Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya uteuzi wa majina ya wagombea uenyekiti wa wilaya sita.
Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho tawala kufuta uchaguzi kwenye wilaya hizo hivi karibuni.
Wilaya ambazo uchaguzi wake ulifutwa ni Moshi Mjini, Hai, Siha, Makete, Musoma Mjini na Musoma Vijijini.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na CCM jana na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ilieleza kuwa Kamati Kuu ya chama hicho kwa niaba ya Halmashauri Kuu imeteua majina ya wagombea katika Wilaya ya Hai ambayo ni ya Abdulah Mriri, Magai Maganda na Justice Masawe.
Kwa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro walioteuliwa ni Justice Mkita, Wilfred Mossi na Humfrey Nnko, huku Wilaya ya Moshi Mjini walioteuliwa ni Absalom Mwakyoma, Joseph Mtui, Faraji Swai na Alhaji Omar Amin Shamba.
Kwa Wilaya ya Makete walioteuliwa ni Aida Chengula, Mwawite Njajilo na Onna Nkwama; Wilaya ya Musoma Mjini ni Robert Sylvester, Magiri Maregesi, Amina Nyamgambwa na Daud Misango.
Polepole alisema kwa upande wa Musoma Vijijini walioteuliwa ni Gerald Kasonyi, Kananda Hamisi Kananda na Nyabukika Bwire Nyabukika.
Katika taarifa hiyo Polepole alisema Kamati Kuu imeagiza mikutano mikuu ya uchaguzi ya wilaya za Makete, Musoma Vijijini na Musoma Mjini ifanyike Novemba 25 na 26,2017.
Huku kwa wilaya za Moshi Mjini, Hai na Siha mikutano hiyo itafanyika Desemba Mosi na 2, 2017