27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waganga Wakuu imarisheni mifumo wa udhibiti-Dk. Gwajima

Na Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma

Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya,Wafawidhi na Maafisa Afya Mazingira nchini wametakiwa kuendelea kuimarisha mifumo yote ya udhibiti na kinga ya magonjwa kwa kushirikiana na wananchi ili kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima wakati akitoa ufafanuzi juu ya maswali ya wanahabari kuhusu kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza kwenye ukumbi wa wizara jijini Dodoma.

Dk. Gwajima amesema viongozi hao wanatakiwa kuwakumbusha wananchi kwenye elimu ambayo Wizara imekuwa ikiitoa ikiwemo kuimarisha usafi, kujifukiza, kufanya mazoezi, kula lishe bora, kunywa maji mengi bila kusahau matumizi ya tiba asili ambazo taifa hili limejaaliwa.

“Serikali itaendelea kuchukua tahadhari zote za ufuatiliaji wa mwenendo wa magonjwa yote kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote na kuendelea kuelimisha wananchi juu ya hatua za kuchukua,” amesisitiza Dk. Gwajima.

Aidha, Dk. Gwajima amesema wizara yake haina mpango wa kupokea Chanjo ya COVID-19 inayoripotiwa kuwepo na kutumika kwenye mataifa mengine kwani Serikali kupitia wizara ya afya inazo taratibu zake za kufuata pale inapotokea kupokea bidhaa yeyote ya afya na hufanyika baada ya Serikali kujiridhisha na sio vinginevyo.

Kwa upande wa Tiba Asili, Dk. Gwajima amesema Wizara kwa kushirikiana na Mkemia Mkuu wa Serikali , Baraza la Tiba Asili na wananchi wajuzi wa tiba asili tayari wameshafanya usajili wa bidhaa (dawa) za tiba asili, alizitaja miongoni mwa dawa hizo ni COVIDAL,NIMECAF,PLANET++,BINGWA na COVOTANXA.

Aliongeza bidhaa za mafuta tete ambayo imehakikiwa na Mkemia Mkuu kuwa ni salama na zinatumiwa na watu mbalimbali ni Uzima Herbal Drops, BUPIJI, EUCALYPTUS OIL, LEMONGRASS ESSENTIAL OIL na bidhaa zingine zitaendelea kutajwa na Baraza la Tiba Asili

“Uko ushahidi wa kutosha kabisa kuhusu watu wengi ambao wamepata nafuu na kupona magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyo ambukiza yaliyokuwa yanawasumbua mara baada ya kutumia dawa za tiba asili hata kama walikuwa kwenye matibabu mengine ya dawa za hospitali,” amesema Dk. Gwajima.

Hata hivyo Waziri huyo alilielekeza Baraza la Tiba Asili/Mbadala kutoa orodha ya dawa zote ambazo zimepita kwenye utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kimaabara ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuonekana kuwa matokeo ya awali ya uchunguzi ni salama kwa matumizi na kuwa dawa hizo zimekuwa zikitumiwa na watu wengi kwa muda mrefu na kuwaponya ama kupata nafuu.

Dk. Gwajima amewataka wataalamu wote na wajuzi wa tiba asili wasisite kujitokeza na kufuata taratibu za kuwasilisha dawa na bidhaa zao kwa mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali ili zifanyiwe uchunguzi wa kimaabara kabla ya kukabidhi taarifa ya matokeo ya uchunguzi Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel amesema Waziri amesisitiza kwenye kujikinga na hivyo Serikali imeboresha kwenye viwanja vya ndege,mipaka pamoja na sehemu za kupimia magonjwa mbalimbali ili yasiingie nchini kwa watu wanavyoingia na kutoka.

“Tiba asili sio jambo la leo,tumezaliwa tumeona akina mama zetu wanatumia baadhi ya majani kwa kutibu mafua au homa na kujifukiza na baada ya hapo wanatoka salama na kuendelea na kazi,hivyo tiba asili haijatokana na ugonjwa wa Corona bali ni kutoka enzi na enzi”.

Dk. Mollel amesema hatua za usafi zinatakiwa kuongezwa nguvu na kuwataka wataalamu wa afya kuacha kufikiria mgonjwa anavyoenda kwenye kituo cha afya anaumwa kifua ana Corona bali kuhakikisha wanampima vipimo vingine ili wasije kuuwa watu na mambo mengine ambayo hayana uhusiano na Corona.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles