24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI NZITO DC KUJIUZULU


Na Mwandishi Wetu, Tabora

MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele, amejiuzulu wadhifa wake, huku akiwa na siri nzito.

Mnyele ambaye kitaaluma ni mwanasheria msomi, amejiuzulu jana huku akiwa amedumu katika wadhifa huo kwa miezi minane tangu ateuliwe na Rais Dk. John Magufuli.

Hata hivyo hakuweka wazi sababu za kujiuzulu kwake.

Taarifa zinaeleza kuwa, jana Mnyele alikutana na Kamati ya Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuwaaga rasmi kuwa yeye si mtumishi tena wa Serikali.

Mnyele anakuwa mkuu wa wilaya wa pili kuachia ngazi, baada ya Ali Maswanya aliyegomea uteuzi wa Rais Dk. Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, licha ya kula kiapo cha maadili ya utumishi wa umma Ikulu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Said Ntahoni ambaye alihudhuria kikao cha madiwani wa Wilaya ya Uyui, alikiri kujiuzulu kwa Mnyele na kusema ameacha pengo kubwa katika wilaya hiyo.

“Ni kweli amejiuzulu nafasi hii tangu jana, amekuja mbele ya Kamati ya Madiwani CCM Wilaya, akatwambia amejiuzulu nafasi yake, japo hakuweka wazi sababu za kuchukua uamuzi huo.

“Aliwaambia wajumbe kwamba amemwandikia barua Rais Magufuli na ameridhia aachie ngazi…wajumbe wengi walibaki wameduwaa kwa sababu yeye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya yetu… kwa kuwa ni uamuzi wake hatukuwa na namna tena.

“Tumekuwa naye kwa miezi nane hapa, ametusaidia katika mambo mengi, nguvu yake ilikuwa bado inahitajika kwa wanaUyui ambao amekuwa akifanya nao kazi za kila siku,” alisema Ntahoni.

Alisema pengo la Mnyele ni kubwa, lakini anaamini Rais Magufuli atawapelekea kiongozi mwingine mchapakazi ambaye watashirikiana nae kwa kila nyanja ili kuinua maendeleo ya wilaya hiyo.

MNYELE
MTANZANIA ilimtafuta DC Mnyele na alipoulizwa iwapo amejiuzulu nafasi yake, alianza kwa kusema. “ Ndo nasikia kwako niko ofisini kwangu naendelea kuchapa kazi niliyotumwa na mamlaka za uteuzi.

“…unajua unapoteuliwa unatangazwa, unapotumbuliwa unatangazwa sasa taarifa hizo wewe umezitoa wapi?
“Ukitaka kujua suala hili, sehemu nzuri na ‘source’ wa uhakika mtafute Gerson Msigwa (Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu), anajua ‘issue’ (suala) hili,” alisema Mnyele.

Hata hivyo Msigwa alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema hajapata taarifa zozote kutoka mamlaka zinazohusika juu ya kiongozi huyo kujiuzulu.

Wakati ikiwa haijulikani sababu za kujiuzulu kwake, taarifa nyingine zinasema Mnyele amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na kutingwa na majukumu yake binafsi aliyonayo.
Chanzo chetu cha uhakika, kinasema Mnyele aliandika barua ya kuomba kijiuzulu mwaka jana, kwa Rais Magufuli ambayo ombi lake limekubaliwa na amejibiwa juzi.

Baadhi ya watumishi wa halmasahuri hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao, waliiambia MTANZANIA kuwa jana asubuhi Mnyele alipita kila idara akianzia ofisini kwake kuaga wafanyakazi, huku akionekana kuwa ni mwenye furaha.

“Bosi wetu alianzia ofisini kwake kuaga watumishi, baadae alipita kila idara na kubwa ambalo alikuwa akieleza ni uamuzi ambao ameufanya yeye mwenyewe bila shinikizo.

“Bosi wetu kasema uamuzi wa kusitisha ajira yake hautokani na kushindwa kwendana na kasi ya Rais Dk. Magufuli, bali anataka kufanya kazi zake
binafsi,” alisema mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo (DED), Hadija Makuwani alisema yeye ni miongozi mwa watu walioagwa jana asubuhi na mkuu huyo wa wilaya.
Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ili kuzungumzia suala hilo, hazikufanikiwa kutokana na kuwa wilayani nzega kwa shughuli ya ukaguzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles