26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

NAMNA YA KUTAMBUA THAMANI ILIYOMO NDANI YAKO

Unavyoweza kutambua lengo linalokutofautisha na wengine

 

 

Na Christian Bwaya,

KIPAJI kinaweza kukutofautisha na watu wengine. Namna moja ya kukifahamu kipaji chako ni kujikagua kujua kitu unachokipenda. Kipimo kuwa unapenda kitu fulani ni utayari wako wa kukifanya bila malipo. Unaridhika tu kukifanya hata bure. Nikijitolea mfano mwenyewe, sisubiri kulipwa ili niandike. Navutiwa na maandishi.

Mwimbaji hali kadhalika maisha yake ni kuimba. Huhitaji kumlipa ili aimbe. Mwalimu naye huhitaji kumlipa ili akuelekeze kitu. Kufundisha ndiyo maisha yake. Wewe unavutiwa na nini? Lazima ukifahamu.

Kusema hivi haimaainishi tusilipwe kwa sababu tu tunapenda tunavyovifanya. Hapana. Tunachokisema ni kupenda kitu kwa dhati kabisa.

Labda mpaka hapa bado huelewa unavutiwa na nini. Nikupe kipimo kingine. Hebu  fikiria watu maarufu wanaokuvutia. Nani unampenda? Mimi nawapenda wengi. Mmoja wao anaitwa Rick Warren. Nimejifunza vingi kwake. Mwingine Stephen Covey. Kuna vitu vinanivutia kwa hao wawili.

Hiyo ndiyo njia rahisi ya kujua unachokipenda. Usiishie kusema nampenda fulani. Nenda hatua moja mbele. Tafuta sababu kwa nini unawapenda watu hao. Kwa mfano mimi hao jamaa niliyokutajia nawapenda kwa sababu ya namna wanavyoyachukulia maisha.

Na wewe lazima ujiulize kwanini unavutiwa na hao uliowafikiria hapo juu. Hicho kinachokuvutia kinaweza kuwa ni sehemu ya kitu unachokipenda kwenye maisha. Huo ndio wito wako.

Uridhika na nini?

Kwa kuwa zipo sababu nyingi zinaweza kukufanya ukavutiwa na kitu lazima kuongeza kipimo cha kupima udhati wa msukumo ulio ndani yako. Hapa tunazungumzia kuchukua hatua ngumu lakini zinakufanya unaridhika.

Kuridhika ni kujisikia utoshelevu na kitu unachokifanya. Hapa hatuzungumzii utoshelevu wa kuwaridhisha watu. Hatuzungumzii kuamua kufanya kitu fulani unachojua kuna watu wanatarajia ukifanye wala hatuzungumzii msukumo wa kuridhisha watu unaowapenda.

Tunazungumzia msukumo wa kimaamuzi unaoanzia ndani yako kukushawishi kufanya vitu unavyodhani ni vya muhimu kwako bila kuangalia wengine wanasemaje. Hiki ndicho kipimo cha juu cha wito wako. Gharama ya kuijua tofauti yako na watu wengine.

Uamuzi huu mara nyingi ni yale yatakayobadili maisha yako. Mfano kuacha kazi na kubadili fani uliyosomea. Si jambo jepesi, inahitaji moyo. Fikiria mtu anayeweza kuamua kuacha kazi. Lazima awe na sababu kubwa kiasi cha kutokuwa na woga na changamoto zinazoweza kuambatana na uamuzi wake.

Uamuzi huu unaweza kuwa na changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza ni kupishana na hata kuachana na baadhi ya watu muhimu kwenye maisha yako. Mara nyingi si kila mtu atauelewa wito wako. Watu hawataelewa mantiki ya unachokifanya, watakuona kituko lakini ndani yako unajua unafanya kitu sahihi.

Hata hivyo, si mara zote unapouendea wito wako mambo yatakuwa mepesi. Unakumbana na changamoto nyingi lakini kama umeupambanua wito wako vizuri hutarudi nyuma hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani. Utaendelea kusimama imara huku ndani yako ukiwa na amani.

Kama bado hujaweza kufanya uamuzi mgumu kwenye maisha yako; kila mtu anaelewa kile unachokifanya, unapenda kufanya kitu kwa sababu tu wengi wanakipendekeza; unafanya kufanya kitu usichokipenda au unajaribu kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja, inawezekana kabisa bado hujautambua wito wako. 
Rudi ndani yako tafakari wito wako na ujielewe. Fanya uamuzi wa kuufuata wito wako. Ukifanya kitu ulichopaswa kukifanya, utakuwa mtu mwenye utoshelevu mkubwa. 

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles