Na Sheila Katikula,Mwanza
Waumini wa Dini ya Kiislam jijini Mwanza wameombwa kuweka utaratibu wa kutembelea vituo vya watoto yatima ili waweze kuwashika mkono kwa kutoa misaada mbalimbali kwa mashirika yanayolea watoto hao hasa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Wito huo umetolewa juzi na Sheikh wa Msikiti wa Ibadh uliopo jijini hapa, Nouh Mousa wakati alipotembelea kituo cha Sos Children’s Village Mwanza kilichopo jijini hapa wilayani Nyamagana kinachotoa malezi na makuzi kwa watoto yatima kutoka maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Mousa alisema ni vyema wananchi kuweka utaratibu wa kutoa sadaka kwa watoto hao ambao wamepoteza wazazi wao ili kuweza kuwapa faraja na kuwapa moyo.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Shabab Daawat Islamiya, Ally Mbarak alisema lengo la kutembelea kituo hicho ni kuwatia moyo walezi ambao wanalea watoto hao ili waweze kutambua kuwa jamii inawathamini na kuwajali kwa kuona umuhimu wao.
“Tumekuja kuwapa moyo watoto hawa na walezi wao kwani ni jambo jema kumthamini mtu mwema ambaye anajali yatima hata mtume amesema atakuwa karibu na mja ambaye atakuwa karibu na atakaye msaidia mtoto yatima.
“Tumetoa sadaka yenye thamani ya sh milion 1Â vitume nunua vitu mbalimbali ukiwamo unga wa ngano, mafuta ya kupikia, chumvi, Sabuni, Mchele, sabuni za unga mifuko miwili, maharage, Sukari mifuko miwili tunaamini vitawasaidia kwa kipindi hiki na tunawaomba watu wengine watembelee kotio hiki,” alisema Mbarak.
Naye Afisa wa kituo cha Child and Youth Development, Masoud Hussein alisema kituo hicho kina watoto 85 wakiwemo wakike 37 na wakiume 48 na kina watoto wa umri wa miaka miwili hadi 15.
“Sisi tunafanya kazi na Serikali na watoto wao tunawapokea kutoka kwenye ofisi ya Ustawi wa jamii wanawafatilia kwa kina wapojilidhisha wanasifa za kuwaleta kwenye kituo chetu wanawaleta na sisi tunawapokea,” alisema Husein.
Kwa upande wake kiongozi wa wanawake wa kituo hicho, Apoche Mwenjesha aliwashrukuru viongozi hao kwa kuona umuhimu wa kuwatembelea watoto hao ambao ni yatima kwani kutoa si utajili bali ni moyo wenye kuamini na kujali.