NA BENJAMIN MASESE
JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoani Mwanza imewatangazia wafanyabiashara kutofunga maduka badala yake kungoja maelekezo ya vikao.
Akizungumza na gazeti jana, Mwenyekiti wa JWT mkoa wa Mwanza, Christopher Wambura, alisema wafanyabiashara hawatafunga maduka yao kwa kuwa vikao vinaendelea sasa.
Tamko la JWT limetolewa ikiwa ni siku moja baada ya TRA na polisi kutoa tangazo la kusisitiza matumizi ya mashine EFD’s.
TRA pia imewaonya wale wanaohamasisha kuwarubuni wafanyabiashara kutotumia mashine hizo.
Taarifa ya TRA na polisi imeonya watakaokiuka au kuhamasisha mgomo juu ya matumizi ya mashine ya EFD watachukuliwa hatua za sheria kwa kuwa ni kosa la jinai.
Wambura alisema wameanza vikao vya ndani kujadili jinsi ya kukabiliana na matakwa ya TRA na polisi kutumia mashine za EFD wakati bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa kama alivyoelekeza Rais Jakaya Kikwete Aprili 22, mwaka huu alipokuwa Karatu mkoani Arusha akifungua ofisi za TRA.
“Sisi hatuna nguvu ya kupambana na vyombo vya Serikali ambavyo vinavyotaka matumizi ya mashine hizo.
“Silaha tuliyobaki nayo ni umoja wetu kama ulivyoona jana (juzi) wafanyabiashara wa Dar es Salaam walifunga maduka yao.
“Hapa Mwanza tumewaeleza wasifunge maduka yao ila sisi viongozi tunaanza vikao vya ndani kupanga namna ya kupambana na matakwa ya TRA na polisi, siku tukitangaza mgomo utakuwa ni nchi nzima,”alisema.
Mgomo wa wafanyabiashara nchini dhidi ya mashine za EFD ulianza Desemba mwaka jana na umekuwa ukisimamishwa kwa muda huku Serikali ikifanya mazungumzo na wafanyabiashara hao ingawa hadi sasa haujapatikana mwafaka.