29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara wa sukari wapambana na Magufuli

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Mwenyekiti wa Bodi aibuka asema wemelenga kumkomoa

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

SASA ni wazi kwamba wafanyabiashara wa sukari nchini wameamua kuanzisha vita na Rais John Magufuli, kwa kuamua kuficha bidhaa hiyo na hivyo kuadimika katika soko na kupanda bei.

Hatua hiyo ya wafanyabiashara imekuja baada ya Rais Magufuli kutangaza utaratibu mpya hivi karibuni wa kutaka uagizwaji wa sukari kutoka nje ufanywe na wazalishaji wa bidhaa hiyo hatua ambayo inakata mrija wao wa ulaji.

Jana Bodi ya Sukari ililazimika kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kile walichokibaini baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa bidhaa hiyo imeadimika.

Akitoa tamko kwa niaba ya Bodi ya Sukari na wazalishaji bidhaa hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Ami Mpungwe, alisema tangu Rais Magufuli alipotangaza utaratibu mpya wa kuwatumia wazalishaji kuagiza sukari wamebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wameanza kufanya mipango ya kuhujumu taratibu hizo.

Alisema wafanyabiashara hao wameamua kuficha bidhaa hiyo ili kuwaaminisha wananchi kwamba sababu kubwa ya kuadimika kwa sukari inachangiwa na uamuzi huo wa rais.

Kabla ya uamuzi huo haujafikiwa na Rais Magufuli, wafanyabiashara wengi wa bidhaa hiyo walikuwa hawalipi kodi hali iliyochangia kufanya biashara hiyo kiholela huku wakipata faida nyingi na kuinyima mapato Serikali.

Hili linathibitishwa na kauli iliyotolewa na Mpungwe jana ambaye aliwanyooshea vidole waziwazi wafanyabiashara hao kwamba walikuwa wakinufaika na uingizaji holela wa sukari bila kulipia kodi na kwamba hata wanachokifanya sasa cha kupandisha bei ya sukari ni mbinu chafu ili kudhoofisha juhudi za Serikali za kuendeleza viwanda vya ndani kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi.

“Wameanzisha kampeni za kuwatia hofu wananchi wakiwaonyesha sukari imeadimika kutokana na agizo lililotolewa na Serikali la kudhibiti uingizaji sukari nchini,” alisema Mpungwe.

“Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuficha maghalani na kuendesha propaganda kwamba bei ya sukari imepanda na wapo waliopandisha kwa ghafla bei ya sukari kwa madai kwamba kuna upungufu viwandani na wengine wakiwalaghai watu kwamba bei wanayonunulia viwandani imepanda,” alisema Mpungwe na kusisitiza kuwa wanaofanya hujuma hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia utaratibu huu mpya alisema unafanyika kwa kuzingatia ulipaji kodi kwa sukari ya nje inayoingizwa nchini lakini pia umelenga kulinda viwanda vya sukari kwa kuimarisha soko la ndani.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya sukari nchini, alisema wazalishaji nchini wanatambua kwamba viwanda vyote vya wasambazaji vinauza sukari kati ya shilingi 1,700 na 1,800 kwa kilo na hakuna kilichopandisha bei tangu tamko la Rais lilipotoka.

“Hali ya uzalishaji sukari msimu huu 2015/2016 ni nzuri na msimu utafungwa Aprili kupisha matayarisho ya msimu mpya 2016/2017 Mei na Juni 2016 kama ilivyo taratibu kwa kila mwaka na viwanda vina akiba ya tani 32,000 za sukari inayoendelea kuuzwa,” alisema na kuongeza:

“Kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Moshi na kile cha Kagera vinaendelea kuzalisha sukari hadi Aprili 2016 na Serikali imeshatangaza utaratibu wa uagizaji wa sukari ambao utahakikisha sukari inayoruhusiwa kuingizwa nchini na kiasi kinachohitajika kuziba mahitaji ya wakati viwanda vinapokuwa vimefunga uzalishaji.”

Aliongeza kuwa kutokana na utaratibu huu mpya wa kuweka uwazi katika usimamizi wa bidhaa ya sukari, utasaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti sukari ya magendo na kuhakikisha inayoingia ni ile iliyoruhusiwa kwa kulipiwa kodi.

Mwenyekiti huyo alisema Bodi ya sukari na wazalishaji wanawahakikishia Watanzania kwamba hali ya upatikanaji wa sukari nchini ni nzuri na wao kwa kushirikiana na vyombo husika vya Serikali watahakikisha wanaendelea kuwa na sukari ya kutosha kwa muda wote.

KAULI YA RAIS MAGUFULI

Hivi karibuni Rais Magufuli alitoa kauli ya kupiga marufuku uingizwaji wa sukari kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje.

Rais huyo alisema Taifa haliwezi kufikia malengo yake ya kuimarisha viwanda vya ndani iwapo viwanda vya sukari nchini havitalindwa na kuwezeshwa dhidi ya uingizaji huo.

Rais Magufuli alielezea kuwepo kwa viwanda nchini ambavyo hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo na viwanda hivyo huzalisha sukari, lakini pia ajira ni chanzo cha mapato ya Serikali.

Alisema ingawa ipo hifadhi ya kutosha ya sukari lakini wapo watu serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje.

Aliwaelezea watu hao kama ni sehemu ya kukandamiza juhudi za Serikali hali iliyosababisha kuchukua hatua ya kuzuia utolewaji wa vibali kuruhusu uingizaji wa sukari, hadi itakapotokea mahitaji maalumu.

Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wamekuwa wakiingiza sukari nchini iliyoisha muda wake wa matumizi na haifai kutumiwa na binadamu.

Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 ambako tani 170,000 zinatumiwa kwa mahitaji ya nyumbani na nyingine iliyobaki hutumiwa viwandani.

Alisema viwanda vya hapa nchini vimekuwa vikizalisha tani 300,000 hali inayosababisha kuwepo kwa upungufu wa tani 290,000 kila mwaka kwa matumizi ya nyumbani na yale ya viwandani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles