28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Wachimbaji wadogo Shilalo walia kudhulumiwa, Serikali yatoa kauli

Na Mwandishi Wetu, Misungwi

BAADA ya kufanya shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu kwa miaka saba tangu 2017 katika eneo la Shilalo wilayani Misungwi mkoani hapa, wachimbaji wadogo wametakiwa kumpisha mwekezaji kampuni ya China, huku wakipinga malipo kidogo ya fidia ya wastani wa Sh 500,000 hadi Sh milioni 2 kwa kila duara moja lenye watu sita mpaka 10.

Mgodi huo ulianza shughuli za uchimbaji mwaka 2017 ukiwa rashi kisha mwaka 2019 hadi 2020 uzalishaji ukasimama, mwaka 2022 ukakatiwa leseni na kurasimishwa, ambapo mwaka huu wamiliki wa leseni wameingia makubaliano na kampuni ya China, Tanjikuangye Company Ltd kufanya utafiti na kusaidia vifaa na utaalam ili kurahisisha uzalishaji.

Mmoja wa wachimbaji hao, Antony Madono, amesema wao ndiyo waanzilishi wa eneo hilo na wamefanya uwekezaji mbalimbali ikiwemo kukodi vifaa, kusawazisha eneo na kutengeneza barabarani kwenda mgodini, lakini baada ya mwekezaji kupatikana wametupwa kando na watu wengine kunufaika.

“Ugomvi wetu ulianza baada ya kutaka watulipe kwa kukisia na tukaanza kuhoji majibu ya utafiti wa Mchina na mkataba wa makubaliano uko wapi, hawataki kutoa mkataba wanataka wasikie kila duara Sh milioni 2 mko 10 mnagawana Sh 200,000, je tutasafirisha familia zetu kwa fedha hii.

“Makubaliano yalikuwa kama wakipata mwekezaji sisi wachimbaji wadogo tunapata asilimia mbili ya 10, kama tumepata sisi tunawapa wao asilimia mbili. Tunaomba kilio hiki kimfikie Rais wetu atusaidie hatuna msaada wowote hapa tumetengwa, hatukatai kulipwa sisi tunaomba mkataba uwekwe wazi tuko tayari kuondoka,” amesema Madono.

Naye, Janeth Bwire, amesema wamekuwa wakichimba eneo hilo kwa miaka saba tangu 2017 ambapo Juni 17, mwaka huu walitakiwa kumpisha kwa siku 30 mwekezaji achukue sampuli na kufanya uchunguzi kubaini kiwango cha dhahabu kilichopo, kisha watakubaliana namna ya kuendesha shughuli zao na kila upande unufaike.

“Baada ya siku 30 kupita tukakuta Julai 17 kupata mrejesho wa uchunguzi huo na kujua wamefikia wapi wakatuambia tuonane Julai 24 kumaliza mambo yote, lakini tulivyofika badala ya kupewa majibu tukaanza kukadiriwa tukaambiwa tupewe kila duara moja Sh milioni 2.

“Tunaomba Rais atusaidie wanatunyanyasa waliochukua leseni hawana maduara sampuli Wachina wamechukua kwenye maduara yetu lakini leo baada ya kupata fedha wanatuona sisi ni takataka genge la wahuni. Tunaomba Rais atuhurumie apaze sauti yake atutetee ili tupate haki yetu,” amesema Janeth

Kichere Malale amesema: “kwenye huu mgodi sisi ndiyo wawekezaji wa hapa tumefanya utafiti tukapata mwamba mpaka leo tangu Wachina wamekuja hapa hakuna aliyepata chochote, tumevamiwa na tunamlalamikia mwenye leseni ndiye ametudhulumu,”

 Akitolea ufafanuzi wa madai hayo, Mwenyekiti wa Shilalo Mining Group wanaomiliki leseni ya mgodi huo, Peter Charles, amesema kikundi chao kiliundwa mwaka 2018 kikiwa na wanachama 24 na kupewa haki za kusimamia uchimbaji mdogo kwenye rashi hiyo na mwaka 2022 wakapewa leseni.

Amesema baada ya kupata leseni kikundi kikatafuta usaidizi wa vifaa na utaalam kwenye makampuni ya kigeni ndipo akapatikana Tanjikuangye Company Ltd ambayo kwa sasa inafanya utafiti ili kuweka mali zao na kutoa usaidizi wa vifaa

“Lakini wakati tukiendelea kuzungumza na Mchina kulikuwa na wachuuzi wadogo wadogo ambao tumeshakaa nao zaidi ya mara tatu, na Julai, mwaka huu tulielewana namna ya kutupisha pale ili tupate technical support kwenye hiyo kampuni. Iliundwa kamati ya kufanya tathmini ya fidia zikapatikana duara 35.

“Duara nyingi zikaonekana zina thamani ya Sh 500,000, Sh milioni 1, Sh milioni 2 ndogo kabisa ni Sh 100,000 wenye maduara wakakubali kulipwa fedha kulikuwa na wamiliki 114 wakapokea fedha 10 watu 14 ndiyo waliogoma kupokea kwamba hawajaridhika na wametengeneza kikundi wanataka malipo makubwa zaidi kuliko tathmini iliyofanyika.

“Hao watu 14 tuliwaambia endapo watakubali kuja kufuata fedha zao waje wachukue zipo milango iko wazi, mpaka sasa sisi tunawatambua kama ni watu waligoma kuchukua hela lakini fedha zao zipo kama wako tayari kuchukua waje wazichukue,” amesema Charles

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza, Nyaisara Mgaya, amesema ofisi yake inatambua kinachoendelea na imetoa maelekezo kwa pande zote mbili (Wachimbaji wadogo na wamiliki wa leseni) kukutana kupata ufumbuzi wa mgogoro huo, huku akiwataka wenye leseni kuhakikisha wanapopata wawekezaji wasiwaondoe wachimbaji bila kufuata utaratibu na sheria.

“Tulishwapa maelekezo ya nini cha kufanya na taarifa nilizonazo iliundwa kamati iliyoshirikisha pande zote wakazungukia yale maeneo ofisi yetu ilishiriki pia kubaini nani ana nini na kiko wapi kwahiyo walifanya tathmini wakapata jumla ya duara 39 yenye watu 114, taarifa zilizopo watu 10 ndiyo hawakuridhika na kiwango cha malipo,”

“Kwahiyo walitunadikia barua nikawasiliana na viongozi wao na kikundi nikawapa nafasi nyingine wakakae nao ili kufikia muafaka, hata kama ni wachache tuwasikilize nilitegemea wiki hii nipate taarifa kutoka kwenye kikundi ili ofisi yetu ione majibu ya kikundi na kama wachimbaji wanayakubali au la,” amesema Mgaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles