
Na PENDO FUNDISHA-MBEYA
JESHI la polisi mkoani Mbeya limewafukuza kazi polisi wawili kwa kukiuka maadili ya kazi baada ya kuwafanyia vitendo vibaya wanafunzi wa kike wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Isuto iliyopo Mbeya vijijini.
Askari hao ni PC Petro Mgana mwenye namba H 4925 wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani Mbeya (FFU) na PC Lukas Ng’weina wa Wilaya ya Polisi Mbalizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea November 15 usiku, katika Shule ya Sekondari ya Isuto iliyopo Kijiji na Kata ya Isuto Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Polisi Mbalizi.
Alisema inadaiwa askari hao kwa pamoja wakiwa kwenye ulinzi wa mitihani ya taifa ya kidato cha nne ya mwaka huu, waliwatoa kwenye hosteli wanafunzi wa kike kwa kile walichodai kuwa walikuwa wanapiga kelele.
“Baada ya kuwatoa wanafunzi hao nje, waliwapeleka eneo la foleni na kuwapa adhabu zikiwamo kupiga push up, kuruka kichura, kushika masikio na kuwachapa viboko,”alisema.
Alisema adhabu hizo ziliwasababishia maumivu makali na baadhi yao kuondoka shuleni kurudi nyumbani kwao.
“Baada ya vitendo hivyo, jeshi la polisi limewachukulia hatua za nidhamu askari hao kwa kuwafukuza kazi kuanzia tarehe 08.11.2016 na baadaye watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika,”alisema.
Hata hivyo, habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kwamba Magana amelitumikia jeshi hilo kwa miezi minne tu tangu afuzu mafunzo yake katika Chuo Cha polisi Moshi (CCP) huku Lukas akiwa amekwisha kuilitumikia kwa miaka miwili.