24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIASA ZILIVYOZALISHA GENGE KUBWA LA ‘UNGA’ JAMAICA – 2

Christopher Coke a.k.a Dudus (kulia), tajiri wa dawa za kulevya

 

Luqman Maloto,

TUNAENDELEA na makala yetu ya Shower Posse ambayo ilianza wiki iliyopita ambapo tuliishia kuangalia mwanzo wake. Endelea….

Shower Posse Marekani

Katika kitabu cha Born FI’ Dead (Kuzaliwa Mpaka Kufa), mwandishi wa Marekani, Laurie Gunst anaeleza kuwa kutokana na Jim Brown kuiweka Serikali ya Jamaica mfukoni wakati wa utawala wa Seaga, Shower Posse ilikuwa huru mno kusafirisha mihadarati na bunduki kwenda kuuza Marekani.

Gunst anaandika pia kuwa mwanzoni miaka ya 1980, Shower Posse ilijitanua Marekani kwenye majimbo ya New York, New Jersey, Florida na Pennsylvania peke yake.

Hata hivyo, kutokana na mafanikio makubwa ya kibiashara ambayo Shower Posse iliyapata kupitia biashara ya bangi, cocaine na bunduki, ilitanua wigo mpaka kuenea maeneo mengi Marekani na baadaye Canada na Uingereza.

Kufikia mwaka 1983, tayari Jim Brown alikuwa tajiri mkubwa na anayetafutwa mno na Marekani. Akageuka kuwa mfadhili wa JLP kifedha na kiulinzi. Seaga akawa anamfuata Jim Brown kuomba misaada na si kumtuma tena kazi za ulinzi.

Mpaka hapo unaweza kuona maajabu ya biashara ya dawa za kulevya, kwamba mtu anahama kutoka maskini kabisa, anayeamua kutumia ushawishi wa mtaani kumiliki genge la vijana wahuni wa ghetto mpaka kuwa tajiri anayemiliki mtandao mkubwa kwenye mataifa makubwa matatu, yaani Marekani, Uingereza na Canada ndani ya muda mfupi.

Mtu mbaya, Vivian Blake, ndiye aliyekuwa msimamizi wa matawi ya Shower Posse nchini Marekani. Blake pia ni mzaliwa wa Tivoli Gardens. Mwaka 1973 alihamia New York, Marekani na kuanza kuwa msambazaji wa bangi na cocaine kwenye jimbo hilo.

Machi 30, 2010, mwandishi Patrice O’Shaughnessy, aliandika kwenye gazeti la New York Daily News kuwa Blake ni kati ya watu wachache kuwahi kutokea duniani ambao waliweza kufanya ubunifu wa kuendesha biashara ya unga kwa mtindo wa kisasa bila kukamatwa.

Jim Brown alimtumia Blake kueneza mtandao wa Shower Posse Marekani, akaunda mtandao mwingine Toronto, Canada kisha Uingereza. Mpaka hapo Shower Posse likawa miongoni mwa magenge (cartels) ya unga yanayotisha na yanayochunguzwa zaidi duniani.

Mwaka 1984, Jim Brown alikamatwa lakini aliachiwa kisha akaendelea kuchanua katika ulimwengu wa mihadarati. Mwaka 1989, mmoja wa wanachama wakubwa wa Shower Posse, Charles Miller ‘Little Nut’ alikamatwa na maofisa wa Marekani.

Baada ya kukamatwa, Little Nut aliahidiwa msamaha endapo angetaja mtandao wa Shower Posse na viongozi wake. Ndipo Little Nut alipomtaja Jim Brown kama bosi mkuu, vilevile akawaweka wazi viongozi wengine wa juu wa Shower Posse.

Kuanzia mwaka huo Little Nut alipofichua siri za Shower Posse, Marekani iliwekeza nguvu kubwa kumsaka Jim Brown. Iliweka mipango mingi ya kuhakikisha anakamatwa.

Jim Brown alianza kufuatiliwa Jamaica hasa kwenye maskani yake, Tivoli Gardens na watu wake wa karibu walifuatiliwa. Jim Brown alijikuta kwenye wakati mgumu kila upande baada ya majasusi wa Marekani kumwandama kwa ukaribu.

Mwaka 1992, Serikali ya Jamaica kwa shinikizo la Marekani, iliamua kumshikilia Jim Brown katika gereza la Tower Street Adult Correction, Kingston na huo ndiyo ukawa mwisho wa Jim Brown, kwani hakutoka tena nje.

Jim Brown akiwa gerezani, alipokea taarifa za kifo cha mtoto wake mkubwa wa kiume, Mark Anthony Coke ‘Jah T’ ambaye ndiye alikuwa msimamizi wa shughuli zote za Shower Posse wakati kigogo huyo alipokuwa mahabusu.

Jah T alikuwa akiendesha gari la kifahari Maxfield, St. Andrew, Jamaica, kabla ya kushambuliwa na watu ambao inasadikiwa ni mahasimu wa biashara za unga na genge la Shower Posse au maofisa wa Marekani ambao waliamua kumaliza nguvu zote za genge hilo.

Baadaye polisi walitoa ripoti kuwa takriban watu 12 waliuawa katika kipindi ambacho Jah T aliuawa. Mauaji hayo yalihusishwa na vurugu za wauza unga. Hata hivyo, upande wa pili, watu wengi walisema kuwa 12 waliouawa wakati huo walitokana na mtandao wa Shower Posse na watekelezaji wa mauaji hayo walikuwa majasusi wa Marekani.

Februari 1992, Jah T alizikwa, hivyo kukamilisha pigo kubwa zaidi kwa Jim Brown na genge lake la Shower Posse. Hata hivyo, kwa ujasiri kubwa aliendelea kuratibu mtandao wa genge lake akiwa gerezani. Kifo cha Jah T kilimuuma lakini hakurudi nyuma na hakutangaza kuachana na biashara ya mihadarati.

Baada ya kifo cha Jah T, hakikupita kipindi kirefu, moto wa ajabu ulitokea kwenye gereza la Tower Street Adult Correction na kumuunguza Jim Brown na huo ndiyo ukawa mwisho wake.

Moto huo ulipozimwa na Jim Brown kusadikiwa, tayari tajiri huyo wa dawa za kulevya alikuwa ameshafariki dunia kutokana na shambulio hilo la moto. Mpaka hapo ikawa imethibitika kuwa Jim Brown si wa dunia tena bali kaburini.

Unaitwa moto wa ajabu uliochukua uhai wa Jim Brown gerezani, lakini inaelezwa kuwa majasusi wa Marekani ndiyo ambao walitengeneza moto huo na kumuua tajiri huyo wa unga kwa sababu waliona hakukuwa na dhamira ya dhati kwa Serikali ya Jamaica kushughulikia mashitaka dhidi yake ya kuuza unga.  

 

Mwisho wa shower Posse

Christopher Coke ‘Dudus’ au President (Rais), ni mtoto wa kuasili wa Jim Brown. Kwa maana hiyo, Dudus hakuwa mtoto wa kibaiolojia wa Jim Brown, ingawa ndiye marufu kuliko wengine wote.

Baada ya kifo cha Jim Brown mwaka 1992, Dudus ndiye aliyeonekana mtoto mwenye uwezo wa kuendesha genge la Shower Posse, kwa hiyo majukumu yote yalikabidhiwa kwake.

Hivyo, mpaka wakati huo, ilionekana Shower Posse bado ipo kwenye mikono salama ya familia ya Jim Brown baada ya Dudus kuchukua hatamu ya uongozi.

Rekodi mbalimbali zinamtaja Dudus kama mtu sahihi zaidi kuongoza genge la Shower Posse kwa sababu alifanikiwa kupita kwenye njia ambazo alipita baba yake (Jim Brown), hivyo kuufanya mtandao wao kuwa mkubwa zaidi.

Zaidi ni kwamba Dudus alifanikiwa kuusambaza mtandao wa Shower Posse katika maeneo ambayo hayakuwahi kufikiwa na baba yake. Matokeo ya jumla, yalimfanya Dudus kuwa mmoja wa viongozi wa magenge ya biashara ya dawa za kulevya, wenye nguvu zaidi duniani.

Moja ya mambo ambayo Dudus alionekana kupitia nyayo za baba yake ni ukarimu. Kwamba Jim Brown alikuwa mtoa misaada mkubwa kwenye jamii. Jim Brown aliwapa chakula wenye njaa, mavazi wasiokuwa na nguo, vilevile aliwasaidia makazi waliokuwa kwenye shida za maeneo ya kuishi.

Jim Brown aliwasaidia wanafunzi ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha kwa kuwalipia ada ili wasikose haki ya kielimu. Ni mambo hayo ambayo yaliwafanya watu wengi kumwona Dudus kuwa alikuwa na roho sawa na aliyokuwa nayo baba yake, kwani naye alikuwa mtoa misaa mkubwa kwenye jamii.

Dudus alipata nguvu kubwa kwenye mji wa Tivoli Gardens, yalipo makao makuu ya Shower Posse hadi kutamkwa kuwa kiongozi wa mji, ingawa haikuwa kwa sheria za nchi.

Ilimchukua miaka 18 Dudus akiendesha genge la Shower Posse, akiwindwa na Marekani kama ilivyokuwa baba yake bila mafanikio. Dudus aliongoza kisasa kuliko alivyokuwa Jim Brown.

Hata hivyo, mwaka 2010, Dudus alikamatwa na Marekani na mwaka 2012 alihukumiwa kifungo cha miaka 23 jela. Mpaka sasa Shower Posse wanaendelea na biashara kwa sababu ni mtandao mpana lakini bosi wao, yaani Dudus yupo jela.

Shower Posse kama ambavyo unatambulika kuwa mtandao mkubwa zaidi wa usafirishaji wa dawa za kulevya kutokea Jamaica, asili yake ni wanasiasa. Hivyo, chuki za siasa kama zikiachwa bila udhibiti madhara yake huwa ni makubwa mno.

Bila Jim Brown kupigwa risasi tano mwaka 1966, asingebadilika kitabia na kuwa mtu mbaya, mpaka kuunda genge la vijana wa ghetto ili naye aweze kuwa na nguvu kwenye jamii. Jim Brown alipigwa risasi katika vurugu za kisiasa.

Bila siasa Jim Brown asingepata nguvu za kuanzisha Shower Posse, kwani baada ya genge lake kukiwezesha chama cha JLP kushinda uchaguzi Jamaica na Edward Seaga kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo mwaka 1980, ndipo alipopata jeuri ya kujinatua na kusafirisha dawa za kulevya kwa jeuri kuwa asingebughudhiwa Jamaica, maana Serikali iliyokuwepo, aliiweka mwenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles