26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NARCO yahamasisha matamasha ya ulaji nyama

Na Edward Kondela, Sumbawanga

KAMPUNI ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO), imetoa wito kwa viongozi wa mikoa kujenga utaratibu wa kufanya matamasha ya ulaji nyama ili kuhamasisha wananchi kuongeza wigo wa kula nyama, kujenga afya zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.

Hayo yamesemwa na Meneja Masoko wa NARCO, Immanuel Mnzava wakati wa tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lilioandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa lililokwenda sambamba na uanzishaji wa mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.

Akizungumzia tamasha hilo, Mnzava amesema NARCO kama mdau mwalikwa katika inahamasisha ulaji wa nyama hasa nyama ya Kongwa Beef inayozalishwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) ambayo ina ranchi 14 nchini ikiwamo Ranchi ya Kalambo iliyoko mkoani Rukwa.

Mnzava  amesema uhamasishaji huu unafanyika ili kuongeza ulaji wa nyama nchini kwa kuwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ulaji wa nyama nchini kwa mtu mmoja bado uko chini ambapo ni wastani wa kilogramu 15 kwa mwaka tofauti na pendekezo la dunia la ulaji wa kilogramu 50 kwa mwaka.

“Ulaji unaopendekezwa duniani ni kilogramu 50 kwa mwaka. Kwa hiyo kwa wastani kila mwananchi ili afikie viwango vya ulaji nyama vinavyopendekezwa duniani anatakiwa kuongeza kilogramu 35 kwa mwaka, ili kufikia viwango hivyo, Tanzania inadaiwa wastani wa tani za nyama 2,100,000 kwa mwaka.

“Hili ni soko kubwa la ndani ikiwa watanzania wote watakula nyama kulingana na viwango vinavyopendekezwa duniani. Hivyo, tunapofanya matamasha kama haya tunalengo la kuhamasisha wananchi kuongeza ulaji wa nyama.

Kwa kuwa nyama inajenga miili yetu na ni kitoweo kizuri na tunapoongeza kula nyama wazalishaji wetu wa mifugo na mazao yake nchini wanakuwa wamepata soko la mifugo yao na mazao yake ikiwemo nyama,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti akizungumzia tamasha hilo, amesema ni moja ya vyanzo vya mapato na matamasha hayo yatafungua fursa ya utalii wa ndani nchini.

Amebainisha pia uwepo wa NARCO ni sehemu ya kuliongezea thamani zao la ngozi kwa kuwa ulaji wa nyama ukiongezeka utasababisha uwepo wa ngozi za kutosha katika matumizi ya viwandani pamoja na chakula.

Baadhi ya washiriki katika tamasha hilo wamesema wamefurahishwa na uwepo wa NARCO kwa kuwa imekuwa ikitoa mbegu bora za mifugo ikiwamo mbuzi na kondoo ambayo imekuwa ikitoa nyama yenye ubora mkubwa.

 Tamasha la Sumbawanga litafanyika kila mwisho wa wiki sambamba na mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles