Na MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM
WADAU wa habari nchini wameanza kujadili muswada wa sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri(TEF), Theophil Makunga alisema kutokana na umuhimu wa sheria inayotungwa umeonekana umuhimu wa kupanua wigo wa kukusanya maoni.
Alisema taasisi mbalimbali za habari na wadau wa habari wamekwisha kuanza kutekeleza wajibu huo Dar es Salaam, lakini pia wameweka mpango utakaowezesha kukusanya maoni ya watu wengine kutoka mikoa mbalimbali nchini.
“Maoni haya yatakusanywa kupitia klabu za waandishi wa habari ambazo zimesambaa nchi nzima.
“Kupitia kwa viongozi wao na tunaamini waandishi wa habari na wadau wengine wa habari watasoma muswada huo, kufanya uchambuzi wa maudhui yake na kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana sheria bora,” alisema.
Makunga alisema muswada huo si mali ya wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri au vyumba vya habari vya Dar es Salaam pekee bali unagusa maslahi mapana ya sekta nzima ya habari nchini.
“Sheria inayokusudiwa kutungwa inaweza kutumika miaka 50 ijayo au zaidi kama ilivyo kwa sheria ya magazeti ya 1976 ambayo imekuwapo kwa miaka 40 sasa hivyo ni muhimu kushirikisha wadau iwe bora zaidi,”alisema.
Katibu wa TEF, Nevile Meena, alisema kuna changamoto ya muda katika suala hilo lakini watajitahidi kadri inavyowezekana kuwafikia wadau wa habari watoe ushiriki wao katika muswada huo.
“Kwa taarifa hii tunawaomba waandishi wa habari kote nchini na wadau wa habari kutumia fursa hii kuwezesha upatikanaji wa maoni yatakayosaidia itungwe sheria bora kwa maslahi ya nchi, sekta ya habari na taifa kwa ujumla,” alisema Meena.