Na Joseph Lino
SOKO la magari la Afrika Mashariki ni kubwa na linazidi kukua kila mwaka hasa ikizingatiwa kuwa hata nchi za jirani ambazo hazina bandari hutumia huduma za uagizaji na upitishaji magari katika bandari hizo.
Suala hilo si dogo kwani zaidi ya nchi sita hutumia bandari za Afrika Mashariki ikiwamo Mombasa, nchini Kenya na Dar es Salaam, Tanzania. Nchi hizo ni Malawi, Zambia, DR Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda.
Biashara hii yenye kufikia mabilioni ya dola katika vyombo vya moto ikiwamo magari mapya na yaliyotumika, pikipiki, mabasi na malori na mitambo sasa ni biashara ambayo inatarajia kubadilisha eneo la Kigamboni kuwa soko kubwa la magari Afrika na kuziba ombwe hilo haraka la shughuli mukelebu wilayani Kigamboni, baada ya kuvunjwa Mamlaka ya Maendeleo Kigamboni (KDA).
Kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ni kuwa kuanzia Januari mwakani biashara ya imedhibitiwa ambapo magari yote yatakuwa yanauzwa katika maeneo maalumu ya jijini yaliyotengwa na kujulikana kama Dar es Salaam Automobile Zone iliyoko eneo la Kigamboni.
Eneo hilo lenye jumla la mita za mraba milioni 2, ilitegemewa kuwa soko kubwa la magari katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na kama nchi imepania kushiriki kikamilifu katika biashara hii nono isiyo na matatizo mengi.
Mwezi uliopita Makonda aliagiza wamiliki wa ‘showroom’ za kuuza magari kuhamia Kigamboni ifikapo Januari 2018, kutokana na kuchipuka ‘showroom’ kila mahali na katika maeneo yasiyo rasmi na kufanya udhibiti wa biashara hiyo kuwa tatizo na hivyo kulea wizi.
Hata hivyo, wamiliki hao walimwomba Makonda kuharakisha kwa ujenzi wa miundombinu katika eneo la Kigamboni, ili kuboresha mazingira mazuri ya kibiashara katika eneo husika kwani kwa hali ilivyo kwa sasa ni mapori tu na hakuna huduma yoyote iliyowekwa zaidi ya viwanja vinavyoendelea kupimwa.
Wamiliki hao walikubali kuhamishia ‘showroom’ eneo la Kigamboni baada ya kikao kati ya Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na mkuu wa mkoa ambao walijadili hali ya uamauzi huo kwa marefu na mapana.
“Tumekubaliana kuhamia lakini tumeomba Serikali kuheshimu ahadi ya kuweka miundombinu inayohitajika ili kuwavutia wafanyabiashara na wateja wengi waweze kufika Kigamboni bila vipingamizi,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye.
Simbeye anaelezea wazo la kuhamia Kigamboni kuwa ni zuri kutokana kuwa linatoa fursa kwa wauzaji wa magari kuwa katika sehemu moja ya kuuzia magari katika Afrika Mashariki na Kati na hivyo kutakuwa na mvuto wa aina yake.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Raymond Mbilinyi, anasema wamekubali wazo la mkuu wa mkoa ambalo limelenga kupunguza changamoto za msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Na anaelezea kuwa wataweka mipango ya kuhakikisha wanahamia katika muda uliopangwa.
Makonda aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea barua za maombi 100 kutoka wamiliki ambao wapo tayari kuhamia Kigamboni kufikia mwezi Januari mwakani. Tatizo la ufinyu wa sehemu ya shuguli wakati huu lilijionesha wazi na tukio la moto la Superdoll katika Barabara ya Nyerere ambapo moto ulichukua siku mbili kuzimwa.
Makonda anasema umuhimu wa kutenga eneo maalumu la kuuzia magari ni kuwa wafanyabiashara wataonyesha magari yao sehemu moja na itarahisisha Mamlaka ya Mapato (TRA) kukusanya mapato katika ofisi zao zitakazokuwepo eneo hilo hilo, kwani maduka hayo yatakuwa maeneo ya forodha na hivyo kuleta ushindani wa kweli.
Manufaa mengine itakuwa rahisi kudhibiti wizi wa magari na changamoto za msongamano wa magari ambao unasababisha hasara kubwa. Isitoshe mradi huo utasababisha matumizi yanayostahiki kwa daraja la Kigamboni na hivyo kuleta thamani kamili ya daraja hilo kwa wawekezji wake kutokana na kuongezeka kwa haraka ukubwa wa matumizi yake. Isitoshe wizi wa magari utadhibitiwa kwani Kigamboni ni kama kisiwa na Daraja la Nyerere au Feri itatumika kudhibiti wizi huo baada ya tukio au hali ya kutishia wizi kutokea.
Pia mpango wa kutenga eneo maalumu ni kufanya Jiji la Dar es Salaam kuwa soko kubwa la kimataifa la kuuzia magari Afrika. Alifafanua kuwa atahahakikisha wamiliki hao wana miundombinu ya kutosha ikiwamo vituo vya mafuta, gereji za magari, umeme na maduka ya huduma nyingine zinazoandamana na magari yakiwamo matairi, betri, vilainishi na vipuri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, anasema wafanyabiashara wote ambao watahitaji eneo la biashara ya magari watamilikishwa kwa muda wa miaka mitatu ya mwanzo bure kisha baada ya hapo watawekewa utaratibu wa malipo, pia wamiliki hao watatakiwa kutoa kiasi cha Sh 300,000 kama dhamana ya kuonyesha nia.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, amesema mradi huo ni fursa kubwa ya maendeleo kwa wilaya hiyo na mpango huo utaifanya Kigamboni kuwa kwenye mpangilio mzuri.
Hii inatokana na ukweli kuwa baada ya kuvunjwa kwa Mamlaka ya Kuendeleza Kigamboni (KDA) na Rais John Magufuli ili kuboresha utoaji huduma katika eneo hilo, ilionekana kuwa maendeleo ni muhali ukikopa uzoefu uliokuwepo kwenye Mamlaka ya Maendeleo ya Makao Makuu Dodoma (CDA) ambayo Rais aliivunja hapo awali na hivyo hatua hiyo ni sehemu ya Mkakati wa kuziba pengo kwa ombwe uliozuka wa mipango ya maendeleo.
Hivyo basi, wazo la Makonda limekuwa lulu kwa maendeleo ya haraka ya eneo na wilaya mpya ya Kigamboni.
Naye mmiliki na muuzaji wa magari wa siku nyingi, Salim Chicago, anaelezea kuwa mpango huo utawapa unafuu wa kupata huduma zote ikiwamo za mamlaka ya mapato, bandari, polisi na huduma za kibenki pamoja za Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ndani ya eneo moja.
Upembuzi yakinifu wahitajika
Wachunguzi wa mambo na wataalamu wa uchumi wametoa hadhari kuwa pamoja na uzuri wa wazi wa wazo lenyewe lisichukuliwe na kutekelezwa kama lilivyo bila utafiti, ila lifanyiwe utafiti wa ujumla wake kwa maana ya kutengeneza upembuzi yakinifu.
Hii itatoa picha kamili ya yanayotegemewa na hivyo kuwaruhsu wadau kujitayarisha nayo badala ya kuwa ya kushtukiza tu kiutendaji. Lichukuliwe wazo kuwa ni la Serikali ya mkoa na si ya Makonda pekee ili kufanikisha vizuri wazo hili adhimu.
Biashara ya magari Tanzania
Ripoti ya Delloite inaonesha kuwa soko la magari nchini limegawanywa sehemu tatu yaani la magari mapya, yaliyotumika na ya kutengenezwa upya (refurbished). Ili kuongeza soko la mauzo ya magari mapya, makampuni ya kuuza magari wanaangalia njia ya kutengeneza magari kwa kutumia spea za magari za ndani au kuagiza kutoka magari yaliyotengenezwa nchini Kenya. Hatua hii pia inaepuka ushuru wa kuagiza kwenye gari mpya.
Kufuatana na ACG Autobei, ripoti ya magari inaonesha kuwa magari yanayoongoza katika soko la Tanzania ni aina ya Pick up ambao soko lake ni asilimia 60, ikifuatiwa na magari ya aina Sport Utility Vehicle (SUV), gari ndogo au ya kifamilia (station wagon) ambayo ni asilimia 30 ambapo magari aina ya ‘canter’ huchukua asilimia 2 au 1. Lakini wengi wanakataa ripoti hiyo kwa kudai haina uhalisia.
Magari ya aina SUV yanapendwa sana katika soko la Tanzania, ni aina ya Toyota, Land Rover na Nissan. Pia magari ambayo ni Van (yaliyofunikwa) soko lake si kubwa lakini linaongozwa na magari ya kampuni ya Maruti.
Bei za magari
Kwa mfano bei ya magari ya SUV ambalo limetengenezwa upya huuzwa kwa dola za Marekani 12,000 na bei ya gari mpya ni dola 24,000.
Pia makampuni ya kutoka China ambao Original Equipment Manufacturer (OEMs), huzalisha magari na pikipiki kwa kutumia spea za makampuni mengine na wao kuweka nembo yao na hivyo wanajaribu kuingia katika soko la Afrika Mashariki kwa kuzalisha magari aina SUV na mizigo.
Kwa upande wa magari ya Pickup, magari ya kampuni ya Toyota, Ford na Nissan yanashikilia soko lakini linaongozwa na magari aina ya Toyota Hilux. Soko la magari makubwa au malori kuwa na soko kubwa kunatokana na ukubwa wa nchi ya Tanzania.
Magari ya kampuni za Kichina (OEM) yanaongoza katika soko kwa sababu ya uwepo wa uhusiano mzuri wa kisiasa na uchumi wa nchi za Afrika. Pia kuna tofauti kwa bei ya magari kutoka China na kampuni nyingine yenyewe ni nafuu kwa bei karibu kwa nusu bei.
Bidhaa za magari ya Kichina yameboreshwa katika miaka michache iliyopita kama Sino Truk, Foton na Dongfeng ni magari ya Kichina yanayojulikana sana nchini pamoja na mabasi aina ya Yutong.
Makampuni ya Kichina huzalisha magari yaliyotengenezwa kulingana na uchumi na soko la Tanzania. Kwa mfano, wao huweka injini nzito na matenki makubwa ya mafuta ambayo yanakabiliana na umbali mrefu wa magari. Bei ya gari mpya la Kichina ni karibu nusu ikilinganishwa na bei ya gari mpya kutoka nchi nyingine.
Magari ya Volvo na Scania yanaongoza katika soko la malori yaliyotengenezwa upya. Kwa upande wa mabasi ya Scania yanajulikana katika mabasi ya kifahari.
Magari aina ya Tata kutoka India huongoza kwenye magari ya uzito kati (Medium Duty Truck) wakati Mitsubishi huongoza katika kundi la magari pepesi (Light Duty Truck).
Eicher, Kinglong na Tata ni wenye magari mengi kwenye kundi la mabasi. Kigezo kikubwa cha ununuzi wa magari ya mzigo ni maili ngapi hutumia kwa lita, gharama ndogo ya matengenezo na bei au thamani yake ya kuliuza tena.
Ili kulinadi na kulijulisha sokoni njia mwafaka zinazotumika kwa promosheni ni matangazo ya mabango, majarida ya magari na maonesho ya biashara.
Magari yaliyotumika
Kutokana na kipato kuwa cha chini na gharama kubwa ya magari mapya, magari yaliyotumika yanaongoza katika soko la rejareja Afrika na magari mengi huagizwa kutoka Japani yanakotengenezwa.
Kwa mujibu wa utafiti wa kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa mahesabu ya Deloitte, inakadiriwa kuwa Ethiopia, Kenya, Nigeria angalau magari 8 kati ya 10 yaliyoagizwa ni yaliyotumika. Vilevile hakuna uwiano wa fedha zinazotumika na magari yaliyonunuliwa.
Hii ni hali ya kawaida Afrika kuagiza magari na spea mara nne kuliko mauzo yake ya nje, mwaka 2014 Afrika iliagiza magari yenye thamani ya dola bilioni 48 ikilinganishwa na mauzo ya dola bilioni 11.
KENYA
Katika Afrika Mashariki, Kenya ina uchumi mkubwa na ina mazingira mazuri ya biashara ya magari na chama imara cha watengenezaji magari (Auto Manufacturers), pia ina historia nzuri ya soko la magari.
Kiasi cha magari na pikipiki zinazoagizwa zimekuwa zikiongezeka kutokana na upatikanaji wa mikopo yenye kuvutia kutoka kwa mabenki kwa mujibu wa ripoti ya Delloitte.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Kenya (KNBS), kiasi cha magari yaliyonunuliwa kutoka nje kati ya 2003 na 2012 imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 300 kutoka magari 33,000 hadi 110, 474.
Kenya itakuwa na magari milioni 5 barabarani ifikapo 2030.
Hadi sasa, Kenya bado inategemea uagizaji wa magari ili kukidhi soko la ndani kwa asilimia 94 ambapo asilimia 80 ni magari yaliyotumika.
Kenya hutegemea Bandari ya Mombasa ambapo asilimia 99.9 ya mauzo ya magari kwenda nchi nyingine za Afrika kama Uganda na Tanzania, hufanyika ikiwa kitovu (hub) kwa nchi hizo ambazo ni soko lake kubwa.
Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya magari ya kifahari nchini humo ni yaliyotumika ambayo yanafikia milioni 1.3 kwa takwimu ya 2014.
Pia KNBS inasema 2015 magari 112,536 yalisajiliwa ikijumlisha aina zote, mapya na yaliyotumika. Magari yaliyotumika yanapendwa zaidi kutokana na unafuu wake wa bei, kwani huuzwa kati ya shilingi za Kenya 350,000 hadi 500, 000.
Mauzo ya magari mapya ni kwa ajili ya usafiri, ujenzi, madini, utalii, kilimo na nishati, hata hivyo Serikali ya Kenya na mamlaka za usalama ndio wanunuaji wakubwa wa magari mapya.
NIGERIA
Kutokana na ukosefu wa uzalishaji wa magari nchini humo, Nigeria inategemea sana uagizaji wa magari ili kukidhi mahitaji yake ya ndani yanayokuwa kila siku katika uchumi wa mafuta.
Magari yaliyotumika yanashikilia soko la magari nchini humo ambapo asilimia 90 yanaagizwa kutoka nje ambayo asilimia 10 ni mapya. Magari mengi ‘mitumba’ yaliyotumika huingizwa kutoka Marekani ambayo ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ghafi ya Nigeria.
Kabla ya kuongezeka kwa ushuru wa magari yaliyotumika, Nigeria ilikuwa inaagiza magari zaidi ya 100,000 kwa mwaka kutoka Marekani. Kuanzia mwaka 2015, Nigeria ina magari ya kifahari milioni 1.3 hadi milioni 10.
Kwa ujumla magari mapya na yaliyotumika yanayoagizwa katika soko la Nigeria ni kati ya 500,000 hadi milioni moja kwa mwaka. Magari yaliyotumika huitwa Tokunbos yanaongoza kwenye soko ambapo jamii ndogo sana inaweza kununua magari mapya na Serikali ndio mnunuzi mkubwa wa magari mapya hayo.
AFRIKA KUSINI
Afrika Kusini ni nchi inayoongoza katika biashara ya magari Afrika. Huzalisha magari zaidi ya 500,000 aina ya magari tofauti.
Sekta ya magari ni miongoni mwa sekta kubwa ya viwanda nchini humo, Afrika Kusini hutengeneza magari mapya na kwa ufanisi wa hali ya juu kila mwaka kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika. Magari hayo huuzwa sana Marekani na Ulaya hususan Ujerumani na Uingereza.
Makampuni makubwa yanayozalisha magari nchini humo ni pamoja na Ford, Volkswagen, Mercedes Benz, Nissan na Toyota na huuzwa barani kote. Nchi hiyo huzalisha magari zaidi ya 600,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, mauzo ya magari mapya nchini Afrika Kusini inazidi kushuka kutoka 714,000 mauzo ya 2005 hadi kufikia 617,000 mwaka 2015. Huku soko la magari yaliyotumika linazidi kuongezeka kila siku. Kwa kipindi cha miaka 10 watu wanahamia katika matumiza ya magari yaliyotumika. Ni dalili kuwa uwezo wa kiuchumi wa watu unapungua au wengi wanakuwa masikini na hivyo gari inaonekana kuwa ni ghali kwa wengi. Uchumi wa Afrika Kusini nao unaonekana kukosa kukua na unapungua nguvu kila mwaka kwa kukosa waekezaji wapya.
JAPAN
Japani imekuwa nchi inayozalisha magari kwa wingi kuliko nchi nyingine yoyote duniani tangu miaka ya 1960, na inaongoza katika utengenezaji wake na teknolojia.
Magari kutoka Japan yanayajulikana zaidi duniani kote.
Kwa mwaka jana peke yake ilizalisha magari milioni 9.2, na iliagiza magari mapya kutoka nje 344,000, huku magari yaliyotumika yaliyoagizwa kutoka nje yalikuwa 531,000. Hata hivyo mauzo ya magari yaliyotumika mwaka jana yalikuwa milioni 6.76.