27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wabunge wanne CCM wakatwa

Rita Mlaki-Viti MaalumVirajilal Jituson-Babati VijijiniSaid Nkumba-SikongeKisyeri Chambiri -Babati MjiniNa Bakari Kimwanga, Dodoma

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), imepitisha majina ya wagombea ubunge wa majimbo pamoja na viti maalumu, huku baadhi ya wabunge wakongwe wakijikuta wakitupwa nje.

Katika kikao hicho kilichoanza juzi na kumalizika jana mjini hapa, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, waliokatwa ni Mbunge wa Babati Mjini anayemaliza muda wake, Kisyeri Chambiri na mwenzake wa Babati Vijijini, Virajilal Jituson.

Wengine walioangukiwa na rungu la Kamati Kuu ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu ambaye alishinda katika kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali, Rita Mlaki na Mbunge wa Sikonge anayemaliza muda wake, Said Nkumba.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM, kiliiambia MTANZANIA jana mjini hapa kuwa hatua ya kufikiwa kwa uamuzi huo ni kutokana na wagombea hao kuhusishwa na tuhuma za rushwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, pamoja na baadhi yao kushinda na hata kukatiwa rufaa, lakini bado walionekana kuwa na makosa ya wazi ikiwamo ya kuhonga wajumbe kwa kuwashawishi ili wachaguliwe katika nafasi hiyo.

Katika mchakato huo, Jituson wa Babati Vijijini alipata kura 8,523 kati ya 32,073 zilizopigwa na aliyemfuatia alikuwa Daniel Sillo aliyepata kura 6, 222.

“Hali imekuwa tete kwa baadhi ya wabunge, hasa wa Babati Mjini na Vijiji ambao wote wameondolewa katika uteuzi na Kamati Kuu, unajua Chambiri ana tuhuma za rushwa na ripoti ya Takukuru ilisaidia sana kummaliza katika vikao hivi vya uteuzi.

“Ila mwenzake wa vijijini, Jituson yeye alilalamikiwa na wagombea wenzake na hata kumuhusisha na tuhuma za rushwa hali ambayo pia vilipatikana baadhi ya vielelezo dhidi yake.

“Ila kwa Rita Mlaki ni wazi hapa unaweza kusema kama kuna uonevu wa wazi kwani alishinda kura za maoni kupitia UWT kundi la NGO’s, lakini CC ikatumia hoja ya uwiano bara na Zanzibar.

“Badala yake wamemwondoa yeye aliyeshinda na kuteuliwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Hadija Abood ambaye yeye katika kundi hili sasa amepangwa na Mchungaji Getrude Lwakatare, hoja hii ya uzanzibari imetumika katika kundi hili tu haikugusa kundi la wafanyakazi wala walemavu,” alisema mtoa habari huyo ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake.

Katika kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi mwaka huu, Chambiri alishinda dhidi ya makada wengine saba wa chama hicho ambao walipinga matokeo hayo.

Katika mchakato huo wa kura za maoni, Chambiri alipachikwa jina la ‘ATM inayotembea’ kutokana na madai ya kugawa fedha kwa wapiga kura, madai ambayo hata hivyo aliyakanusha mara kwa mara.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa Chambiri alikamatwa mchana na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) akiwa ndani ya ofisi za CCM Wilaya ya Babati Mjini.

Habari zaidi kutoka ofisi za Takukuru zinaeleza kuwa hatua ya kumtia mbaroni mbunge huyo ilitokana na kutafutwa kwake kwa zaidi ya siku tano baada ya kudaiwa kushiriki vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni.

Inadaiwa Chambiri alinusurika kukamatwa na maofisa wa taasisi hiyo katika Kijiji cha Kiongozi ambapo wapambe wake wawili walikamatwa wakiwashawishi wapiga kura kwa kuwapa fedha na kukutwa na kitita cha Sh milioni 12.5.

Chambiri alipoulizwa, alikana kuhusika na kudai kuwa ni mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu wasiomtakia mema.

Alidai kuwa yeye kama mgombea na mtetezi wa jimbo hilo, amekuwa akipata taarifa mara kwa mara za kupangiwa njama kama hizo ili kudhoofisha juhudi zake za kurejea madarakani.

Wafuasi wa Lowassa

Wakati mchakato wa vikao ukiendelea taarifa za ndani ya kikoa cha CC zinaeleza kuwa pamoja kuibuka kwa hofu dhidi ya waliokuwa wapambe wanaomuunga mkono waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kuenguliwa wote wamejikuta wakipeta.

Lowassa alikuwa ni moja ya makada 38 wa chama hicho katika mbio za urais, na kujikuta wakienguliwa katika hatua za awali na baadaye kutimkia Chadema na sasa ni mgombea urais kupitia chama hicho chini ya mwamvuli wa Ukawa.

Makada hao ambao awali walihisiwa kuenguliwa ni pamoja na Hussein Bashe (Nzega Mjini), Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini) na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Elibariki Kingu (Ikungi Magharibi).

Kauli ya Nape

Jana asubuhi akizungumza na waandishi wa habari waliokuwa wakitaka ufafanuzi wa mwendelezo wa vikao hivyo vya CC, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema vikao bado vinaendelea na kwamba taarifa ataitoa hadi pale vitakapokamilika.

“Leo (jana) sina kitu ndugu zangu ni yale ya jana (juzi), kifupi CC bado inaendelea na vikao vyake na kazi yake inatoa mapendekezo kwa vikao vya juu yaani NEC maana tukisema nani kakatwa kwa sasa tunaweza kuleta mvurugano isiyokuwa na tija kwa chama chetu.

“… maana unaweza kusema nani amekatwa lakini kikao cha juu cha NEC kikikataa mapendekezo ya CC unafikiri itakuwaje. Ninachoweza kusema subirini vikao vimalizike nitatoa taarifa yote na si vinginevyo,” alisema Nape

 Serikali tatu zamng’oa waziri

Katika mchakato huo wa kura za maoni ndani ya CCM, taarifa za ndani zinaeleza kuwa kung’olewa kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Mahadhi Juma Mahadhi, kunatokana na kitabu chake cha utafiti alichoandika kuhusu muundo wa Serikali tatu faida zake na hasara.

Kutokana na hali hiyo mahasimu wake kisiasa walitumia kitabu hicho kama nyenzo ya kummaliza waziri huyo na kujikuta akiangukia pua katika mchakato huo uliofanyika katika Jimbo la Muyuni.

Mbali na Waziri huyo pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, naye aliangushwa katika kura za maoni katika Jimbo la Chumbuni, ambapo alidaiwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya vurugu zilizokuwa zikiendelea visiwani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles