Na ASHA BANI
-DAR ES SALAAM
WADAU wa habari nchini wamepinga hatua ya Serikali kupitia Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kulifungia gazeti la kila wiki la Mawio kwa muda wa miezi 24.
Wameitaka Serikali kutengua uamuzi wake wa kulifungia gazeti hilo kwa vile  umekwenda kinyume na Katiba ya nchi  na Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ambayo haimpi mamlaka ya kufungia chombo cha habari waziri mwenye dhamana.
Wakizungumza   na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, wadau hao kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Umoja wa Vilabu vya Habari Tanzania (UTPC), walisema   kufungiwa kwa vyombo vya habari si mara ya kwanza licha ya sheria kutotoa fursa hiyo.
Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo, alisema si mara ya kwanza kwa waziri mwenye dhamana kutumia sheria kandamizi ikiwamo ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyofutwa mwaka 2016 na kuridhiwa na sheria ya huduma za vyombo vya habari ya 2016.
Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu,   baadhi ya magazeti yaliyowahi kufungiwa ni Mwananchi, Mawio, Mwanahalisi na Mtanzania huku   Mawio ikiwa ni mara ya pili.
Alisema Januari 15, mwaka jana gazeti la Mawio lilipigwa marufuku na kuamua kuishitaki Serikali kwa kufungua kesi mahakamani na hatimaye lilishinda kesi.
“Itambulike kuwa kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga utaratibu wa  sheria wa kumpa Waziri mamlaka makubwa katika sekta ya habari   kulifungia gazeti   kwa makosa atakayoyaona yeye kwa sababu ni kinyume na maslahi ya umma.
“Sheria hii mpya imeendelea kumfanya waziri awe Mhariri Mkuu, mlalamikaji, mpelelezi, mwendesha mashtaka na hakimu kwa wakati mmoja,’’ alisema Nsokolo.
Mratibu wa   Mtandao waWatetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),  Onesmo Olengurumwa, alisema kifungu kilichotumika kulifungia gazeti hilo, cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari kwa madai ya kuchapicha picha za viongozi wastaafu, ni kinyume na maslahi ya umma.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania Watanzania wana uhuru wa kutoa maoni na kupashana habari kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao.
Pia alisema kitendo cha kuzuia watanzania au vyombo vya habari visichapishe picha za viongozi wastaafu hasa katika mijadala ya taifa ambayo inahusu mambo yaliyotekea wakiwa madarakani ni kuwaziba watanzania midomo katika suala  la vita dhidi ya wizi wa madini .
Katika kosa la pili gazeti hilo lilitumia makala ya mbunge mmoja na mtaalamu wa sheria za madini nchini yenye maelezo juu ya mambo muhimu katika kumsaidia Rais katika vita dhidi ya uporaji wa rasilimali madini.
“Tumeshangazwa kuona waziri ambaye kwa taaluma ni mwanasheria ametumia agizo la rais kama sheria kitendo ambacho ni hatari kwa mustakabali wa taifa… kama kila kitakachoagizwa na kiongozi mkuu kitachukuliwa kama ni sheria.
“Hata hivyo kwa mujibu wa Mawio, agizo la rais kuhusu kuzuia marais wastaafu wasitajwe au kujadiliwa kwenye suala la madini, lilitoka wakati tayari gazeti hilo  limekwisha kuchapishwa na kusambazwa kwa mawakala nchi nzima,’’ alisema Olengurumwa.
Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Habari Tanzania (MCT),  Pili Mtambalike aliitaka Serikali itengue uamuzi wake wa kulifungia gazeti la Mawio kwa sababu ni   kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  a na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 ambayo kimsingi haimpi mamlaka waziri kutoa adhabu aliyoitoa.
Alisema juhudi za Serikali katika kuhakikisha uchumi unakua   na kupambana na rushwa lazima ziende sambamba na viongozi kuwa wavumilivu na kukubali kukosolewa kwa mambo ambayo ni muhimu katika kufikia malengo na matarajio.