Na Clara Matimo, Mwanza
Baadhi ya wafuasi wa Chama cha CHADEMA jijini Mwanza wamekusanyika katika ofisi za chama hicho Kanda ya Viktoria na kufanya maombi kwa ajili ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Maombi hayo yameongozwa na Askofu wa Kanisa la Evangelical Pentecostal Restoration(EPRC) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Mkoa wa Mwanza, Amos Hulilo.
Akizungumza kabla ya kuanza maombi, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mbutusyo Mwakihaba, amesema wamekusanyika kwa ajili ya maombi na si kuvunja amani maana wanaamini Mwenyekiti wao hana hatia kwa shauri linalomkabili ambalo ndani yake kuna shitaka la ugaidi hivyo wanamuomba Mungu akatamalaki katika kesi hiyo.
“Lengo la maombi ni kumuomba Mwenyezi Mungu awakumbushe kutenda haki na weledi waliosomea viongozi wote wanaofanya kazi ndani ya vyombo vyote vya ulinzi na usalama, sheria na watu wote wanao toa haki, watende haki si tu kwa wanachama wa chadema bali kwa wananchi wenye tuhuma mbalimbali mtu akifikishwa mahakamani afikishwe kwa tuhuma za kweli,” amesema Mwakihaba.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Jimbo la Nyamagana, Hyasinta Wanchelele, amesema wanaamini mamlaka zote zinatoka kwa Mungu ndiyo maana wamefanya maombi hayo wakimsihi Mungu awakumbushe watawala kutumika kwa haki ili kuepuka mipasuko miongoni mwa watanzania.
Amesema watanzania waliishi kama ndugu hawakutengenezeana visasi kutokana na misingi imara ya upendo, umoja na mshikamano aliyoijenga Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Biblia Takatifu kitabu cha Yeremia 1:7 Mungu anasema kabla sijakuumba nalikujua kabla sijakutoa tumboni mwa mama yako nalikutakasa ili ukawe nabii na mfalme wa mataifa.
“Kwa hiyo kama Mungu alimuumba Mbowe akampa mamlaka aje kuwatumikia watanzania kupitia Chadema tumeona tuje tumuombe asimuache mwenye haki aendelee kuteseka, tunamlilia yeye aliyehakimu wa haki ashuke ahukumu kwa haki kutokana na tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wetu pamoja na viongozi wengine wapenda haki ndani ya taifa hili.
“Sisi sote ni watanzania hakuna aliyemkimbizi ndani ya taifa hili kila mtu anayo nafasi ya kuongoza kadri Mungu alivyomkusudia, tunapozuia makusudi ya Mungu juu ya wanadamu aliyowaumba tunakuwa tumemkosea inamaana tunamkosoa, tusifike mahali tukaingilia nafasi ya Mungu tumpe nafasi afanye kazi kama alivyokusudia juu ya watu wake,”amesema Hyasinta.
Akizungumza na wafuasi hao kabla ya kuanza maombi, Askofu Hulilo amesema ili nchi idumu katika amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, Mungu ampe hekima na washauri wema ambao watamshauri vizuri.
“Nafasi aliyonayo rais ni kubwa anaongoza wanaompenda na wasiompenda, wanachama wa vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini na watanzania wenye dini mbalimbali, tuliombee pia taifa letu ili liwe na amani matukio ya kuuwana, kukamatana na kuchukiana yanasababisha mgawanyiko miongoni mwa watanzania.
“Ukisoma Biblia Takatifu kitabu cha Mithali 14:34 inasema haki huinua taifa dhambi ni aibu ya watu wote. Kwa hiyo tuombe bila kuchoka ili viongozi wetu wa taifa hili watende haki Mungu aliinue taifa letu,”amesema.