33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU ALIYEHOJIWA URAIA AFANYA MAOMBI

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM


ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi (61) aliyehojiwa mara mbili na Idara ya Uhamiaji kuhusu uraia wake, ameanza kufanya maombi maalumu.

Kwa mujibu wa ujumbe uliosambaa jana kwenye mitandao ya kijamii, ambao Askofu Niwemugizi alilithibitishia MTANZANIA kuwa ni wake, maombi yake anayafanya kupitia Kitabu cha Zaburi.

Ujumbe huo ulisomeka: “Ee bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki.

“Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu, kwanini umenitupa? Kwanini ninakwenda nikihuzunika adui wakinionea?

“Nafsi yangu kwanini kuinama na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu kwa maana nitakuja kumsifu aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu (Zaburi 43: 1-2, 5)… ahsante Rais wangu JPM kwa faraja uliyonipa.”

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Askofu Niwemugizi alisema pamoja na kuwa na maombi maalumu, kila siku asubuhi kabla ya kuanza kazi, huanza kusoma na kufanya tafakari ya neno la Mungu.

Kuhusu ujumbe wake wa kumshukuru Rais Dk. John Magufuli, alisema kwa kifupi kwamba alimpigia simu jana kumpa pole juu ya yaliyompata.

“Kwahiyo, huo ujumbe niliouandika ni sala ya Zaburi ya kanisa, kwa kweli umenigusa kipekee na leo nikaufanya sehemu ya maombi maalumu,” alisema Askofu Niwemugizi.

 

ALIVYOSEMA JUZI

Akizungumza na MTANZANIA juzi katika mahojiano maalumu, Askofu Niwemugizi alisema ameshahojiwa mara mbili na Idara ya Uhamiaji, Wilaya ya Ngara.

Alisema alihojiwa Novemba 28 na Desemba 4, mwaka huu na alipeleka nyaraka muhimu kama hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa pamoja na kutakiwa kujaza fomu maalumu.

Katika mahojiano hayo na MTANZANIA, Askofu Niwemugizi alisisitiza kwamba yeye ni Mtanzania wa kuzaliwa na kwamba alizaliwa Juni 3, mwaka 1956, katika Kitongoji cha Kayanza, Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo, Wilaya ya Biharamulo.

Alisema pia kwamba alibatizwa katika Parokia ya Katoke, Biharamulo.

Kuhusu elimu yake, alisema alisoma katika Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo na Shule ya Sekondari Nyakato, iliyoko Bukoba kwa elimu ya O-level.

“Baada ya kumaliza O-level, niliingia Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba halafu nikatoka hapo nikaenda Kipalapala Tabora,” alisema.

Kwa mujibu wa askofu huyo, mama yake mzazi alizaliwa Lusahunga, mkoani Kagera wakati baba yake alizaliwa katika Tarafa ya Nyarubungo, Kijiji cha Kabukome Kitongoji cha Kayanza.

Pamoja na hayo, alisema katika maisha yake yote, hakuwahi kuhisiwa kuhusu uraia wake na mara zote amekuwa akitumia hati ya kusafiria ya Tanzania na pia ana kitambulisho cha kupigia kura cha Tanzania.

“Lakini, baada ya kutoa ushauri hivi karibuni, kwamba ni vizuri mchakato wa Katiba ukarejewa, watu wali-react na naweza kupata picha sasa nini kimesababisha nianze kuhisiwa mimi siyo raia,” alisema.

Pamoja na kuhojiwa mara mbili, alisema kwa sasa anaendelea kujaza fomu alizopewa na Uhamiaji.

Kuhusu usalama wa maisha yake, alisema hana shaka na hilo na anaendelea kuwajibika kama askofu.

 

IDARA YA UHAMIAJI

Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, aliiambia MTANZANIA juzi, kwamba Askofu Niwemugizi anahojiwa na Idara ya Uhamiaji Ngara na kwamba bado suala lake ni tuhuma ila itakapothibitika itajulikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles