26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali ya Iringa kutua bungeni

GRACE SHITUNDU, DAR NA RAYMOND MINJA, IRINGA
MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ametangaza azma yake ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu matukio ya ajali nchini ikiwamo iliyotokea juzi mkoani Iringa.
Mbatia amesema lengo la kuwasilisha hoja hiyo ni kuhakikisha watendaji waliosababisha ajali hiyo kwa namna yoyote wanawajibishwa na kufikishwa mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema mashuhuda wa ajali wamesema chanzo ni shimo lililokuwa barabarani na mwendo kasi.
Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema kutokana na sababu hizo ni lazima Serikali itoe taarifa ya kina ili watendaji ambao wanahusika kwa namna yoyote wawajibishwe kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Ajali hii ni lazima iwawajibishe watu kwani imekuwa ikionekana ni jambo la kawaida tu kila inapotokea ajali na watu wanaishia kusema pole, huku baadhi ya familia zikiwa zimepoteza watu waliokuwa wakiwategemea.
“Mimi sitolifumbia macho suala hili na ninaamini kwamba kuna wabunge ambao wataniunga mkono, kwani eneo lilipotokea ajali kuna uongozi wa ngazi ya chini hadi mkoa na shimo hilo lilikuwapo na walikuwa wanaliona, hivyo hatuwezi kusema ajali hii ni Mungu kapanga,” alisema Mbatia.
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mhandisi wa masuala ya majanga na mipango miji, alisema hata kama taarifa itaonyesha kuna waziri anatakiwa kuwajibika, itabidi afanye hivyo ili kukomesha matukio ya ajali yanayoweza kudhibitiwa mapema.
Alisema Serikali iangalie upya sheria na utoaji wa leseni kwa madereva kwani wengi wanaonekana ni wazembe na wanasababisha ajali kwa mambo mengi yakiwamo ya ulevi na utoaji wa rushwa uliokithiri.
Mbatia alisema pamoja na tukio hilo kubwa kutokea, Serikali haijatoa tamko lolote hali inayoonyesha kuna ubaguzi hata kwenye matatizo.

MAITI WAONGEZEKA
Taarifa kutoka mkoani Iringa zinaeleza kuwa watu wanane wamefariki na kufikia maiti 50 hadi kufikia jana.
Katika ajali hiyo iliyotokea juzi Kijiji cha Changalawe, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa ikihusisha basi la Majinjah Express, watu 42 walifariki dunia papo hapo.
Basi hilo lenye namba za usajili T 438 CDE mali ya Kampuni ya Majinjah Express lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, liligongana na lori lilobeba kontena ambalo lililiangukia. Lori hilo lilikuwa limebeba mbao likitoka Iringa kuelekea nchini Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema kati ya majeruhi, tisa waliokuwa na hali mbaya wamehamishiwa hospitali ya mkoa.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, ilieleza kuwa baada ya kutokea kwa ajali hiyo maiti wengine wanane walipelekwa katika hospitali ya mkoa badala ya wilaya.
Alisema kutokana na maiti hizo, idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali hiyo imefikia 50 kwa sasa.
Marehemu waliotambuliwa na ndugu zao hadi sasa ni wanane na majina yao ni Mbezi Florence (29) mkazi wa Mbeya, Editha Ngunagwa (28) Mbeya, Mohamedi Hamadi (32) mkazi wa Mbeya, Ndenya Erick (25) ambaye alikuwa dereva wa basi hilo, James Kanyamaguho mkazi wa Morogoro, Ester Emmanuel (30) na Abuu Mangula mkazi wa Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles