Na EMMANUEL IBRAHIMU, GEITA
WATU 13 akiwamo raia wa China, wanahofiwa kufa baada ya Mgodi wa Dhahabu wa RZ Union uliopo Nyarugusu mkoani Geita kuwafunika.
Watu hao walifunikwa na udongo huo jana wakati wakiwa ndani ya shimo wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa madini.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tukio hilo jana, Msemaji Mkuu wa Mgodi huo, Frances Kiganga, alisema shimo walimokuwa wachimbaji hao linakadiriwa kuwa na urefu wa mita 30 kwenda chini na upana wa zaidi ya mita 30.
“Taarifa hizi mimi nimezipata alfajiri ya leo, sasa siwezi kujua kwamba hitilafu hii ilitokea saa ngapi.
“Lakini kwa uhakika zaidi ninachoweza kusema hawa waliofukiwa walikuwa ndiyo wanajiandaa kutoka kupisha zamu ya watu wengine.
“Hata hivyo, taratibu za kuwaokoa zinaendelea kwa sababu hata wenzetu wa Mgodi wa Busolwa na GGM ya Geita, wameleta mashine zao kusaidia uokoaji,” alisema Kiganga.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Elisa Mugisha, alisema anaamini waliofukiwa na udongo wanaweza kuwa bado hai.
“Kwa hiyo tunaendelea na uokoaji kwa sababu kuna mpira mrefu wa kupitisha hewa umezamishwa ndani ya shimo walimokuwa,” alisema Kamugisha.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alifika eneo la tukio na kuhimiza uokoaji uliokuwa ukiendelea.
Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku saa 10.00 alfajiri wakati wachimbaji hao wakiendelea na uchimbaji wa madini.
“Tayari kikosi cha waokoaji kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) pamoja Mgodi wa Bulyankulu wilayani Kahama, wameombwa kufika eneo la tukio kusaidia uokoaji.
“Wapo pia askari wetu, wapo askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na waokoaji wa Mgodi wa Busolwa wanaendelea na jitihada za kufukua kujaribu kuwaokoa waliofukiwa.
“Kwa ujumla, hatujui waliofukiwa wana hali gani, lakini tunafanya kila jitihada kuhakikisha kuwaokoa wakiwa hai,” alisema Kamanda Mponjoli.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kiyunga, alisema jana alipotembelea eneo la tukio kuwa nguvu kubwa za uokoaji zimeongezwa kurahisisha uokoaji.
“Kuna uwezekano watu hawa wakawa hai hivyo nimegiza juhudi za ufukuaji wa shimo ziongezwe ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vya kuokolea.
“Katika hilo, nimewaomba wawashirikishe watalaamu wa migodi mingine kwa ajili ya kusaidia hatua hii,” alisema Kiyunga.
Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo walisema tukio hilo linaweza kuwa lilichangiwa na kutozingatiwa maelekezo ya watalaamu kwa kuchimba bila kuweka nguzo za kuzuia kuta za shimo zisianguke.
Mmoja wa wafanyakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la James Moga, alisema eneo la mgodi huo liliwahi kuchimbwa miaka iliyopita.
“Kwa hiyo kukosekana kwa umakini wa ufuatiliaji wa njia za zamani zilizochimba ndiko kunaweza kuwa sababu kubwa ya mgodi huo kuporomoka,” alisema Moga.
Naye Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Ally Said, alisema ni vigumu kwa sasa kubaini sababu ya mgodi kuporomoka mpaka uchunguzi wa kina utakapofanyika.
“Lakini inawezekana pia wamiliki wa mgodi huo hawakuzingatia kanuni za uchimbaji na kusababisha uporomoke.
“Nasema hivyo kwa sababu eneo hilo lilikuwa na mgodi katika miaka ya 1960, hivyo inawezekana huku kulikuwa na mashimo ya zamani ambayo yalikuwa yakichimbwa.
“Sasa basi, inawezekana waliokuwa wanachimba, walichimba juu na kufika eneo la mashimo ya zamani na hivyo kujikuta ardhi ikititia.
“Lakini hilo tutalithibitisha baada ya uchunguzi kufanyika.
“Kwa maana hiyo, hilo suala tuliache kwanza kwa sababu kikubwa sasa ni kuokoa wenzetu ndiyo maana unaona tunatumia mashine tatu, mbili zikiwa ni kataveta na buludoza moja inafukua eneo walikofukiwa,” alisema Said.
Hilo ni tukio la kwanza kwa mwaka huu kutokea kwa mgodi kutitia na kufukia wachimbaji.
Tukio la aina hiyo lilitokea Oktoba 5 mwaka 2015 baada ya machimbo ya Mgodi wa Nyangalata wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga kutiti na kuwafukia wachimbaji watano.
Wachimbaji hao waliokoloewa Novemba 15 mwaka 2015 wakiwa hai baada ya kuishi kwa siku 40 wakiwa shimoni kwa kula wadudu na mizizi.