26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Wahitimu NIT watakiwa kugeuza changamoto kuwa fursa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), Profesa Sylivester Mpanduji amewataka wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kugeuza changamoto zilizopo kwenye jamii na kuwa fursa ya kujiajiri badala ya kufikiria kuajiriwa.

Profesa Mpanduji alikuwa akizungumza katika kongamano la saba la wanajumuiya wa NIT ambapo mada kuu ilihusu mchango wa vituo vya ubunifu na uatamizi katika ukuzaji na uendelezaji wa viwanda nchini.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa, akimpongeza mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri

Akitoa mada kuhusu uzoefu wa Sido katika kuanzisha na kukuza viwanda nchini, amesema wanawasaidia vijana wenye nia ya kuanzisha viwanda kuhakikisha hawaendi kuajiriwa bali wanakwenda kutengeneza ajira.

“Tunatoa mafunzo ya ujasiriamali, tunatoa mikopo tunataka vijana wasitegemee kwenda kuajiriwa tu kwani wanaweza kujiajiri kutokana na ujuzi walioupata, wasifikirie tu kufanya kazi Tanzania kuna nafasi nyingi hata Afrika Mashariki na kwingineko duniani,” amesema Profesa Mpanduji.

Amesema pia hivi sasa wanalazimika kushiriki katika kila maonyesho yanayoandaliwa ili kuwaibua vijana na kuwasaidia kuanzisha viwanda na kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa Madundo Mtambo, amesema wamekuwa wakipokea wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na wengi wanafanya vizuri.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda Tanzania (TIRDO), Profesa Madundo Mtambo, akijibu maswali mbalimbali ya washiriki wakati wa kongamano la saba la kitaaluma la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)

“Tunaye kijana ambaye amegundua mashine ya kubangua korosho, huyu ni ‘intern’ ni injinia, wako wengi tu ambao wamefanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali,” amesema Profesa Mtambo.

Profesa Mtambo ambaye alikuwa akitoa mada kuhusu mchango wa utafiti katika ukuzaji na uendelezaji viwanda nchini, amesema mkakati wa matumizi ya gesi kwenye viwanda utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuvifanya viwanda viwe na ufanisi mkubwa.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa, amesema wanajivunia kutoa wataalam katika sekta ya usafirishaji ambao wanafanya vizuri sokoni.

Kuhusu mafunzo ya usafiri wa anga amesema yanasimamiwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) hivyo wanaamini wahitimu watakuwa na uwezo wa kushindana wanapoingia kwenye soko.

“Mafunzo haya kwa muda mrefu yamekuwa yakitolewa nje ya nchi na kumsomesha mhandisi nje ya nchi unatakiwa ujiandae karibu milioni 200 ndiyo anaweza akahitimu na kufanya kazi, je ni Watanzania wangapi wanaoweza kumsomesha mtoto wao kwa milioni 200? Hivyo kwa kuanza kuyafundisha hapa nchini tunaamini kwamba idadi ya wataalamu itaongezeka,” amesema Profesa Mganilwa.

Mmoja wa wahitimu wa Stashahada ya Uhandisi wa Mitambo, Mohamed Athuman, amesema ataibadili elimu aliyoipata na kuwa fursa.

Mhitimu mwingine wa Stashahada ya Uhandisi wa Magari, Joseph Mwijage amesema; “Nchi yetu imejikita katika uchumi wa viwanda na bila usafirishaji haviwezi kufika, tutatumia taaluma tuliyoipata ili kukuza sekta yetu na kuwashawishi wengine wanaotamani kuingia katika sekta hii kujifunza katika njia ambayo ni rasmi.

Katika kongamano hilo chuo hicho kwa kushirikiana na walimu pamoja na wadau kutoka katika kampuni na taasisi mbalimbali waliwazawadia wanafunzi waliofanya vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles