Jeremia Ernest, Zanzibar
Wageni kutoka nchi mbalimbali wameanza kumiminika visiwani Zanzibar kuhudhuria tamasha la Sauti za busara litakaloanza Februari 13 hadi 16, mwaka huu.
Tamasha hilo ni miongoni mwa matamasha makubwa duniani yanayokutanisha wasanii na watalii kutoka nchi mbalimbali kwa pamoja na kutumbuiza nyimbo tofauti zikiwamo za utamaduni.
Akizungumza na ukurasa huu meneja wa wa tamasha hilo Jouni Ramadhani, amesema imebaki wiki moja kuanza kwa tamasha wameanza kupokea wadau kutoka sehemu tofauti.
“Tamasha letu mwaka huu lina mwamko mkubwa tumeanza kupokea wadau kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanakuja kwa ajili ya kushuhudia msimu huu wa 17.
“Wasanii watakaotoa burudani wanatarajia kuingia studio Februari 10, kwa ajili ya kurekodi wimbo wa kupinga ukatili wa kijinsia ambao watautambulisha siku ya pili ya tamasha hilo,” amesema.
Kupitia tamasha hili, Zanzibar itanufaika kiuchumi hususani sekta ya utalii kutokana na wageni kutoka nchi tofauti kuhudhuria tamasha hilo.