KIJANA AJINYONGA KWA UGUMU WA MAISHA

0
712

Na Kadama Malunde

-Shinyanga

MATUKIO ya watu kujiua yameendelea kushika kasi katika Mkoa wa Sninyanga ambako kijana mwingine, Paul Ezekiel (17) mkazi wa Mtaa wa Mazinge Kata ya Ndembezi mjini hapa, amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba juu ya mti jirani na nyumba yake kwa kile kinachodaiwa ni ugumu wa maisha.

Tukio hilo lilitokea jana saa 10 alfajiri ambako inaelezwa kuwa Ezekiel alitoka nje ya lango la nyumba yao na kuelekea kwenye mti ambako alijipiga kitanzi kilichosababisha kifo chake.

Baba mzazi wa Ezekiel Paul, alisema awali kijana wake alikuwa na ugomvi na marafiki zake waendesha baiskeli maarufu ‘daladala’, ambao baadaye walisuluhishwa na akaendelea na majukumu yake.

Alisema chanzo cha kifo cha kijana wake hajakifahamu vizuri ingawa alisema kijana wake huyo pamoja na kujishughulisha na kazi mbalimbali za kujipatia kipato, alikuwa akilalamika mara kwa mara kuwa maisha ni magumu.

“Ilipofika saa 10 usiku nilisikia mlango wa chumba cha kijana wangu ukifunguliwa, nikajua ametoka kwenda kujisaidia, lakini ukapita muda mrefu sikusikia kuwa amerudi ndipo nikatoka nje na kukuta lango la uwani likiwa wazi, nikaanza kumtafuta bila mafanikio.

“Niliporudi ndani nikamwamsha mama yake mzazi na wadogo zake wawili wa kike, tukaanza kumsaka ndipo tukamuona akiwa juu ya mti jirani na nyumba yetu akiwa amekwisha kufariki dunia kwa kujinyonga na kamba,” alisema Paul.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jumanne Murilo, alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.

Matukio ya watu kuchukua uamuzi wa kujiua yameanza kukithiri katika manispaa ya Shinyanga na ndani ya mwezi mmoja hilo ni tukio la nne.

Hadi sasa waliofariki dunia kwa utaratibu huo ni Luhende Lusangija (34), Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Manispaa ya Shinyanga, Jacob Paul na Saada Elias ambaye alijijichinja kwa kisu na chupa ya soda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here