22.5 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Godbless Lema kizimbani tena, arudishwa mahabusu

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema)

Na JANETH MUSHI, ARUSHA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akikabiliwa na mashitaka matatu ya uchochezi.

Lema alisomewa mashtaka hayo jana baada ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa siku saba bila kufikishwa mahakamani.

Hatua hiyo ilimlazimu wakili wake, John Mallya kufungua kesi ya jinai namba 56 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha,  akiiomba iamuru mteja wake apelekwe mahakamani baada  ya kushikiliwa kwa zaidi ya saa 175.

Shauri hilo la kutaka mbunge huyo afikishwe mahakamani, lilikuwa linasikilizwa jana na Jaji Salma Magimbi kisha liliahirishwa baada ya mawakili wa Lema kuiarifu mahakama hiyo kuwa mteja wao tayari alikuwa amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kusomewa mashtaka.

Kutokana na hatua hiyo, Jaji Magimbi aliahirisha kusikiliza maombi
hayo na kuwalazimu mawakili wa mbunge huyo kutoka mbio mahakamani na kwenda alipokuwa mteja wao akisomewa mashtaka ya uchochezi.

Akisoma mashtaka hayo jana, Wakili wa Serikali, Matenus Marandu, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Desderi Kamugisha, kuwa mtuhumiwa   anakabiliwa na mashtaka mawili ya uchochezi.

Wakili Marandu alidai   kesi ya kwanza jinai yenye namba 440, inamkabili Lema kwa kudaiwa kuwa kati ya Oktoba 22 mwaka huu, maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara, alisema kama Rais  Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani, iko siku Taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.

“Pia, alisema rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria na mipaka ya Katiba, ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji damu kwa sababu  watu watajaa vifua na wakiamua kulipuka, polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza,” alisema wakili huyo.

Katika kesi ya pili ya jinai namba 441, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, alidai   Lema anakabiliwa na shtaka la uchoezi akidaiwa  kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii.

Alidai   Oktoba 23 mwaka huu, katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema alisema   kiburi cha rais kisiporekebishwa na rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, mwaka 2020 haitafika, Mungu atakuwa amekwisha kuchukua maisha yake.

“Alisema pia kwamba  rais ana kiburi, rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa Serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani na wananyanyaswa.

“Mtuhumiwa alitoa kauli hizo kinyume cha sheria na kifungu cha 63 (B) cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mtuhumiwa huyo alikana tuhuma zote zinazomkabili na  upande wa utetezi uliomba mteja wao apatiwe dhamana hoja
iliyopingwa na Wakili wa Serikali.

Akipinga hoja hiyo, Wakili Marandu aliwasilisha maombi akiomba
mtuhumiwa huyo asipewe dhamana akidai anakabiliwa na kesi nyingine mbili za uchochezi katika mahakama hiyo na hata alipopewa dhamana kwa kesi hizo bado aliendelea kufanya makosa.

“Tunaiomba asipewe dhamana aendelee kubaki rumande mpaka upelelezi utakapokamilika na kusikiliza kesi zote hii ni kwa ajili ya usalama wake na kudumisha amani na utulivu katika jamii yetu,” alidai Wakili Marandu

Upande wa Serikali uliwasilisha hati ya kiapo ambayo
ni barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO) ikisisitiza kutopewa dhamana kwa mtuhumiwa huyo.

Mawakili wa utetezi wakijibu hoja hizo wakiongozwa na Wakili
Sheck Mfinanga walidai hati hiyo haina sifa ya kupokelewa mahakamani kutokana na kutojulikana aliyeiandaa kwa sababu  RCO ni cheo na si mtu.

“Ukiangalia kipengele cha 13 ni maneno ya kuambiwa na kwa mujibu wa sheria maneno ya kuambiwa hayakubaliki na katika hati hii wametaja  Mbunge wa Arusha wakati kuna wabunge wengi, hawajamtaja Lema, hawajamtaja mleta maombi, mjibu maombi wala haionekani nakala zimeenda kwa nani,”alidai Wakili Mfinanga.

Naye Wakili Mallya alidai kuwa haki ya dhamana kwa mshitakiwa ni haki ya Katiba kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 13 6 (b) na
Katiba inataka mpaka mtu athibitike kufanya kosa na kutiwa hatiani.

“Hana hatia mpaka itakapothibitishwa na mashahidi na Mahakama
kuridhia na kumtia hatiani.  Ni rai ya upande  wa utetezi kutupilia mbali maombi hayo na ikizingatiwa kuwa Lema ni Mbunge,”alidai.

Akijibu hoja za pande hizo, Hakimu Mkazi Kamugisha aliziomba zote kumpa muda hadi Novemba 11, mwaka huu ili apitie hoja hizo na kutoa uamuzi endapo Mahakama hiyo itatoa dhamana kwa mtuhumiwa ama la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles