Na Sheila Katikula, Mwanza
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amewataka wafanyakazi wa sekta ya Uchukuzi kujiepusha na vitendo vya rushwa ili waweze kufanya kazi kwa wajibu na weledi kwa kushirikiana.
Hayo aliyasema jana wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta hiyo jiini hapa wenye lengo la kujadili utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, utawala na wajibu wa wafanyakazi.
Alisema kuna aina nyingi za kuomba rushwa kwa mfano kuomba zawadi , fedha, mapenzi na kuwanyima watu haki, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu kufanya hivyo ni kosa na ikibainika sheria zitachukuliwa.
Alisema ni vema kila mtu kukemea, kujiepusha, kupinga vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki siyo vizuri watendaji wabovu na walioshindikana kuonewa aibu.
“Kila mmoja wenu kuwa mshiriki mkubwa wa kupambana na rushwa kwani bado kuna viashiria vya vitendo hivyo katika maeneo yenu kwani hatutavumilia pindi tutakapi baini kuna watu wanafanya,” alisema Chamuriho.
Alipongeza kuwa mtumishi anawajibu wa kufanya kazi kwa weledi kwa kushirikiana ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo siyo kufanya kwa mazoea.
Alisema hawatasita kuchukua hatua pale watakapobaini mazoea yanawekwa mbele badala ya weledi katika utendaji wa kazi.
Aliongeza kuwa ni lazima wajibu uambatane na uelewa wa majukumu ya kila mmoja pamoja na uhusiano mwema kazini Kati ya viongozi na wafanyakazi.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa sekta hiyo, Gabriel Migire alisema katika mpango wa watatu unaoendelea kuandaliwa wa maendeleo ya taifa sekita hiyo imepewa dhamana ya kutekeleza miradi ya kielelezo ikiwemo ujenzi wa reli ya Kati, uboreshwaji wa bandari ya Dar es Salaam na uimarishaji wa kampuni ya ndege Tanzania.
Alisema utekelezaji wa miradi hiyo unasimamiwa na wajumbe wa sekta hiyo hivyo amewaasa wajumbe hao kutekeleza miradi hiyo kwa ubora unaotakiwa na kulinda thamani ya fedha iliyowekezwa.
Naye Mjumbe kutoka Sekta ya Uchukuzi, Stella Katondo alisema atahakikisha wanafanya kazi kwa weledi na bidii ili waweze kukamilisha miradi iliyopo kwenye sekta hiyo.