25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wafungwa maisha kwa kuchoma kituo cha polisi

PATRICIA KIMELEMETA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha maisha jela watu wanane wanaodaiwa kuchoma Kituo cha Polisi Bunju kilichopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao ni aliyekuwa Mtendaji wa Kitongoji cha Bunju, Yusuph Saleh na Juma Ally, Baraka Marko, Abuu Juma, Rashid Awadh, Abraham Minga, Veronica Wambura na Ramadhan Said.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 10, 2015, katika eneo la Bunju baada ya daladala iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Mwenge na Bagamoyo kumgonga mwanafunzi, Tabia Omary (10), katika eneo hilo na kufariki papo hapo.  

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa moja mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema awali washtakiwa hao walikuwa 35, lakini kadiri kesi hiyo ilivyokua inaendelea, washtakiwa 17 waliachiwa baada ya kuonekana hawana hatia na kubaki 18.

Alisema upande wa Serikali uliwasilisha mashahidi 17 wakiwamo askari wa polisi wa Kituo cha Bunju, Kawe na Wazo ambao walikuwa kwenye eneo hilo wakati tukio likitokea, huku washtakiwa wakijitetea wenyewe kwa kudai kuwa hawajafanya tukio hilo na hawakuwepo wakati kituo kikichomwa.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo, ushahidi wa shahidi wa pili na wa 17 pamoja na kwenda kwenye eneo la kituo kilipochomwa, mahakama imejiridhisha pasi na shaka kuwa washtakiwa wanane wamehusika moja kwa moja na uchomaji wa kituo hicho.

Alisema washtakiwa hao walitenda kitendo cha kinyama kwa makusudi jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa pamoja na kusababisha hasara kwa Serikali kutokana na kituo cha polisi cha umma kuchomwa.

Alisema watuhumiwa walisababisha athari kwa wananchi wasio na hatia kutokana na kitendo cha kuchoma moto magari yaliyokuwa kwenye kituo hicho huku mengine yakivunjwa vioo.

 Alisema kwa kuzingatia kifungu namba 319 (a) cha kanuni ya adhabu, mahakama imewahukumu kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wananchi wengine wenye tabia kama hizo.

“Katika kipindi cha ushahidi, mahakama iliweza kufika kituoni hapo na kuona kilivyochomwa moto hadi kuwa majivu, ndani yake kulikuwa na silaha zilizokuwa zinatumiwa na polisi kituoni hapo, lakini katika kipindi cha ushahidi tulielezwa kuwa ndani kulikuwa na mahabusu na hata tulivyokwenda, tuliona damu imeganda kwenye eneo la kituo.

“Kutokana na hali hiyo, mahakama haiwezi kuvumilia hali hiyo, imewahukumu watu wanane kwenda jela kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuchukua sheria mkononi,” alisema Hakimu Simba.

Alisema katika tukio hilo, wananchi hao walirusha mawe na kuvunja vioo vya magari ya watu na kufanya uharibifu mwingine jambo ambalo lilisababisha kuongezeka kwa taharuki.

Alisema kuonekana kwa kitendo hicho kimeonyesha pasi na shaka kuwa wananchi hao walidhamiria kuchoma kituo hicho pamoja na mali zote zilizokuwa eneo hilo licha ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, kufika eneo la tukio na kuwatuliza lakini waliendelea kukaidi.

Alisema wakati tukio hilo linatokea, kulikuwa na askari mmoja ambaye baada ya kuona wananchi wana hasira na wameshika silaha, alikimbia na kujificha ili kuokoa uhai wake kwa sababu wangeweza kumdhuru.

Alisema shahidi wa pili katika kesi hiyo, SSP Idd Omary, ambaye alikuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kawe, alifika katika eneo hilo akiwa na askari 18 ili kutuliza ghasia na kumpa spika Mtendaji wa Kitongoji hicho, Yusuph Saleh, ili aweze kutuliza ghasia, badala yake alitumia spika hiyo kuanza kuchochea vurugu.

“Mtendaji aliwashawishi wananchi kuendelea kufanya ghasia licha ya kuombwa na polisi kutuliza ghasia kwa wananchi wake, badala yake aliwaambia ‘hapa leo hakuna kulala mpaka kieleweke, endeleeni kukomaa’, huku akirudia mara kwa mara hali ambayo ilichochea vurugu,” alisema.

Alisema shahidi wa 17 ambaye ni kutoka kituo cha Zimamoto, aliieleza mahakama hiyo kuwa walipopewa taarifa za kuungua kwa kituo hicho, walifika eneo la tukio na kukuta asilimia 80 ya kituo kimeungua pamoja na mali zote zilizokuwa ndani zikiwamo silaha.

Alisema shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa katika eneo hilo hakukua na shoti yoyote ya umeme wala tatizo linaloweza kusababisha kituo kuungua, zaidi ya wananchi waliokuwa wamefurika huku wakipiga kelele za kutaka wawekewe matuta barabarani.

“Kama hakukua na shoti ya umeme kituo kitawezaje kujichoma chenyewe! Hivyo basi ushahidi unaonyesha wazi kuwa wananchi waliokuwa nje walihusika na wengine walikuwa wamebeba dumu la mafuta ya petroli,” alisema.

Awali kabla ya hukumu hiyo kusomwa, upande wa Serikali uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaopenda kuchukua sheria mkononi na kusababisha uharibifu wa mali za watu au za umma.

Wakili wa Serikali, Ester Martin, aliieleza mahakama kuwa kitendo hicho hakipaswi kuvumiliwa hata kidogo kwa sababu kinaweza kuleta madhara kwa wananchi wasio na hatia.

Mara baada ya Wakili Ester kuieleza mahakama hiyo, washtakiwa hao waliiomba mahakama kuwapa adhabu ya kifungo cha nje kwa madai kuwa wana familia zinawategemea na tayari walishatumikia mahabusu kipindi kirefu.

Wengine waachiwa

Mahakama hiyo pia jana iliwaachia huru washtakiwa wengine 10 waliokuwa kwenye kesi hiyo baada ya kuona hawana hatia.

Walioachiwa huru ni Mrisho Majaliwa, Hamis Ndege, Selemani Gwaya, Antony Mayunga, Ally Said, Mariam Hamza, Rehema Hussein, Rajab Said, Amina Juma na Aloyce Mpina.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka sita likiwamo la kufanya mkusanyiko usiokua na kibali huku shtaka la 2 hadi la 5 wanadaiwa kukusanyika katika kituo cha Polisi Bunju kwa nia ya kufanya makosa, kuharibu mali na kuteketeza kituo cha polisi.

Shtaka la sita wanadaiwa kuwa nje ya kituo cha polisi kulikuwa na magari ya wananchi ambapo washtakiwa hao wanadaiwa kupiga mawe na kuharibu magari hayo kinyume cha sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles