24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

WADAU WAITAKA TFF KUJITAFAKARI

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


WADAU mbalimbali wa mchezo wa soka nchini wameitaka Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutafakari upya vigezo wanavyotumia kumpata kocha sahihi wa kuifundisha timu ya soka ya Taifa.

Hatua hiyo inatokana na matokeo mabaya ya timu ya Kilimanjaro Stars waliyopata katika michuano ya Kombe la Cecafa, yanayoendelea nchini Kenya.

Kilimanjaro wameondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji, Kenya na kumaliza nafasi ya mwisho kwenye kundi A, wakiwa na pointi moja katika mechi nne walizocheza, wakifungwa mechi tatu na kwenda suluhu mchezo mmoja, huku wakifunga mabao mawili pekee katika michezo yote.

Wakizungumza kwa wakati tofauti na MTANZANIA jana, wadau hao walisema Kamati ya Ufundi iweke wazi vigezo vilivyotumika kumteua kocha wa timu, kutokana na ukakasi uliopo, kwa kile kilichotokea kwenye michuano ya Cecafa Kenya.

Kocha wa zamani wa timu ya Mbeya City na Yanga, Juma Mwambusi, alisema wasiwasi wake upo kwa wahusika waliomteua kocha huyo ili kuifundisha timu ya taifa.

“Mimi ni Mtanzania kama wengine, naumia nikiona hali hii kama ilivyo kwa wengine, TFF ndio wenye jukumu la kumteua kocha, ila sijui kama walitumia vigezo sahihi kumpata Ninje.

“Timu ya taifa si ya kufanyia majaribio, hata kama alikuwa mchezaji wa zamani na alisomea ukocha je, anafahamu mazingira ya hapa nchini? Aliwahi kufundisha timu yoyote na alitambua utayari wa wachezaji aliokabidhiwa?” alihoji Mwambusi.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay, alisema waliomteua Ninje kuwa kocha wa timu ya taifa walisahau mahitaji ya Watanzania.

“Hatukwenda Kenya kujifunza, badala yake tulitaka kushinda taji kwa kuwa  michuano ya Cecafa tunaimudu, tulifanya hivyo katika michuano ya mwaka 2010 na tulikuwa na uwezo wa kufanya tena mwaka huu, ndiyo maana kuna wachezaji wazoefu,” alisema Mayay.

Kocha wa timu ya Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio‘, aliishauri Kamati ya Ufundi ya TFF kutojali zaidi vyeti, badala yake wajikite kwenye ubora wa kocha.

“Kocha bora Tanzania kwa sasa ni Meck Maxime, lakini TFF hawakuliona hilo, wao wakavutiwa na kocha anayejua kuzungumza lugha ya Kiingereza.

“Kwa hili TFF na kamati husika wanatakiwa wajitafakari upya na nitakwenda kumweleza Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi, bila kumwonea haya kwamba uteuzi wake haukuwa sahihi,” alisema Julio.

Kocha wa Kagera Sugar, Meck Maxime, alisema licha ya TFF kuwa na viongozi wanaofahamu mpira, wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa, kabla ya kuwapa makocha majukumu ya kitaifa.

“Wahusika wanatakiwa kujifunza na kubadilika, makocha wanaofahamu mazingara ya hapa nyumbani wapo wengi, hao ndio waliotakiwa kutumiwa na si vinginevyo,” alisema Maxime.

 

Kocha Ammy Ninje  ana leseni ya ukocha daraja A la Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) na tayari ameshawaomba radhi Watanzania,  akiahidi kutengeneza kikosi bora   kitakachoshiriki michuano ijayo.

Akizungumza baada ya kuondolewa katika michuano hiyo, Ninje alisema mpango wake ulikuwa kurudi na kombe hilo nchini, ila kutokana na matokeo hayo anarejea kujipanga upya michuano ijayo.

“Tatizo lipo kwa wachezaji namna tulivyowalea, hawakuwa na kasi, ukiacha mchezo dhidi ya Zanzibar, iliyobaki yote tulicheza vizuri, ingawa hatukupata matokeo mazuri.

“Tunaomba Watanzania watusamehe kwa kuwaangusha, kwani halikuwa lengo letu, tunawaomba waendelee kuisapoti timu yao na tunawaahidi kuboresha tulipokosea,” alisema Ninje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles