31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yaijibu Marekani Tume huru ya Uchaguzi

Faraja Masinde, Dar es salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeujibu Ubalozi wa Marekani nchini kuhusu kuanzishwa kwa tume huru, ikisema ushauri uliotoa ni mawazo yao na kwamba tume iliyopo ni huru kwa mujibu wa sheria.

Januari 31 mwaka huu, Ubalozi wa Marekani nchini ulimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuahidi kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na haki, huku ukishauri kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.

Akizungumza jana na gazeti hili mara baada ya kumalizika mkutano wa tume hiyo uliowakutanisha wadau wa uchaguzi kwa Mkoa wa Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera, alisema ushauri uliotolewa na Marekani ni mawazo yao lakini haifanyi kuwaaminisha Watanzania wote kuwa tume hiyo si huru.

Dk. Mahera alisema pamoja na kwamba yeye hahusiki na hilo, lakini NEC imekuwa ikifanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni pasipo kuingiliwa.

 “Mimi sio msemaji wa hilo, lakini tunachotaka kusema ni kwamba tume yenyewe inafanya kazi kulingana na sheria zilizopo kwa sababu ndizo zitakazo turuhusu sisi kuendelea kufanya kazi.

“Suala hilo ni la kikatiba na suala la kisheria kwa hiyo ikibadilika sheria basi tume itafanya kazi kwa kuheshimu hizo sheria kwa kuwa huo ni mhimili mwingine..

Wakati Dk. Mahera akitoa kauli hiyo, juzi Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alimbana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa maswali bungeni akihoji ni lini Serikali itaunda tume huru ya uchaguzi, ambayo itafanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa huru na halali.

Akijibu swali hilo Majaliwa alisema: “Tume hii imeundwa kwa mujibu wa sheria na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote awe Rais wa nchi au chama chochote, chombo hiki kipo huru,”alisema Majaliwa.

TAARIFA YA MAREKANI

Katika taarifa yao Ubalozi wa Marekani iliyotolewa wiki iliyopita mbali na kumpongeza Rais Magufuli pia ilishauri kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.

Ubalozi huo pia ulieleza matarajio yao ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani ambao utawakutanisha wagombea wote kwa amani wakieleza mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.

“Tumetiwa moyo sana na hakikisho lililotolewa na Rais Magufuli hapo la Januari mwaka huu, kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa huru wa haki na wenye uwazi pamoja na mwaliko wake kwa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa. 

“Tunatarajia uchaguzi ambao raia wote na wagombea wa vyama vyote wanaweza kukutana kwa amani, wakielezea mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.  

“Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura lenye uwazi, kuanzishwa kwa tume huru za uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kipindi kifupi,”ilisema taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani.

KAULI YA JPM

Januari 21 mwaka huu, Rais Magufuli katika hotuba yake kwenye hafla ya kukaribisha mwaka mpya aliyoiandaa kwa ajili ya mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwaeleza viongozi hao kuwa, wakati ukifika watakaribishwa kuja kushuhudia demokrasia Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli alisema “kama nilivyoeleza awali mwaka huu nchi yetu itafanya uhaguzi mkuu, zoezi la uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote, inayofuata misingi ya kidemokrasia kama yetu.

“Kwa hiyo basi Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na kama ilivyo kawaida yetu wakati ukifika tutazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi wetu ili kujionea jinsi nchi yetu inavyokomaa katika nyanja ya demokrasia,” alisema Rais Magufuli.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli iliwaibua viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani pamoja na wanaharakati, wakihoji uwezekano wa uchaguzi kuwa huru na haki bila kuwepo tume huru ya uchaguzi.

KUZUILIWA KWA MIKUTANO YA VYAMA

Mbali na hilo la Marekani, jana katika mkutano huo wa NEC na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam, akijibu swali la Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ilala, Dk. Makongoro Mahanga, juu ya kuzuiwa mikutano ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema tume hiyo haihusiki na hilo.

Katika hilo, Jaji Kaijage alisisitiza kuwa badala yake vyama hivyo vitumie mazingira hayo hayo kuweza kuwafikia wapiga kura wao.

“Vyama vya siasa kutokufanya mikutano ya siasa sisi haituhusu cha msingi watumie mbinu mbalimbali zilizopo kukutana na wanachama wao ili waweze kuwahamasisha wajitokeze katika zoezi la uandikishaji ili waweze kupiga kura.

“Lakini kuhusu mazingira ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwamba yanaweza kuathiri uchaguzi huu, niseme tu kwamba sisi tume hatujakasimiwa uchaguzi wa Tamisemi hivyo hatuwezi kulisemea.

“Lakini pia mbona tumekuwa na taarifa kutoka kwenye vyama hivyo wakieleza kuandikisha wanachama wengi,” alisema Jaji Kaijage.

Aidha akizungumzia kuhusu mkutano huo, Dk. Mahera alisema lengo ni kuhamasisha wadau hao ili kusaidia watu kuweza kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji.

 “Uboreshaji huu unalenga watu wenye umri wa miaka 18 kujiandiksiha katika daftari la wapiga kura pamoja na kuhudumia Watanzania ambao wamepoteza kadi zao na hata wale waliopoteza taarifa zao.

Alisema hadi sasa tayari zaidi ya mikoa 23 imefikia na zoezi hilo la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura huku mikoa ya Dar es Salaam na Pwani zoezi hilo likitarajiwa kuanza Februari 14 hadi 10, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles