28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda: Msijifungie ndani kwa kuogopa corona

NA BRIGHITER MASAKI-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema anashangazwa na wananchi wa Dar es Salaam, kujifungia ndani kwa kuogopa corona na kusema hawatakiwi kukaa ndani badala yake watoke kutafuta fedha wasije wakafa kwa njaa.

Alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wakati akikagua mradi wa wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), katika eneo la Kinondoni Shamba.

“Lakini katika ajenda yangu ya kupita kuangalia barabara nilitaka sana kuzungumza na waandishi wa habari ambapo sikutengemea kama nitakutana na watu, nilitaka niongee na waandishi wa habari kwamba katika nchi yetu kuna tatizo linalozidi ukubwa wa tatizo lenyewe la ugonjwa wa corona” alisema Makonda

Alisema  haiingii akilini na wala  hawezi kuelewa kwamba sasa imefika hatua wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanajifungia nyumbani kusubiri corona.

“Wanashindwa kutoka kwenda kufanya kazi wanasubiri ugonjwa unaitwa corona, ugonjwa wenyewe ni ‘virus’ (virusi) watalaamu wanasema hausambai kwa njia ya hewa lakini tumeambiwa wote tukae ndani tujifungie kwa sababu nje kuna corona tutakufa kwa njaa,

“Na ni ugonjwa wa ajabu ambao sijawahi kuuona ambao hautakiwi kutoka kwenda kazini na nimepita Ilala nimeona baadhi ya watu wamefunga maduka kwa sababu ya corona hiyo nao ni uzembe, huwezi kufunga duka lako  kwa kuogopa corona,” alisema na kuongeza

“Corona umeambiwa ina njia za kujikinga ni kunawa mikono yako kwa maji yanayotiririka ni kuhakikisha haukai karibu na mtu anayepiga chafya mwenye homa kali na tukafundishwa na staili ya kukohoa lakini mwisho  tukaambiwa corona imeingia kwa gharama ya mikono yako mwenyewe mnaopenda kupikicha pikicha vidole vyenu kwenye pua ndio mnasafisha corona kutoka kwenye kikohozi cha mtu na kuingiza kwenye mwili wako, dawa ni kuacha kupikisha kunawa kukaa mbali unachapa kazi,” alisema.

Makonda alishangaa na kudai kuwa wameingizwa kwenye hofu ya ajabu ambayo haijawahi kutokea duniani.

“Watu wanajifungia majumbani eti kisa corona mtakufa na njaa tokeni kafanyeni kazi, tulichozuia ni uzururaji, huna jambo la kufanya unaanzisha safari ya kwenda Tegeta, huna jambo la kufanya unakwenda Mbagala aaah uwe na kitu cha kufanya sasa nikuulize swali hapo nyumbani hamkai karibu? Hamuongei? Ulichofanya nyumbani hauwezi kufanya kazini? Tokeni nendeni kufanya kazi acheni uvivu” alisisitiza. 

Makonda alisema watu hawawezi kujifungia mahala halafu kwani hata  Mungu atawashangaa .

“Kweli tunajifungia pahala kusubiri ugonjwa! Halafu kuna wapuuzi huko wanasema Serikali inadanganya idadi imeongezeka wewe taahira kwelikweli kwenu kuna mtu amekufa na corona? wewe kwenu kuna mtu anaumwa corona? Hiyo idadi imetoka wapi? Kwahiyo unataka idadi iwe kubwa ili ufanyeje? 

“Tumekubali halafu waandishi wa habari sikilizeni msifanye kazi ya kuchukua kile kinachoendelea duniani na kuleta tu hapa, kila kunapokucha wamekufa kadhaa, wamekufa kadhaa wanakufa siku zote tangu corona ianze duniani  Tanzania amekufa mtu huyo mmoja.

“Nenda sasa hivi hapa hospitali hakuna wagonjwa wengine? Tumesahau kama magonjwa mengine hayapo, malaria tumeisahau, tulikuwa na kipindupindu hapa watu wanakufa tumesahau watu kibao wanakufa hata hivi tunavyoongea kuna mtu anakata roho ni corona nayo hiyo?” Alihoji Makonda  

Alisema ukiangalia idadi ya watu nchini ni mmoja tu aliyekufa tangu mwezi wa 12, na kushangaa hofu hiyo inakotokea.

“Unaogopa hautoki ndani utakufa tu! acheni uvivu hatuwezi kuishi hivi  ndio maana leo nikasema nawafuatilia na wakandarasi nikimkuta mkandarasi naye amepaki eti anasema corona wee! tumekulipa fedha sisi barabara ipite unapaki kwa sababu ya corona? mvua itakuja nyumba za watu zitaondoka, magari yataharibika corona ndio kitu gani jamani?,” alihoji Makonda. 

Alisema kuna  nchi hataki kuitaja ambako watu wanaokufa na mafua  ni 100,000 na kwamba  kipindi hiki ni kipindi cha mafua dunia nzima kwamba watu wanakohoa halafu dawa ni zile zile  zilizokuwa zikitumika tangu zamani.

“Sasa hivi tumekuwa na uoga, uoga  unaopitiliza nchi yetu tuna watu 20 watatu kwa mujibu wa wizara ya afya wamepona, mmoja ndio huyo tena wanasema amefariki akiwa na magonjwa mengine eeeh, wewe unabaki ndani? Toka kafanye kazi toka katafute hela ukijifungia ndani huna hela utashangaa dunia imebadilika halafu utaanza kulia hakuna anatakayekusikia.

“Mimi nawaombeni sana suala la corona lisiwe kigezo cha watu kujifungia ndani unachotakiwa wewe kunawa mikono na bahati nzuri kinga ni nafuu kwa watu wa kada zote iwe maskini tajiri” alisema.

Makonda alieleza pia kushangazwa na watu wanaotaka nchi ifungwe na kuhoji  ifungwe kwa sababu gani? “Tusifungwe na mambo yanayotokea huko si lazima yatokee huku ndio maana Rais wetu akasema tumefika hatua hata Mungu tumemsahau, unaangalia habari za michezo corona, biashara corona halafu habari zenyewe huambiwi mafanikio. 

“Halafu waandishi wa habari fanyeni utafiti hawa virusi wametokea wapi chanzo ni nini wanaishi mazingira yapi tusibebe tu mambo tukayakumbatia tukahangaika nayo 

“Najua kuna watu watatoka ooh huu ugonjwa wa kidunia, watalaamu wamesema aah ahaa kwani watalaamu ndio Mungu? Kwani wangapi wanaambiwa utakufa halafu Mungu anawaponya, watu wanarudi mtaani wanapiga maisha  wewe mwenyewe uliambiwa hapa mjini utaondoka  mbona upo? Alisema.

Makonda aliwataka machinga, bodaboda na watu wa kada tofauti kuchapa kazi  kwa kuzingatia kunawa mikono na kujikinga kutoweka mikono kwenye pua.

“Unabaki nyumbani unasubiri ugonjwa upite, upite umekuwa upepo huo? Huu ndio wakati mzuri zaidi, mkulima akalime kwa bidii kwa sababu kuna wakati chakula kitahitajika, mfanyabiashara aangalie fursa kwa sababu kuna fursa  kubwa ya kujenga uchumi tusibaki majumbani kwa kisingizio kinachoitwa corona.

“We pita Ocen road, Muhimbili vituo vya afya  kote kumejaa ni corona hiyo? Mbona magojwa mengine hatuogopi mbona ukimwi unakazana tu tuna magonjwa kibao Mungu amekupigania  upo leo unaogopa corona?” alihoji Makonda.

Makonda pia aliwataka watu kuacha uzushi kwa kuchukua taarifa huko duniani na kujaza kwenye vichwa vya watu na kuonya kuharibu uchumi.

Akizungumzia mradi wa Tarura katika eneo hilo la Kinondoni Shamba, Makonda alimtaka mkandarasi kuendelea na kazi na kuacha kusingizia corona.

Alisema wananchi wanaingia hasara kwaajili ya kukwepa majukumu yao mambo yakienda tofauti ndipo wanalalamikia Serikali kwa kutaka kupata msaada.

Pia aliwataka wananchi kuacha kujifanya wajuaji wakati tatizo linapokuwa kubwa kwasababu wakati watu wanaingia katika eneo la mradi, wanawaona na hawawaambii kuwa wanavamia eneo la mradi.

Wakati huo huo alikagua miradi ya barabara inayotekelezwa na TARURA katika Wilaya ya Ilala na Kinondoni .

“Barabara ni ahadi ya muda mrefu ya Mh Rais wa Dk John Magufuli ijengwe kutoka makao makuu wa Bakwata hadi Biafra.

“Atakapokuja kuzindua msikiti azindue na barabara na wananchi mnatakiwa kulinda miundombinu kama maeneo ya barabara, hospitali na viwanja vya michezo”alisema Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles