31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majina mapya yachomoza u-DCI

kamishina-robertNa Mwandishi Wetu

SIKU tatu baada ya Rais Dk. John Magufuli  kutengua nafasi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, majina mapya matatu yamechomoza kurithi nafasi hiyo.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata jijini Dar es Salaam jana, zinasema mbali ya majina hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amemteua Mkuu wa Intelejensia, Kamishina Robert Boaz kukaimu nafasi hiyo tangu jana.

“Ni kweli afande IGP Mangu, amemteua Boaz kukaimu nafasi hii baada ya kuondolewa Diwani…tunaamini ni mtu sahihi katika nafasi hii.

“Kutokana na uwezo wake wa kuwa mwanasheria, afande IGP hapa hajakosea nafasi inastahili mtu ambaye amebobea katika masuala ya intelejensia kama huyu,”kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema hadi jana mchana, majina mapya yalikuwa yamechomoza kurithi nafasi hiyo, huku yakifanywa kuwa siri.

Kamishina Boaz anaelezwa kuwa amebobea zaidi katika masula ya upelelezi, kwani katika mikoa ambayo amewahi kuwa kamanda wa polisi, aliongoza kwa mafanikio makubwa.

Akiwa mkoani Arusha, Kamishina Boaz aliweza kupambana na njia haramu za magendo, uingizaji wa dawa za kulevya, bangi na matukio makubwa ya uhalifu  ambayo yalikuwa yameshamiri katika mitaa mbalimbali.

Majina hayo, ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Camilius Wambura, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC), Naibu Kamishna wa Polisi, Charles Mkumbo na Boaz.

Julai, mwaka huu, Wambura alikuwa miongoni mwa maofisa 34 walipandishwa  cheo  kutoka Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP).

Akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Wambura aliweza kupambana na mitandao ya ujambazi na kila aina ya uhalifu, jambo lililomjengea umaarufu mkubwa.

“Tangu jana asubuhi wakubwa walikuwa kwenye vikao vya suala hili, kati ya majina haya ndiyo yanaweza kupelekwa  ngazi za juu kuanza mchakato wa uteuzi,” kilisema chanzo chetu.

MTANZANIA lilipomtafuta IGP Mangu kuzungumzia suala la kukaimishwa Kamishina Boaz alisema suala la uteuzi si jambo la siri.

Alisema utenguzi na uteuzi wa nafasi hiyo huwekwa wazi, hivyo mwandishi anapswa kuwa na subira hadi itakapotangazwa rasmi.

“Suala la kutengua na kuteua DCI au kaimu siyo siri na mimi hizo taarifa unazosema umezisikia kuna uteuzi mimi sizijui, mpigigie msemaji wa jeshi la polisi akupe ufafanuzi,” alisema Mangu na kukata simu.

Jitihada za gazeti hili kumpata Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba ziligonga mwamba, baada ya simu yake kuita bila kupokewa.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Diwani ambaye alidumu kwenye nafasi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne.

Baada ya kuondolewa, ilielezwa kuwa Diwani atapangiwa kazi nyingine, ingawa hadi sasa hakuna sababu zilizotolewa juu ya kuondolewa kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles