LONDON, UINGEREZA
WABUNGE 40 wa chama tawala cha Conservative nchini Uingereza, wamekubaliana kusaini barua ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Theresa May.
Taarifa hizo zimeripotiwa juzi na Gazeti la Sunday Times, na kwamba idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na wabunge 48 wanaohitajika kushinikiza kufanyika uchaguzi mpya, ambao huenda ukamwondoa May madarakani.
May amekuwa katika shinikizo kutoka ndani ya chama chake kutokana na uchaguzi mkuu wa mapema uliofanyika Juni 8, ambao bila kutarajia kilipoteza wingi wa kura bungeni.
Utawala wa May pia umekosolewa jinsi unavyoyashughulikia mazungumzo ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, mchakato unaojulikana kama Brexit.
Wakosoaji wamesema kuwa awamu sita za mazungumzo ya Brexit kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, yamepiga hatua kidogo sana na hayana uwazi wa kutosha kuhusu mchakato mzima wa kujiondoa kwenye umoja huo pamoja na ratiba kamili.