30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wataka posho zao zisiguswe

dsc_0806-fileminimizer

Na Bakari Kimwanga-DODOMA

WABUNGE wamegomea hatua ya Serikali kutaka kusimamia posho na marupurupu yao, huku wakitaka suala hilo waendelee kujipangia wenyewe.

Msimamo huo uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, umetolewa  baada ya Serikali kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba tatu ya mwaka 2016.

Awali Serikali ilitaka suala la stahiki hizo kwa watumishi wa umma liamuliwe na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.

Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa, alisema wametoa pendekezo hilo katika  Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298    kulinda dhana  ya mgawanyo wa madaraka.

“Tume ya Utumishi wa Bunge na Tume ya Utumishi wa Mahakama zipewe uhuru  kusimamia upangaji wa mishahara, posho na marupurupu mengine,” alisema.

Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, alisema kifungu cha 18 cha Muswada huo kuhusu muda wa mnufaika   kurejesha mkopo, Mchengerwa alisema kamati inashauri mkopo uwe mwaka mmoja baada ya kumaliza masomo.

Alisema hali hiyo itasaidia kutoa fursa kwa mnufaika kuanza kulipa mkopo wake,   utaratibu ambao hutumika katika nchi nyingine kama Kenya na Zambia.

“Kuhusu wanufaika waliojiajiri kamati inapendekeza kiwango cha kurejesha mkopo kisipungue Sh 100,000 badala ya Sh 120,000 kama Serikali ilivyopendekeza,” alisema Mchengerwa.

Awali, akiwasilisha hotuba ya mabadiliko ya sheria hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema   kifungu cha 8 cha Sheria hiyo kinaanisha mamlaka ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi) kuwa ni pamoja na kufanya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza ufanisi wa utumishi wa umma.

Alisema Ibara 24 ya Muswada huo inapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A cha Sheria kinachoweka masharti kuwa Taasisi, Wakala au Tume za Serikali hazitakuwa na mamlaka ya kuidhinisha mishahara na marupurupu kwa watumishi wa taasisi hizo na badala yake kibali kwa ajili hiyo kitatolewa na Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais (Utumishi).

“Marekebisho hayo yanalenga kuwa na mamlaka moja inayoratibu mishahara, posho na marupurupu na watumishi katika taasisi za Serikali na pia kuwianisha mishahara posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa taasisi hizo.

“Masharti yaliyopendekezwa hayatatumika. Ibara hiyo imefutwa na kuandikwa upya masharti yanayopendekezwa hayatatumika kwa mishahara, marupurupu na masilahi mengine kwa Bunge,Mahakama, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Polisi,Magereza,JKT, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa ili utaratibu huo kuendelea kama ilivyo sasa katika sheria zinazosimamia taasisi hizo.

“Kifungu cha 20 (1) (c) cha Sheria ya Utumishi wa umma kinaipa Tume ya Utumishi wa Umma mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu usaili wa watumishi wa umma unaofanywa na tume hiyo,” alisema Masaju

Awali kifungu cha 8 kilikuwa kinapendekeza kufanyiwa  marekebisho  kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi) kurekebisha na kuwianisha  mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma wakiwamo   wabunge na idara ya mahakama.

Huku ikipendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A kinachozizuia taasisi za umma, wakala, bodi na tume zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine  kwa watumishi.

Sehemu ya tano inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 kwa lengo la kutoa tafsiri ya neno “recruitment secretariat”, maneno hayo yametumika katika Sheria lakini hayakuwa yamepewa tafsiri.

Kiama kwa waajiri

Alisema Ibara ya 19 ya Muswada huo, inapendekeza kufuta kifungu cha 20 na 21,ambacho kilikuwa kinaeleza kwa kuwa si rahisi mwajiri kufahamu kama mtumishi anayeajiriwa ni mnufaika wa mkopo.

Kutokana na hali hiyo,alisema Muswada unaainisha kuwa mwajiri atatakiwa kuifahamisha Bodi ya Mikopo ndani ya siku 28,baada ya mwajiriwa huyo mwenye Shahada au Astashahada ili bodi  iangalie kama mwajiriwa huyo ni mnufaika wa mikopo.

“Mwajiri ambaye atashindwa kutekeleza masharti ya kifungu hicho atakuwa anatenda kosa la jinai ambalo adhabu yake ni Sh milioni moja au kifungo cha miezi sita gerezani. Pia inapendekezwa baada ya mnufaika wa mkopo mwajiri atatakiwa kukata asilimia 15 ya mshahara wa mwajiriwa.

“Bodi au mawakala wake wawe na mamlaka ya kukagua kumbukumbuku za waajiriwa kwa lengo la kufuta taarifa zinazohusiana na wanufaika wa mkopo pamoja na kumbukumbu za  waajiriwa kwa lengo la kutafuta taarifa zinazohusiana na wanufaika wa mkopo kwa hatua zao muhimu kuhusu makusanyo wa mikopo,” alisema

AG Masaju alisema kifungu cha 57 cha sheria hiyo, kinaweka masharti kuhusu zuio kwa shughuli za binadamu zinzoathiri ulinzi wa bahari, mito, mabwawa zisifanyike ndani ya mita 60 kutoka kingo za bahari, mito au mabwawa.

Alisema hatua hiyo imekusudiwa kuimarisha ulinzi na usalama wa mazingira ya maeneo husika ya bahari, maziwa na mito na mabwawa.

“Ibara ya 11 ya Muswada inapendekeza kifungu hicho kirekebishwe katika kifungu kidogo cha pili   kuweka mwongozo wa namna ya kupima mita 60 ambako shughuli za  binadamu zimezuiliwa kufanyika.

“Kifungu cha 184 kinaeleza athari na uthamini wa mazingira. Ibara ya 12 inapendekeza kuwa kitendo cha mtu yeyote kushindwa au kukataa kufanya tathimini ya athari za Mazingira kwa mradi unaohitaji tathmini hiyo kufanyika ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka miwili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles