25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wachezaji Brazil wapata ajali ya Ndege

3ad871e900000578-3980974-alan_ruschel_is_said_to_have_suffered_head_injuries_in_the_crash-a-38_1480408091114

MEDELLIN, COLOMBIA

NDEGE iliyobeba watu 81, wakiwemo wachezaji wa klabu ya soka ya Chapecoense ya nchini Brazil, imeanguka katika eneo la Medellin nchini Colombia.

Maofisa wa polisi nchini humo wamedai kuwa kati ya watu hao 81 wakiwemo abiria 72, ni watu sita tu ambao tayari wamepatikana wakiwa hai na wamekimbizwa hospitalini nchini humo kwa ajili ya matibabu zaidi. Kati ya watu sita ambao wametambulika kuwa hai ni pamoja na beki wa Chapecoense, Alan Ruschel, mwenye umri wa miaka 27, mlinda mlango, Jakson Follmann na Marcos Padilha (Danilo).

Ndege hiyo inadaiwa kupata hitilafu za mfumo wake wa umeme na kusababisha kuishiwa nguvu ikiwa angani kisha kuanguka usiku wa kuamkia leo.

Ndege hiyo ilikuwa inatoka Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji wa klabu ya Chapecoense ambao walikuwa wamepangiwa kucheza mechi ya fainali ya Copa Sudamericana dhidi ya timu ya Medellin, Atletico Nacional ya nchini Colombia.

Mechi ya awamu ya kwanza ya kombe hilo ambalo ni la pili kwa umuhimu kwa Amerika Kusini, ilikuwa imepangiwa kuchezwa Jumatano (leo), lakini sasa mchezo huo umesitishwa kutokana na janga hilo ambalo limetokea.

Timu ya Chapecoense inatoka Mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil, ilipanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza nchini humo mwaka 2014 na ilifanikiwa kufika fainali ya kombe hilo la Sudamericana kwa kuifunga San Lorenzo ya Argentina.

Taarifa zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace 146 ambayo imekuwa ikitumiwa na Shirika la ndege la Lamia la Bolivia, ilikuwa na abiria 72 pamoja na wahudumu tisa wa ndege hiyo.

Ilianguka eneo la milimani nje kidogo mwa Mji wa Medellin majira ya saa sita usiku saa za huko nchini Colombia ambapo ni sawa na saa mbili asubuhi Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maofisa wa uwanja wa ndege, marubani walisema ndege hiyo ilikuwa imepoteza nguvu mara baada ya kuwa na tatizo katika mfumo wa umeme.

Meya wa Medellin, Mayor Gutierrez, amesema ajali hiyo ni janga kubwa kwa taifa la Colombia pamoja na Brazil na klabu ya Chapecoense kwa ujumla.

“Ni pigo kubwa sana kwa taifa, ni tukio ambalo halielezeki, klabu ya Chapecoense itakuwa katika wakati mgumu sana kutokana na tukio hilo pamoja na soka la nchini Brazil,” alisema Gutierrez.

Maofisa wa Uwanja wa ndege wa Jose Maria Cordova de Rionegro uliopo Medellin, wamesema juhudi za uokoaji zinaendelea japokuwa hali mbaya ya hewa ilizuia maofisa hao kufika katika eneo la tukio hilo kwa urahisi.

Inadaiwa kwamba baada ya ajali hiyo kutokea, hakukutokea na mlipuko wa moto, jambo ambalo liliibua matumaini kwa waokoaji.

Klabu ya Chapecoense ilianzishwa mwaka 1973, ilifanikiwa kupanda daraja la kwanza (Serie A) mwaka 2014 kwa mara ya kwanza na kwa sasa ipo katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles