27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wahariri wamshukia Serukamba

peter-serukamba2Na LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limemshutumu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba, kwamba ni kikwazo katika mchakato wa kufanikisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016.

Wamesema   Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CCM, anaharakisha muswada huo uwasilishwe bungeni wakati akijua wadau wa habari hawajauchangia ikizingatiwa kamati hiyo ilitoa muda mfupi kwa wadau hao.

Shutuma hizo zilitolewa   Dar es Salaam jana na wadau hao walipokuwa wakizungumza katika mkutano wao wa kupitia na kujadili muswada huo kifungu kwa kifungu.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TEF, Jesse Kwayu, alisema Serukamba amekuwa akiongoza kamati hiyo kama sehemu ya Serikali ingawa hatakiwi kufanya hivyo.

“Serukamba ndiye tatizo kubwa katika muswada huu kwa sababu analazimisha mjadala uendelee licha ya kutambua kuwa bado unahitaji michango zaidi ya wadau.

“Hata tulipokutana Dodoma hivi karibuni kujadili muswada huo, alituambia wazi wazi kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

“Pamoja na msimamo wake huo, sisi hoja yetu itaendelea kuwa ile ile, kwamba tunaomba muda zaidi wa wadau kutoa maoni yao muswada uwasilishwe katika Bunge la Februari mwakani.

“Katika hili, idadi kubwa ya waandishi wako mikoani na hadi sasa wanalalamika kuwa hawajapata muda wa kukaa na kuusoma muswada huo na kuuelewa ili watoe maoni yao.

“Waandishi hawa ndiyo walengwa wakuu  lakini hawajapeleka maoni yao. Ni kweli Serukamba kavuruga mchakato, nasema, naamini ametumwa ndiyo maana anasema ni mzuri na wanataka kuweka historia.

“Ni kweli wanataka kuweka historia ya kupitisha sheria mbaya kuwahi kutokea katika historia ya dunia, ndiyo maana analazimisha muswada uende kama anavyotaka,” alisema Kwayu ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa jukwaa hilo, Absalom Kibanda, alimtaka Rais Dk. John Magufuli, amtumbue Serukamba, akisema ni jipu linalotakiwa kutumbuliwa.

“Katika hili Rais Magufuli naomba aniamini kwa sababu namfahamu Serukamba kwa muda mrefu.

“Narudia tena, huyu Serukamba ni jipu  kwa sababu ana tabia ya kung’anganiza mambo yasiyofaa kwa kusema ni mazuri.

“Kwa mfano, ule muswada wa awali wa huduma za habari enzi za Waziri Dk. Fenela Mukangala, alionekana akiuunga mkono wakati ulikuwa muswada mbaya zaidi.

“Kwa hiyo, sishangai kumuona aking’ang’ania muswada mbovu kwa kuutetea kuwa ni mzuri. Huyu jamaa amekuwa na tabia ya kuzungumzia muswada huo kana kwamba yeye ndiye waziri wa habari.

“Yaani ningekuwa na uwezo, ningemuomba Rais Magufuli atoe agizo la kuondolewa muswada huo usijadiliwe katika Bunge linalotarajiwa kuanza kesho (leo) mkoani Dodoma.

“Serukamba anadiriki kusema wadau mbalimbali kama TLS na Twaweza wamepeleka maoni na watayatumia hayo, lakini atambue suala la habari lina wadau wake muhimu ambao ni waandishi wa haabri.

“Hivi kama unataka maoni kwenye famila yako, unaweza kupeleka maoni ya mtoto wa jirani yako ukamwacha mwanao?

“Au kama unataka maoni kwa ajili ya Tanzania, unaweza ukachukua maoni kutoka Kenya, Burundi, Rwanda au Malawi halafu ukasema ni maoni ya Watanzania?  Hapa amekiuka misingi kama mbunge,”alisisitiza Kibanda.

Katika maelezo yake, Kibanda aliyataja majipu mengine kuwa ni baadhi ya watendaji wa Serikali wanaotaka muswada huo upitishwe kama ulivyo kwa kuwa wanawachukia waandishi wa habari.

“Majipu mengine ni baadhi ya watendaji wa Serikali wanaomsukuma waziri kupitisha muswada huo na wanawachukulia waandishi kama wahalifu.

“Ukiangalia ule muswada, hakuna sehemu wanakosema mwandishi atafanya kazi kwa uhuru, yaani hao nao ni majipu kwa sababu hawa wanawaona waandishi kama maadui,” alisisitiza Kibanda.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, alimtaka Serukamba na viongozi wengine wanaotetea muswada huo, waangalie historia ya baadhi ya viongozi duniani waliowahi kupitisha sheria mbaya wakati wakiwa madarakani na baadaye sheria hizo zikaja kuwaumiza baada ya kuondoka madarakani.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, alisema kuna baadhi ya waandishi wa habari, wamekutana na viongozi wa Serikali kwa ajili ya kuhakikisha muswada huo unawasilishwa na kupitishwa kama ulivyo.

Wadau wa habari wamekuwa wakiulalamikia muswada huo uliowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni Septemba 16 mwaka huu wakisema unahitaji muda mrefu wa kuujadili kwa kuwa una dalili za kuua vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Pamoja na wadau hao kuupinga, ratiba ya Bunge linaloanza leo mjini Dodoma, inaonyesha utawasilishwa Ijumaa wiki hii kabla ya kuanza kujadiliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles