29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WADHAMINI WATHAMINI MASHINDANO YA VIJANA

VIJANA ni nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo katika kila sekta kutokana na nguvu walizonazo tofauti na wengine.

Kila Taifa linategemea rasilimali ya vijana katika kujiletea maendeleo, iwe katika soka, sanaa na shughuli nyingine za kijamii.

Hata katika soka vijana hupewa kipaumbele kwenye timu kwa kuwa ndio ni mhimili wa kupambana ili kufanikisha ushindi.

Pamoja na hayo, mashindano ya vijana bado hayapewi kipaumbele na yamekosa wadhamini na hivyo kusababisha vijana wengi kutoonekana kwa vipaji vyao.

Wadhamini wamekuwa wagumu kufadhili mashindano ya vijana, hivi sasa mashindano mengi ya vijana yameota mabawa na kikubwa ni wadhamini kuziangalia timu kubwa  zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika miaka ya nyuma tumekuwa tukishuhudia mashindano mbalimbali ya vijana kama Copa Coca Cola, Uhai Cup na mengineyo, lakini kwa sasa hivi hali imekuwa tofauti na hivyo vijana wengi kukosa fursa ya kucheza soka.

Ushindani na hamasa ulikuwa mkubwa katika mashindano ya vijana na hii ilichangia kwa kiasi kikubwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na timu bora za vijana walio chini ya miaka 20, ambao baadaye hupandishwa katika timu ya wakubwa.

Mashindano ya vijana ni muhimu katika kukuza taifa letu kwa kuwa yanachangia katika mafanikio kwa timu za Ligi Kuu Bara, lakini pia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Wadhamini wana nafasi kubwa katika kuchangia mafanikio ya michezo, isiwe wanaangalia timu kubwa pekee, bali waangalie namna ya kuwapata wachezaji kupitia mashindano mbalimbali ambayo yatawaibua wachezaji watakaozichezea hizo timu kubwa.

Kwa namana yoyote ile, ipo haja ya wadhamini kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali katika kukuza soka la vijana kwa kuhakikisha mashindano ya vijana yanachezwa nchi nzima ili kuwa na zao bora la vijana ambao watakuwa hazina kwa Taifa.

Wadhamini wawekeze fedha zao katika mashindano ya vijana ambayo yatazalisha vipaji vingi vitakavyoonekana vikicheza kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ miaka ijayo.

Ipo haja kwa TFF kufufua mashindano ya vijana yaliyokufa kwa ajili ya kuwa na hazina ya vijana wenye vipaji ambao wataleta chachu katika kuchangia mafanikio ya Taifa Stars.

MTANZANIA tunaona kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kufanya vema wakiwezeshwa hususan kwa kuwaandalia mashindano mengi ambayo yatawapa uzoefu wa mashindano mara kwa mara.

Itakumbukwa kuwa timu ya vijana walio chini ya miaka 20 ‘Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Afrika kwa umri huo yaliyofanyika mwaka huu nchini Gabon, vijana waliwakilisha vema nchi licha ya kutolewa katika hatua ya makundi.

TFF ijipange vizuri kusaka wadhamini kwa ajili ya mashindano ya vijana na si kuangalia wadhamini kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara pekee, kwani kufanya hivyo ni kudhohofisha soka la vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles