
NA ALOYCE NDELEIO,
UCHAGUZI wa Marekani lilikuwa ni tukio moja ambalo lilitawala nyanja nzima ya habari hususani baada ya matokeo yake kutangazwa na kuibua picha tofauti na matarajio ya walio wengi.
Aidha wale wanaoegemea kutabiri masuala ya siasa za Marekani walibakia kuegemea umaarufu ambao uongozi unaomaliza muda wake umejipatia katika Afrika, hawa waliduwazwa; wale wanaoielewa sura ya kinyonga ya Marekani hawakushangaa kuyaona mabadiliko yaliyotokea.
Kwa upande mwingine matamanio na matarajio ya watu na hususani miongoni mwa nchi za Afrika walikuwa upande wa Democrat taswira ambayo inaweza kuelezwa kuwa ni kutokana na kudekezwa na uongozi unaomaliza muda wake na hususani kwa mtazamo wa masuala ya ‘Kwa hisani ya watu wa Marekani.’
Wale wanaozielewa siasa za Marekani ni kwamba haziwezi kushabikiwa kama ligi ya soka ya Ulaya, au kule Marekani kwenyewe katika ligi ya Mpira wa Vikapu ya NBA.
Kilichojitokeza na ambacho kinaweza kuelezwa kuwa tukio la ajabu ni ile taarifa kwamba wabunge wanawake wa Tanzania wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democratic, Hillary Clinton.
Kauli hiyo inatosha kuwafikirisha wavuja jasho na kuipata picha halisi kwamba ni upande upi wanawake hao walikuwa wameuegemea katika mtazamo na matamanio yao katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani.
Kama ujumbe huo wa kusikitishwa na matokeo hayo miongoni mwa wabunge wanawake wa Tanzania ulimfikia au la, hilo wavuja jasho hawawezi kulifahamu. Lakini kama ujumbe huo ulimfikia wavuja jasho wanavuta hisia tofauti.
Kwa mbali hisia za wavuja jasho zinakutana na mwangwi wa sauti ikisema, “Msinililie mimi enyi wanawake wa Bongo, jililieni wenyewe na muwalilie wenzenu ambao hamuwaungi mkono katika chaguzi zenu.”
Kwa upande mwingine inaweza kuelezwa kuwa wabunge hao hawajawaona wanawake waliogombea nfasi za uongozi nchini mwao na ambao huenda walishindwa kutokana na kutoungwa mkono na wanawake wenzao.
Kwa kuangalia uhalisia hali hiyo inaonesha unafiki uliomo ndani ya wanasiasa wanawake kwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana wa Rais na wabunge na madiwani walikuwapo wanawake waliogombea nafasi mbalimbali na hata nafasi ya Urais.
Pamoja na hali hiyo wapo wanawake pia waliotangaza nia na kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo na hata kufikia hatua za mchujo ambapo majina yao yalikatwa.
Hoja ni wanawake wangapi miongoni mwao hadi leo wameshaonesha kusikitishwa kushindwa katika uchaguzi huo kwa wanawake wenzao?
Leo hii wamekuwapo wanawake ambao pamoja na kushinda uchaguzi huo katika ngazi ya ubunge, wapinzani wao wamefungua kesi mahakamani kupinga ushindi wao. Mmojawapo ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya ambaye katika kesi zilizofunguliwa katika mahakama ngazi tofauti ameshinda kesi yake dhidi ya mpinzani wake Mzee Steven Wassira.
Hoja ni wanawake wangapi wameweza kujitokeza hadharani kumlilia katika mapambano yake ya kesi hiyo na walau hata kumpongeza hadharani kama ambavyo wangetarajia kumpongeza Clinton iwapo angeshinda?
Inapotokea wachambuzi wa mambo wakasema kuwa baadhi ya akili za wanasiasa na hata baadhi ya wasomi wetu zimehamishiwa Ughaibuni nani atakataa uhalisia huo kwamba hawaoni yaliyomo ndani mwao bali kwa wenzao? Je, wabunge hao wanawake hivi kweli walimsikitikia Anna Mghwira aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya ACT – Wazalendo kwa kushindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita?
Upo usemi hisani huanza nyumbani lakini hilo kwa wanasiasa hao halifahamiki ila lililo muhimu kwao labda ni lile ambalo linatokana na ‘Kwa hisani ya watu wa Marekani.’
Si ajabu kwamba hivi sasa wapo katika matamanio ya kinjozi kwamba kura hizo zikirudiwa kuhesabiwa Clinton ataibuka mshindi. Haiyumkini hawa wanatakiwa kutoa boriti jichoni ndipo waone vibanzi hivyo vilivyopo Ughaibuni.