya kisheria kumuasili mtoto. Mlezi ni mtu anayewajibika kumlea na kulinda mali na haki za mtoto.
Kwa mujibu wa sheria hii, mzazi/mlezi au watu wengine wanaomlea mtoto watahahakisha mtoto anapata huduma za msingi kama chakula, malazi, mavazi, huduma za afya ikiwa ni pamoja na chanjo, elimu na ushauri, uhuru wa kucheza na kuburudika.
Kwa kutambua kuwa huduma hizi ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto, ni kosa kumnyima mtoto huduma hizi kwa sababu yoyote ile ikiwamo dini/imani, utamaduni au hata ulemavu alionao mtoto.
Sambamba na huduma hizi, mzazi/mlezi na mtu mwingine atawajibika kumlinda mtoto na aina zote za uonevu, udhalilishaji, kutelekezwa, maumivu kihisia, kiakili au kimwili. Katika mazingira ambayo mzazi hayupo kwa muda, atahahakisha mtoto anaangaliwa na mtu anayeaminika.
Itaendelea
Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754-870-815.