26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga wanaswa na meno, nywele za albino

VALENTINO MLOWOLANA SHEILA KATIKULA, MWANZA
JESHI la Polisi mkoani Mwanza limewakamata waganga wa kienyeji 55 wakiwa na viungo vya binadamu vikiwamo meno na nywele vinavyodaiwa kuwa ni vya watu wenye albino.
Vitu vingine walivyokutwa navyo ni ngozi ya simba, nyumbu, mamba, vibuyu, njuga, vioo, shanga na debe tatu za bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema waganga hao walikamatwa katika wilaya za Mkoa wa Mwanza kwenye msako ulioanza juzi.
Alisema katika msako huo wamefanikiwa kuwakamata waganga hao wanaodaiwa kupiga ramli chonganishi zinazosababisha kuchochea matukio ya mauaji kwa albino na vikongwe.
“Katika msako wa Jeshi la Polisi ulioanza juzi tumefanikiwa kuwatia mbaroni waganga wa jadi 55 ambapo kati yao tumewakuta na nywele, meno za watu wenye albino waliouawa katika matukio tofauti mkoani hapa,” alisema Kamanda Mlowala.
Kamanda huyo wa Polisi alisema waganga hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ikiwamo kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria pamoja na viungo vya binadamu.
“Kama Jeshi la Polisi, tunashangaa kukuta nywele za albino na meno na vitu vingine vikiwa kwa waganga wa jadi wakati ni kinyume cha sheria, tutahakikisha wanatoa maelezo ya kina walivyopata vitu hivi.
“Tunatoa wito kwa waganga wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo wajisalimishe wenyewe kwani polisi wanaendelea na msako, tunaomba wananchi watoe ushirikiano kwetu ili kuondosha vitendo hivi kwa jamii,” alisema.
Mbali na tukio hilo, taarifa kutoka wilayani Misungwi zinaeleza kuwa watu wanne wamefikishwa kortini mjini hapa kwa tuhuma za kuuza mafuta maalumu ya ngozi yanayotumiwa na watu wenye albino.
Mafuta hayo yenye thamani ya Sh milioni tano, ambayo yalitolewa na Hospitali ya Bugando kwa watoto wenye albino wilayani humo.
Wakati huo huo, polisi jijini humo linawashikilia wahamiaji haramu sita ambao ni raia wa Ethiopia waliokuwa wamehifadhiwa kwenye nyumba ya Richard Juma mkazi wa Nyambiti (18) jijini Mwanza.
Wahamiaji hao ni Alam Lameho (21), Tinsahel Digala (28), Mustapha Rashid (28), Liejau Baiyana (25), Tarigasa Atupia (25) na Baiyan Abdiligadri (25). Kamanda Mlowola alisema wahamiaji hao tayari wamefikishwa Idara ya Uhamiaji kwa hatua za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles