25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO SITA WAPELEKWA ISRAEL KUTIBIWA MOYO

Na VERONICA ROMWALD–DAR ES SALAAM


WATOTO sita wenye umri wa mwaka mmoja hadi miaka 13, wamesafirishwa juzi kwenda nchini Israel kupatiwa matibabu ya magonjwa ya moyo.

Safari ya matibabu hayo imeratibiwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya nchini Israel.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Masoko wa JKCI, Anna Nkinda, alisema watoto hao waliondoka alfajiri ya Desemba 10, mwaka huu, kwenda nchini humo wakiongozana na wazazi wao pamoja na wauguzi wa taasisi hiyo.

“Baada ya matibabu ya watoto kukamilika, maofisa wauguzi wawili watabaki nchini humo kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa waliopo katika Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU) na chumba cha upasuaji,” alisema Nkinda.

Alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa matibabu mbalimbali ya moyo kwa watoto kwa kutumia wataalamu wazalendo.

Alisema wana mkataba na Israel kwa baadhi ya wagonjwa wachache wanaohitaji utaalamu wa juu zaidi kuwapeleka nchini humo kwa matibabu.

“Tuna ushirikiano mzuri na Israel, gharama za matibabu ya watoto hawa zinagharamiwa na Waisrael wenyewe.

“Pia, ieleweke kwamba, hili ni kundi la tano la watoto kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nchini humo tangu mwaka 2015, JKCI tulipoanza kushirikiana na Waisrael hadi sasa watoto 46 wameshatibiwa nchini humo na wanaendelea vizuri.

“Pamoja na hayo, bado tunaendelea kuwasihi wazazi na walezi wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwa sababu magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles