23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Rukwa wapewa somo la kodi

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

WAFANYABIASHARA Mkoa wa Rukwa wametakiwa kuwa na tabia ya kulipa kodi kwa hiari ili kuwezesha serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Agizo hilo limetolewa na mkuu w mkoa huo, Joseph Mkirikiti jana Septemba 13, wakati alipofungua semina ya utoaji elimu ya kodi iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Sumbawanga.

“Ni vizuri wafanyabiashara wote mkawa na utaratibu wa kulipa kodi kwa hiari badala ya kusubiri mivutano kwani serikali inategemea fedha hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa umma” amesema Mkirikiti.

Katika semina hiyo iliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali wa mjini Sumbawanga, Mkirikiti amewataka watumie pia fursa ya fedha zinazotolewa na serikali kwa miradi ya afya, shule na miundombinu ili washiriki  ujenzi wa miradi hiyo.

Mkirikiti ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea kutoa fedha nyingi za miradi ikiwamo sh milioni 750 za hivi karibuni zilizotokana na tozo ya miamala ambazo zinakwenda kujenga vituo vitatu vya afya kwenye Tarafa za Mkoa wa Rukwa.

Amevitaja vituo vya afya vitakavyojengwa kuwa ni  Mwazye ( Kalambo), Kate ( Nkasi) na Kipeta ( Sumbawanga) ambapo kila kimoja kimepatiwa sh milioni 250 kwa awamu ya kwanza Agosti mwaka huu.

“Ninapenda wafanyabiashara wa Rukwa muwe na taarifa za miradi na fedha zinazotolewa na serikali ili iwe chachu kwenu kujitokeza kutekeleza na kutoa huduma ili mpate fedha, pia serikali ipate kodi badala ya kuwaachia miradi hiyo wafanyabiashara toka nje ya Rukwa” amesisitiza Mkirikiti.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA,Richard Kayombo akizungumza katika semina na wafanyabiashara mjini Sumbawanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa  TRA, Richard Kayombo amesema wapo mkoani Rukwa kuelimisha walipa kodi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na kusikiliza changamoto zao.

Kayombo  amesema TRA itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato bila mikwaruzano ambapo msingi mkubwa ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuona kodi inakusanywa kwenye mazingira rafiki na si kutumia nguvu.

Naye Anusisye Thomas mkandarasi wa ujenzi ametoa ombi kwa serikali ya mkoa kuwezesha wazabuni na wakandarasi wa ndani kupata kazi za miradi ya serikali ili wanufaike kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya mkoa wa Rukwa badala ya kutumia wakandarasi wa nje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles