26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Jalada kesi ya Zitto laitwa kwa Jaji Kiongozi

kabweNa Mwandishi Wetu, Dar es Salam
SAKATA la kufukuzwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), limechukua sura mpya baada ya Jaji Kiongozi, Shabani Lila kuitisha jalada la kesi yake hali inayoonyesha kupitiwa upya kwa kesi hiyo.
Wiki hii Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi la Zitto la kutaka Kamati Kuu ya Chadema kutomjadili na hatimaye kumfukuza uanachama wake baada ya makada wenzake, Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha na Profesa Kitila Mkumbo kufukuzwa uanachama Desemba 2013.
Akieleza hukumu hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema, Tundu Lissu, alisema kutokana na hukumu hiyo na kulingana na Katiba ya chama chao, Zitto amejifukuzisha uanachama.
Hata hivyo, akizungumza na MTANZANIA jana, Zitto alikiri kuwa na taarifa za jalada lake kuitishwa kwa Jaji Kiongozi huku akimtaka mwandishi kuwasiliana na wakili wake.
Mmoja wa mawakili wake, Emmanuel Mvula, alisema taarifa za jalada kuitwa kwa Jaji Kiongozi alizipata jana alipokwenda mahakamani kuchukua hukumu ya kesi hiyo.
“Tangu Mahakama Kuu imetoa hukumu tumekuwa tukifuatilia hukumu ikiwa pamoja na kulipia. Baada ya kulipia ilitakiwa hukumu hiyo ipitiwe na mwenendo mzima wa kesi pia uchapwe. Leo nilipokuja kuchukua hukumu nikaambiwa siwezi kupewa kwa sababu jalada limeitwa kwa Jaji Kiongozi,” alisema Mvula.
Alisema kuna kasoro nyingi zilizojitokeza katika kesi hiyo hali inayotia wasiwasi uhalali wa hukumu hiyo.
“Kuna walakini mwingi katika kesi hiyo, kwa sababu kwa mara ya kwanza ilitajwa Novemba 12, 2014 na ilisikilizwa na Msajili wa Mahakama kwa sababu Jaji (John) Utamwa alikwenda kwenye mkutano,” alisema Mvula na kuongeza:
“Iliamuliwa kuwa kesi itasikilizwa tena Machi 12. Kuanzia hapo hatukuelewa kilichoendelea tena. Lakini kumbukumbu zinaonyesha kuwa kesi ilitajwa tena Februari 25 na uamuzi umefanyika Machi 10 bila sisi kuwapo.”
Alisema kuna utata wa jinsi wakili wa Chadema, Peter Kibatala alivyopata wito wa mahakama bila wao kuupata.
“Mahakama ilimwagiza Kibatala kutuandikia barua ya wito, lakini hakutufikishia barua kwa kuwa barua yenyewe haionyeshi saini yetu ya kupokea,” alisema Mvula.
Alitaja kasoro nyingine kuwa ni kubadilishwa kwa Jaji Utamwa aliyekuwa akiendesha kesi hiyo na kupewa Jaji Richard Mziray bila wao kujulishwa.
“Kesi hii ilikuwa chini ya Jaji John Utamwa, ikahamishiwa kwa Jaji Mziray, ilibidi tuwe na taarifa. Tulidhani ikifika Machi 12 tutajulishwa, lakini haikufanyika,” alisema na kuongeza:
“Mahakama kama chombo cha kutoa haki kwa wananchi, lazima kiwe na uhakika na kuzingatia mwenendo wa kesi nyingine zilizopita. Lakini kama inashindwa kuwa hivyo tutakwenda wapi?”
Hata hivyo, alisema watatoa tamko rasmi la uamuzi wao baada ya kupata hukumu ya kesi hiyo na baada ya kuwasiliana na mteja wao Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles