SEIF TAKAZA – Iramba
WACHIMBAJI wadogo wa madini wa mgodi Sekenke One uliopo Kijiji cha Nkonkilangi wilayani Iramba mkoani wa Singida, wamempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuwafungulia soko la kuuza madini ya dhahabu ambalo limekuwa mkombozi wa kukuza uchumi wao.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti walipotembelea mgodi huo jana, Katibu wa Idara ya Ukaguzi wa mgodi huo, Jackson Masanja alisema wachimbaji wadogo wamefarijika kwa uamuzi wa Rais Magufuli kuanzisha masoko ya madini jambo ambalo limesaidia wachimbaji wadogo.
Kupata fedha ambapo nyakati za nyuma walikuwa wakidhulumiwa na walanguzi kwa kulipwa fedha ndogo ambazo zilikuwa hazikidhi mahitaji yao ya msingi.
‘’ Ngugu zangu waandishi wa habari, hatuna budi kumshukuru rais wetu kwa kusikia kilio chetu wachimbaji wadogo kwa kutuanzishia masoko ya kuuza dhahabu kwa bei ilekezi, hii imetufanya sisi wachimbaji wadogo kutembea kifua mbele kwani hadi sasa wengi wetu tumejenga nyumba nzuri , tunasomesha watoto wetu kwa kutumia fedha za madini tukilinganisha siku za nyuma ambapo tulikuwa tukidhulumiwa haki zetu .’’ alisema Masanja
Mkurugenzi wa Sekenke One, Ayubu Mrisho aliwaambia waandishi tangu mgodi huo kufungwa na Serikali, umepoteza ajira za vijana wasiopungua 500.
‘’Tangu shughuli za mgodi huu kufungwa na Serikali kutokana kuvunjika nguzo za ndani ya mgodi na kusababisha na kutitia, tumeathirika kwa kiasi kikubwa kiuchumi, tunaiomba Serikali kutufungulia ili tuanze uzalishaji, kutozalisha madini si kumetuathiri, hata mapato ya Serikali yameshuka,’’ alisema.
Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachimbaji Wadogo Kisonga Shelui(UWAWAKISHE) Mchongomani, Masumbuko Jumanne alisema awali hawakuwa wanalipa kodi,sasa kila mchimbaji mdogo analipa kodi.
‘’Sasa hivi tunaona manufaa ya kazi ya madini kwani ofisa madini mkazi Chone Malembo, anatusimamia vizuri hadi sasa kila mmoja wetu anafaidika na uchimbaji ‘’
‘’Kuhusu suala la ugonjwa wa corona wachimbaji wadogo, tumepata elimu kubwa kupitia kwa ofisa madini mkazi, watendaji wa vijiji na kata pamoja na kamati ya usalama ya wilaya yetu jana wamepita kuona kama tunachukua tahadhari ya ugonjwa wa corona’’alisemaMasumbuko.