26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wafugaji nao kuandamana kumpongeza JPM

GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

MASHIRIKA na wadau wanaotetea wafugaji nchini, leo wanakusudia kufanya maandamano ya amani mjini Arusha kumpongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kutoa maagizo na maelekezo yenye kutetea wafugaji waliokuwa katika maeneo yanayopakana na mipaka.

Akitoa taarifa kwa niaba ya wadau hao,  Mbunge wa Simanjiro (CCM), James ole Millya, alisema wanampongeza Magufuli kwa kuwa kwa muda mrefu wafugaji wamenyanyaswa, kufukuzwa, kuchomewa mali na kutaifishwa mali zao katika maeneo yao wanayopakana na uhifadhi.

Alisema hatua ya kumpongeza imekuja baada ya Rais kutoa maelekezo yanayoonyesha kwamba anachukizwa kuona wafugaji wanafukuzwa kila mahali katika maeneo ya vijiji na vitongoji vinavyopakana na hifadhi.

“Wafugaji nchini kwa muda mrefu wamekuwa wakipata tabu na changamoto nyingi zinazotokana na kuondolewa kwa nguvu wakati mwingine kuharibiwa mali zao kwenye maeneo yao ambayo wamekuwepo kwa muda mrefu kwa kisingizio kuwa ni maeneo ya hifadhi. 

“Sisi kama viongozi wa wafugaji nchini tunazo taarifa nyingi za unyanyasaji wa wafugaji katika maeneo yao ambayo yamemegwa na hifadhi, kufukuzwa kwa wafugaji katika maeneo haya kwa muda mrefu imejenga taswira mbaya kwamba uhifadhi unafanywa bila weledi,” alisema.

Millya alisema wanampongeza Magufuli kwa kuyatambua vyema matatizo na manyanyaso wanayoyapata wafugaji katika maeneo yao yanayopakana na hifadhi.

“Tumekutana hapa kumpongeza Rais kwa kutoa maagizo kwa vyombo vya Serikali hususan Wizara ya Maliasili na Utalii na kuwataka kuhakikisha kuwa hakuna mfugaji atakayeondolewa katika kijiji au kitongoji chake kilichoainishwa kuwa katika maeneo ya uhifadhi.

“Pia kwa kuweka wazi bila kuficha kuwa anachukizwa kuona wafugaji wanafukuzwa kila mahali,” alisema Millya.

Pia aliwataka wafugaji kutoa ushirikiano na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kubaini maeneo yao kama ambavyo Magufuli ameagiza na kutolea maelekezo kwa vyombo vya Serikali.

Pia aliwataka wafugaji kutovamia maeneo ya uhifadhi na wabaki katika maeneo yao ya asili kama walivyoishi kwa muda mrefu hata kabla ya mipaka kuwekwa.

Aliiomba Wizara ya Ardhi, Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi nyingine za Serikali kutekeleza maagizo ya Magufuli kwa haraka bila kuchelewa.

Alisema ni vyema vyombo hivyo vikahakikisha wananchi wanashirikishwa kwa uwazi katika mchakato huo ili kusiwe na mfugaji atakayeondolewa katika maeneo yaliyoanishwa.

“Tunatoa wito kwa vyombo vya Serikali hususan Wizara ya Ardhi, Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi nyingine za Serikali kujaribu kujenga uhusiano mzuri baina ya wafugaji na maeneo ya uhifadhi na kuhakikisha kuwa wafugaji wananufaika na ujirani mwema wa kuwa karibu na maeneo ya uhifadhi nchini,” alisema Millya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles