29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wataka miti shamba itumike kutibu corona nchini

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MJADALA wa bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/21 umeendelea, huku suala la virusi vya corona likiendelea kutikisa ambapo sasa baadhi ya wabunge wanataka Serikali ijikite kwenye tiba mbadala katika kutibu virusi hivyo.

Hadi jana duniani kote watu milioni 1.1 walikuwa wameshaambukizwa virusi hivyo huku takribani 60,000 wakiwa wamepoteza maisha na 220,000 wakiwa wamepona.

Kwa Tanzania watu waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo ni 20, kati yao watatu wameshapona na wengine bado wapo chini ya uangalizi huku Serikali ikisema wanaendelea vizuri.

Akichangia bungeni juzi, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anne Tibaijuka, alisema pamoja na kuendelea kufuata tiba za hospitali, hali ikiwa mbaya lazima Watanzania warudi kwenye asili yao kuona kabla ya ujio wa wazungu, walikuwa wanatibu vipi homa ya mapafu.

“Janga kama la corona ni tukio linatokea kila baada ya miaka 100, mara ya mwisho lilitokea mwaka 1918/20 ambayo iliua watu takribani milioni 15 hadi 20, takwimu zinatofautiana, sasa hapa tuna hili janga, mimi naomba nijikite kwenye suala hili kwasababu ni muhimu,” alisema.

Alisema uwezo wa Afrika kukabiliana na mambo ambayo anayaona kwenye mtandao yakitoa China, London, ni mdogo hivyo lazima kuwe na mpango mbadala unaojikita kwenye jamii yetu.

“Tukiri kwamba kunawa mikoni ni lazima, lakini kuna hospitali nyingine hazina maji, wananchi wengine hawana maji kwa hiyo huwezi kusema mkakati ni kunawa wakati nusu ya watu hawana maji.

“Sisemi tusinawe, nasema kama dhahama ikitufikia kama tunavyoiona kule itakuwa kizungumkuti, hapa ndipo ninapompongeza Rais wetu (John Magufuli), tunaanza na sala kwasababu lazima tukiri mpaka sasa Mungu ametuhurumia.

“Ninachotaka kupendekeza, jamii inahitaji mbinu ya kuishi, sisi wenyewe tuna njia zetu mbadala, njia za asilia zipo wapi?  Hakuna jamii itakayokaa na kusubiri kifo lazima itaangalia namna ya kujihami, kama Mungu asipotuepusha dude hili likatupitia mbali, tukafika walipofika wenzetu, lazima tuangalie makabila yetu yana mbinu gani za kukabiliana na homa za mapafu.

“COVID-19 wanasema ni mpya, lakini siyo mara ya kwanza kwa virusi kama hivi kutokea, kufukizia ni muhim, lakini unahitaji mkaa, unahitaji kuni, sasa lazima watu wawe na hivi vitu karibu manake inatakiwa uwe karibu na joto katika tiba zetu nyingi za asilia.

“Naomba wizara ya afya na Ndugulile (Naibu Waziri wa Afya, Faustine Ndugulile) nimeshamwandikia barua rasmi, ni lazima tuangalie option B (mbunu mbadala) sisemi kwamba tusifanye option A, tuvae mask (barako), vifaa vya kusaidia watu kupumua, lakini kama itabidi na watu wengi wameambukizwa, lazima tuangalie namna ya kuokoa watu walio wengi na mimi naamini wataokoka.

“Nimeangalia Ghana sasa hivi wameshapona watu 33, wakati Holland hakuna hata mtu mmoja amepona, hii ni kwasababu wao (Ghana) wamerudi kwenye mwarobaini, wanafukizia wagonjwa na wanapona.

 “Naomba nisema hapa tunawalaum wazungu na huwezi kulaum madaktari wetu, wengi wamefundishwa kwenye desturi ya magharibi, wanabeza mambo yetu, kanakwamba kabla ya wazungu kuja sisi tulikuwa hatuishi, tulikuwa hatuugui, tiba mbadala ni kitu mihum sanani lazima Serikali sasa isaidie, kule kwangu kuna eneo fulani watu wanazuia mkaa, sasa mnataka mtu apikie nini?

“Katika kukabiliana hii corona lazima tuangalie plan A, na plan B, plan A ni hii ya kwenda hospitali, kama tukizidiwa lazima tupeane maarifa, wagogo wanafanyaje, wapogoro wanafanyaje, wanyakyusa wanafanyaje, wahaya tunafanyaje, kwasababu hii elimu ipo, lakini inapuuzwa, sisi tumelelewa na wazee, tumeshuhudia haya mambo,” alisema Profesa Tibaijuka.

Kwa upande wake  Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja,(CCM) alisema kumekuwepo na taarifa kuwa kuna tiba ya kienyeji ya kutibu homa hiyo.

“Sijaelewa kitu gani kimetukumba kama taifa pale Muhimbili kuna kitengo cha tiba mbadala, yaliyofanyika China hadi kuthibiti ugonjwa huu ni siri, si yote yanajitokeza lakini ninachotaka kusisitiza wewe Spika (Job Ndugai) unaweza kutumia kanuni ya tano kutoa mwongozo kwa Serikali na ikatafakari.

“Wengi tumetibiwa na kwa tiba mbadala na kupona, kwa miaka mingi hatuipi nafasi , tuna corona hapa ambayo ni janga la kidunia, hili janga kila nchi ipambane kwa mazingira yake,”alisema Ngeleja.

Mbunge huyo alisema hafdi sasa haijulikani China imefanikiwaje kudhibiti corona.

“Hili jambo Serikali inaweza kuli-promote, Watanzania wakafanya, kila mtu akajifukize asubuhi na familia yake kuna hasara gani tukajifukizia na tukapata nafuu, lakini itatokea nini kama kujifukiza kuna tibu lakini hatuipi nafasi, hii naomba Spika litafakariwe vizuri,”alisema.

Baada ya maelezo hayo Spika Ndugai, alisema “hii kujifukizia hata ugogoni ipo, sio ya kanda ya ziwa peke yake na haihihitaji kujifukizia kila siku, unaweza fanya kwa wiki mara moja au mara mbili, sasa wabunge mmepata tip ya bure hiyo lakini msijifukizie yasiyofukiziwa.” 

Naye Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, (CCM)  alisema Serikali iliangalie kwa makini suala la corona na kwamba kirusi cha hicho ni tofauti na vingine huku barakoa za kujikinga nazo zikiwa hazishikiki kwani bei yake ni kubwa.

 “Kuna barakoa za kitambaa kwa ajili ya wanafunzi wa shule ambazo bei yake ni Sh. 500 na inazuia,”alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya barakoa, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ndugulile, alisema barakoa za kitambaa hazizuii wala hazimkingi mtu kupata virusi vya corona.

“Tuwe waangalifu kwa matumizi ya barakoa, zitumike zilizoshauriwa na wataalam, huu ugonjwa hausambazwi kwa hewa bali kwa maji maji ikiwemo yanayotokana na chafya, hizo barakoa ya kitambaa hazizuii na haimkingi mtu kupata virusi vya corona,”alisema.

MITANDAO YA KIJAMII NA CORONA

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Hawa Mwaifunga (Chadema) aliomba Serikali kuangalia matangazo ambayo yamekuwa yapo katika mitandao ya kijamii kwamba ukichemsha mitishamba unapona ugonjwa wa Corona.

“Kuna mambo katika mitandao ya kijamii unakuta mtu anakwambia chemsha hiki, chemsha hiki jamani tutauana. Tusaidieni ndugu zangu utakuta  kuna mtu anachukua ndimu anaweka katika glasi mtu akisikia inasaidia anafanya. Tunaomba mtusaidie janga hili ni baya sana,”alisema Mbunge huyo.

Pia, alisema namba iliyotolewa katika vipeperushi kama mtu akipata tatizo la ugonjwa wa corona huwa haipokelewi kwa wakati jambo ambalo sio zuri  

“Namba ile iliyotolewa kwenye kipeperushi ukipiga inapokelewa leo inapokelewa kesho au haipokelewi, vinginevyo iongezwe nyingine, jambo hili ni muhimu na ni nyeti, tutapona kama tutaambizana ukweli,”alisema.

Alisema pia kuna changamoto katika utekelezaji wa bajeti katika  vifaa tiba kwani iliyopo haijitoshelezi.

“Bajeti inayotoka ni ndogo lakini tunaambiwa bajeti ipo katika dawa, dawa tu tujitahidi kupeleka na vifaa vya kupimia. Hali ni mbaya mnaongeza bajeti kwenye dawa, ongezeni na kwenye vifaa. Suala la utoaji wa dawa limekuwa ni changamoto kubwa tunaomba hili liangaliwe,”alisema.

Mwaifunga  aliwataka Watanzania kufuata maelekezo ya wataalamu kuhusiana na ugonjwa wa corona kwa kuwa wasafi.

“Niwakumbushe kina mama kina baba tufuate maelekezo ya wataalamu jambo hilo lipo tunaona kwa wenzetu tujitahidi kufuata maelekezo ya watalaamu wetu,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles