23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri wahaha kujiokoa

kassimNA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

SAA chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwapa saa saba manaibu na mawaziri ambao wamekiuka sheria kwa kutojaza mali wanazozimiliki  viongozi hao jana walionekana wakipigana vikumbo katika ofisi hizo ili kuokoa nafasi wanazozishikilia.

Mawaziri hao ambao walikuwa  hawajajaza tamko la rasilimali na madeni na hati ya uadilifu za Sekretarieti ya  Maadili ya Viongozi wa Umma ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba ambao walikuwa hawajawasilisha fomu zote mbili.

Wengine ambao walikuwa wanadaiwa fomu moja moja na kujisalimisha wao wenyewe au kwa kuwatuma wawakilishi wao kujisalimisha katika Ofisi ya Tume ya Maadili zilizopo jengo la Sukari House ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga.

Mahiga alitakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.

Waziri mwingine ni wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alitakiwa kutoa tamko la rasilimali na madeni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Luhaga Mpina, alitakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.

Pazia la kurudisha fomu hizo lilifunguliwa na Waziri Kitwanga ambaye alifika katika ofisi hizo saa saba mchana, saa mbili tu baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kutoa amri hiyo saa tano asubuhi kwa kuwapa saa saba ambazo zilikuwa zikiishia saa 12 jana jioni.

Hata hivyo, Kitwanga alisema jina lake liliwekwa katika orodha hiyo kimakosa kwakuwa alikuwa ameshakamilisha zoezi hilo.

“Mimi leo (jana) nimetajwa kwa makosa na hata kwenye majina ya jana (juzi) sikuwepo nadhani ilikuwa bahati mbaya kuwekwa, kamishna ameangalia akaona nimekamilisha na kaniahidi atamueleza Waziri Mkuu kuwa jina langu lilipelekwa kwa bahati mbaya,” alisema Kitwanga.

Wakati Waziri Kitwanga akisema hayo mmoja wa maofisa wa Tume hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe aliliambia gazeti hili kwamba jina la waziri huyo halikukosewa kupelekwa kwa Waziri Mkuu kwakuwa alikuwa hajasaini hati ya mali.

“Kitwanga ilikuwa lazima aje, alikuwa hajasaini fomu yake ya mali aliijaza tu sasa zile fomu zina utaratibu mrefu lazima zikapigwe muhuri wa mwanasheria kama haina sahihi ya mhusika inakuwa haina maana,” alisema ofisa huyo.

Kwa upande wa Waziri Mahiga ambaye alifika ofisi za Tume hiyo muda mfupi tu baada ya Kitwanga kuondoka, alisema alishindwa kuwasilisha fomu hizo kwa wakati kutokana na ratiba ngumu ya kazi aliyonayo.

“Nimemueleza Kamishna na amenielewa amekubali kuwa kazi yangu ya sasa ni ngumu nakosa muda wa kutosha, tangu nikiwa katika utumishi wa umma miaka ya nyuma sikuwahi kuchelewesha tamko langu hata mara moja,” alisema Balozi Mahiga.

MTANZANIA Jumamosi ambalo lilipiga kambi katika ofisi za Tume hiyo ilipofika saa 9:03 lilishuhudia Naibu Waziri Mpina akiwasili katika ofisi hizo na kisha kuingia ndani kukamilisha utaratibu uliompeleka.

Mpina ambaye alichukua kama dakika kati ya 10-15 hata alipotoka nje mwandishi wa habari hizi alipomuuliza sababu za yeye kuchelewa kujaza fomu hizo alijitetea kuwa alikuwa hajui stahiki zake anazopaswa kupata kama naibu waziri.

“Nimekuja kutimiza oda ya rais lakini mimi sikuchelewesha fomu kwa makusudi kwakuwa sikuwa na shida yoyote.

“Kwenye hii fomu kuna sehemu wanataka utaje mshahara, posho  na stahiki zako zote jambo ambalo mimi nilishindwa kwakuwa nilichelewa kuletewa mwongozo wa masilahi yangu kama kiongozi na maelezo haya yote niliyatoa jana (juzi) kwenye kikao na tulikubaliana kukusanya fomu Aprili lakini mpaka kaamua kututaja maana yake hajakubaliana na maelezo yetu,” alisema Mpina.

Alisema kutokana na agizo hilo alilazimika kumwagiza mhasibu kumpatia mchanganuo huo na baadaye kumalizia kujaza fomu hizo jana asubuhi.

Mbali na mawaziri hao, MTANZANIA Jumamosi haikuwaona mawaziri wawili ambao ni January na Profesa Ndalichako wakifika katika ofisi hizo za Tume kukamilisha mchakato huo.

Gazeti hili lilipotaka kujua kulikoni, maofisa wa Tume hiyo ambao nao hawakuwa tayari kutajwa majina yao walisema viongozi hao waliwatuma wawakilishi kukabidhi fomu hizo.

Kamishna wa Tume ya Maadili Jaji mstaafu Salome Kaganda, alithibitisha kupokea fomu za mawaziri na manaibu wote waliotajwa na Waziri Mkuu.

“Hakuna anayedaiwa wote watano wamekamilisha, kazi iliyobaki ni kuwasilisha katika eneo husika,” alisema Jaji Kaganda.

Kauli ya kutaka kurudishwa fomu hizo imetolewa baada ya juzi Jaji Kaganda kumkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa majina matano ya mawaziri na manaibu ambao walikuwa hawajawasilisha matamko hayo.

Awali akizungumza  na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Waziri Majaliwa alisema agizo la kurudisha fomu hilo limetolewa na Rais John Magufuli ambapo amewataka mawaziri ambao hawajajaza matamko hayo wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo jana saa 12.00 jioni.

“Jana (juzi) nilikabidhiwa majina walioshindwa kuwasilisha fomu za maadili na tamko la mali, Rais Magufuli ameelekeza mawaziri na manaibu wote ifikapo leo Ijumaa (jana) saa 12 jioni wawe wamesharudisha atakayeshindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema uwasilishaji wa tamko la mali  ni maelekezo yanayotokana na sheria ya maadili ya mwaka 1995 kifungu cha tisa 1995 sura 598 viongozi ambacho kinaeleza viongozi wote waliotajwa katika kifungu cha nne wanalazimika kutoa tamko la mali ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi.

Alisema tamko hilo ni fomu maalumu, viongozi watakaoshindwa watalazimika kutoa maelezo ya msingi na kushindwa  kufanya hivyo sheria zitachukua mkondo wake.

Sheria ya Maadili inaeleza kuwa Waziri ambaye hatatangaza mali zake au atatangaza mali za uongo atatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja hadi milioni tano.

Alisema tamko la hati za maadili lilianza kutekelezwa mwaka jana lengo ni viongozi kutoa kiapo cha maadili na uadilifu katika utekelezaji wa shughuli za utumishi wa umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles