29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wazidi kumwandama RC Gama

Leonidas+Gama(1)NA ARODIA PETER, Dodoma

WABUNGE wa upinzani wa Mkoa wa Kilimanjaro wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mchakato wa uwekezaji wa ardhi katika Halmashauri ya Rombo unaomhusisha Mkuu wa Mkoa huo, Leonidas Gama.
Wabunge hao wanamtuhumu Gama kuwa ametumia vibaya madaraka yake kwa kujiingiza kwenye biashara chafu ya kupora ardhi ya wananchi na kuwapa wawekezaji wageni wakati huo huo yeye pamoja na mtoto wake wakiwa ni wabia katika uwekezaji huo.
Joseph Selasini (Rombo) na Augustine Mrema (Vunjo) waliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Takukuru inapaswa kumchunguza Gama na watendaji wengine wa serikali waliotumia vibaya fedha za umma katika kuanzisha kampuni hiyo binafsi.
Selasini alisema wanaziomba mamlaka husika zimlazimishe mkuu huyo wa mkoa arejeshe Sh milioni 168 za Halmashauri ya Rombo kwa kuwa zilitumika kufanya shughuli binafsi na halmashauri na wananchi wa Rombo hawakunufaika na shughuli hiyo.
“Sisi hatupingi uwekezaji lakini ni lazima uwe shirikishi. Wananchi wakubali na wawe wabia au wanufaike na ajira zinazotokana na uwekezaji huo,” alisema Selasini.
Juzi, Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alimtaja Gama bungeni kuwa anahusika na tuhuma za kumiliki ardhi kwa njia za ufisadi wilayani Rombo.
Halima alisema Gama ni mbia katika Kampuni binafsi ya Jun Yu Investment International Company Ltd. inayotaka kumiliki ardhi iliyokwisha kulipiwa fidia ya Sh milioni 168 na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na utaratibu.

Wakati akihitimisha hotuba yake bungeni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema atalifanyia uchunguzi suala hilo na taarifa yake itawasilishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles