25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WASOMI WATAJA VIKWAZO TANZANIA YA VIWANDA

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WASOMI, wadau na viongozi mbalimbali wa Serikali nchini wametaja vikwazo vinavyoweza kuikwamisha Tanzania kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Walisema Tanzania haiwezi kufikia azma yake hiyo kama haitawezesha wananchi kupata elimu inayowawezesha kujitegemea na kuwawezesha kuendana na mahitaji ya soko la ajira duniani.

Akiwasilisha mada katika mdahalo wa kujadili mfumo wa elimu nchini kuelekea Tanzania ya viwanda, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mkandala, alivitaja vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini.

Alisema pamoja na Serikali kufanya ugatuzi wa majukumu katika sekta ya elimu na mafunzo kutoka Serikali Kuu kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha ufanisi bado kumekuwa na changamoto ya mwingiliano wa baadhi ya majukumu katika utekelezaji kwa upande wa utendaji na usimamizi wa elimu katika ya pande hizo mbili.

Kuhusu hali ya ufundishaji alisema pamoja na mabadiliko mbalimbali ya mitaala kumekuwapo na changamoto katika utekelezaji wa miongozo iliyopo kwenye mitaala hiyo ambazo zimekuwa zikiathiri ubora na usawa katika elimu inayotolewa kwa ngazi mbalimbali.

“Mtaala unaotumika sasa wa mwaka 2005, unahitaji ufundishaji unaozingatia ujuzi kwa mwanafunzi kuwa mlengwa na mshiriki mkuu kwenye ufundishaji na ujifunzaji.

“Tafiti zinaonesha kuwa bado hali ya ufundishaji na ujifunzaji mashuleni katika ngazi zote unaendelea kwa kiasi kikubwa kuzingatia maarifa ya mwalimu anachukuliwa kuwa ndiye chanzo kikuu cha maarifa” alisema Profesa Makndala.

Alisema licha ya mtaala huo kusisitiza ujuzi na kutoa fursa kulingana bna uwezo, vipaji na vipawa bado umetawaliwa na muundo wa kuchuja wahitimu ili kupata wahitimu wachache wenye uwezo kitaaluma watakaoendelea ngazi za juu kama kipimo cha ubora wa elimu badala ya kutumia ujuzi na umahiri anaoupata baada ya kuhitimu.

“Dhana hii inapingana na ile ya elimu ya kujitegemea ambayo inashabihiana na mtaala huu wa sasa inayomuhitaji mhitimu kuwa mahiri katika ngazi yoyote anayomaliza na kuweza kujiajiri, vile vile, maarifa na ujuzi wa wanafunzi katika ngazi walizopo ni mdogo ikilinganishwa na ngazi ya elimu waliofikia

Aliongeza kuwa ujuzi wa wahitimu wa mafunzo wa ufundi na elimu ya juu nchini umebainika kutokidhi mahitaji wa ulimwengu wa kazi.

Alivitaja vikwazo vingine kuwa ni pamoja na mfumo wa uandaaji walimu, sifa za kujiunga na elimu ya ualimu, ubora wa mafunzo ya ualimu na sifa za wakufunzi wanaofundisha vyuo vya ualimu.

Murugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Hakielimu, John Kalage, alisema umefika wakati wa kuwa nan sera inayowaandaa wahitimu kujitegemea na endepo sera hiyo ipo iangaliwe kama inaendana na matakwa ya Taifa ya sasa.

“Elimu ya kujitegemea lazima iendane na mfumo wa siasa na uchumi wa nchi, mfumo wetu bado una changamoto tunazopaswa kuzibadili ili uwe na tija, tunaweza kuwa na viwanda lakini tunaandaa rasilimali watu wa kuendesha viwanda hivyo? Alihoji Kalage.

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alisema mfumo wa elimu nchini umekuwa na matatizo makubwa kwani wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawafahamu kusoma na kuandika ikilinganishwa na hapo awali ambapo mwanafunzi aliyekuwa akihitimu darasa la nne aliweza kufanya hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo, ili kujikomboa kiuchumi, kisiasa na kiitikadi ni lazima kuangalia aina ya maudhui na mifumo ya ufundishajiambayo yataunda mfumo wa elimu utakaoweza kulifikisha Taifa huko.

“Tunahakikisha vipi kwamba mfumo wetu wa elimu unazaa watu wenye vipaji vya ubunifu wa hali ya juu, ujuzi wa kutosheleza na kuwa na watu waliokombolewa kifikra ili nchi iondokane na dhoruba ya utegemezi wa muda mrefu” alisema Waziri Jaffo.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema wanafunzi wa Kitanzania wamekuwa na uwezo mkubwa wa kushika vitu wanavyofundishwa, hivyo ikiwa itatolewa elimu inayowawezesha kujitegemea watasadia kufikia uchumi wa viwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles