WACHEZAJI watano wa timu ya Taifa ya Wanawake wenye umri chini ya miaka 20 ya Eritrea, wametoweka kambini nchini Uganda ambako wanashiriki michuano ya CECAFA ya wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Uganda, wachezaji hao wametoroka hotelini kwao Jinja, leo Jumanne asubuhi Novemba 2, 2021.
Wachezaji hao ni miongoni mwa kikosi kinachoshiriki michuano iliyoanza Jumamosi Oktoba 30 na inatarajia kufikia tamati, Novemba 9, 2021 Uganda, Tanzania ikiwa inawakilishwa na timu ya wanawake ya U-20, Tanzanite.
Aidha Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika taarifa yake, limesema wamesharipoti suala hilo polisi wakishirikiana kuwatafuta wachezaji waliopotea.
“Suala hilo limefikishwa Polisi Jinja na uchunguzi unaendelea. CECAFA, FUFA na Polisi wanafanya kila liwezekanalo kuwatafuta wachezaji hawa,” imesema taarifa ya CECAFA.
Imefafanua kuwa majina ya wachezaji waliotoweka hayajatolewa bado.
Eritrea inatarajia kucheza na Uganda kesho Jumatano, ikiwa ni mchezo wao wa tatu baada ya kupoteza miwili kwa kufungwa na Tanzania 1-0 na Ethiopia 5-0.