21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

HATUA MUHIMU ZA KUFUATA MWISHO WA MWAKA

Na AGATHA CHARLES

MSIMU huu wa sikukuu husababisha watu kufanya matumizi nje ya bajeti na wakati mwingine kukosa fedha za kukamilisha baadhi ya majukumu yaliyo mbele kwa wakati huo.

Hilo limesababisha kila mwaka mara baada ya kumalizika kwa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, watu wengi huuita Januari kuwa ni mwezi dume.

Jina hilo linatokana na matumizi makubwa yaliyofanyika msimu wa sikukuu za Desemba na kusababisha kuanza Januari bila kuwa na fedha za kutosha.

Kutokana na hilo, MTANZANIA lilizungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi ambaye alichambua zaidi na kupendekeza kinachotakiwa kufanywa ili kuepuka kukosa fedha mwezi dume.

Profesa Moshi ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, alisema dhana ya matumizi makubwa hujitokeza kutokana na Desemba kuwa na sikukuu zilizoongozana yaani Krismasi na mwaka mpya.

Alisema ni mwezi ambao watu wengi wanasafiri kwa likizo hivyo hufanyika matumizi makubwa kuliko miezi mingine.

“Kutokuwa na mpango mzuri wa matumizi husababisha kuingia Januari ukiwa huna kitu. Ni dunia nzima inakuwa na pirikapirika si Wakristo au Waisilamu kwani kila mtu anasherehekea kumaliza mwaka, huko Ulaya zinaanza tangu Oktoba,” alisema Profesa Moshi.

Akichambua namna ya kukabiliana na hilo, Profesa Moshi alisema suala la kwanza ni kuweka akiba ambayo itakusaidia utakapoishiwa.

Alisema kila mwaka mtu anapaswa kutenga fungu (fedha) kwa ajili ya sherehe hiyo na kuweka fedha za akiba za Januari.

“Usikope, ukikopa utajiona tajiri na utatumia sana, jipange vizuri. Ukikopa utakuwa na mzigo wa deni la kulipa hivyo lazima utaona Januari ni chungu,” alisema Profesa Moshi.

Mmoja wa wachambuzi ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alielezea kuwa kutenga bajeti pekee hakutoshi bali inapaswa kufunguliwa akaunti ya pekee ambayo familia itakusanya fedha ambazo hazitaingiliana na matumizi ya kawaida.

Mchambuzi huyo alisema kitu kingine kinachoweza kuepusha machungu ya Januari ni kupunguza matumizi hasa ya kwenda kusherehekea hoteli kubwa.

Alisema jambo jingine ni kupunguza au kuacha  kusafiri kwenda sehemu za kukutana ukoo mzima kwa kuwa huko matumizi huwa yanavuka bajeti ambayo umeiandaa.

Jambo jingine alilolitahadharisha ni kuwa makini na ofa za mauzo ambazo wauzaji wengi wa bidhaa huzitoa hasa katika msimu wa sikukuu kwa kudai wapo ambao huweka bango hilo lakini bei ikiwa ni ileile.

Wakati huo huo, katika mtandao wa Daily Nation, juzi waliandika vitu vya kuzingatia ili uwe salama wakati wa msimu huu wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Moja ya vitu hivyo ni kuacha kuweka taarifa zako muhimu kwenye mitandao ya kijami,i huku wakitolea mfano kuwa unaweza kuweka picha ya ulipokuwa na si ulipo.

Katika mtandao huo, Mtaalamu na mshauri wa masuala ya kiusalama, Simiyu Werunga, anasema mitandao ya kijamii imewarahisishia watekaji kwa kugundua sehemu mtu anakofanya kazi, siku za kufanya kazi, unapokuwa, unachomiliki na watoto wanakosoma.

“Watekaji wako makini, ni rahisi kukwambia una utajiri gani na kukulenga wewe au watoto wako kwa kutaka kikombozi (ransom),” alisema Werunga.

Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa ni namna ya uendeshaji gari kwa makini na kuhakikisha gari iwapo ni zima.

Kitu kingine cha kuangalia ni sehemu ya kula na kuhakikisha kuwa chakula hicho ni salama na kimepikwa vyema.

Katika andiko hilo, limewaelekeza watu hususani wanaosafiri kuacha nyumba zao zikiwa katika hali ya usalama kwa kutumia mlinzi pamoja na kuhakikisha jirani yako anafahamu kuwa umesafiri ili aweze kusaidia usalama.

Kutokana na wengi kupamba mapambo mbalimbai ya sikukuu hizo, andiko hilo limeelekeza mtu kutumia mapambo yenye usalama zaidi hasa kwa watoto na kuwa makini na swichi za umeme.

Kutokana na familia nyingi kutoka msimu huu wa sikukuu, andiko hilo limewakumbusha wazazi/walezi kutoruhusu watoto wao kuogelea mbali na eneo walipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles