23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

ITA YAHIMIZA MATUMIZI SAHIHI MITANDAO

 

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


KATIKA kuhakikisha chuo kinazalisha wataalamu wa kutosha katika masuala mazima ya ukusanyaji wa mapato, Chuo cha Kodi (ITA) hivi karibuni kimepokea wanafunzi wapya zaidi ya 50 waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho katika mwaka wa masomo wa 2017/18.

Wanafunzi hao watapata nafasi ya kujifunza masomo mbalimbali kutoka kwa wataalamu waliopo katika chuo hicho.

Sambamba na kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa chuo hicho, pia njia mbadala kama teknolojia ya mawasiliano hususani mitandao ya kijamii zinaweza kutumika ili kuweza kupata maarifa zaidi.

Vijana wengi wamekuwa wakiitumia vibaya mitandao ya kijamii ambayo iwapo itatumika vizuri uwezekano wa kupata maarifa ni mkubwa.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha wanafunzi hao katika chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha ITA, Profesa Isaya Jairo anasema kuwa teknolojia ya mawasiliano hususani mitandao ya kijamii ni njia nzuri ya kupata maarifa iwapo itatumika vizuri na jamii.

Anasema kila mwanafunzi aliyejiunga na chuo cha ITA anatakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwaajili ya kupata maarifa badala ya kuitumia katika mambo ambayo hayatakuwa na manufaa yoyote katika masomo.

Anasema kuwa chuo cha kodi kinatumia mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambao unalenga kumuwezesha mwanafunzi kujifunza badala ya kufundishwa.

Profesa Jairo anaongeza kuwa mfumo huo ndio utaratibu unaotumika ulimwenguni na kwamba lengo la utaratibu huo ni kumuwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo wa kujua cha kufanya katika fani yake na kwa chuo cha kodi pindi atakapohitimu.

Anasema kwa upande wa chuo cha kodi, mfumo wa kujenga umahili kwa mwanafunzi lengo lake ni kumfanya ajue namna bora na nzuri ya ukusanyaji wa mapato kwa faida ya nchi.

Anasema vijana wengi hutumia mitandao ya kijamii kwa masuala ya kijamii kwa kiwango kikubwa kuliko kuitumia kujifunza na kupata maarifa kwa mambo ambayo yatawasaidia kukuza kiwango cha elimu.

Anasema kwa miaka ya sasa elimu inapatikana kila mahali katika vitabu, mitandao ikiwa ni pamoja na mambo mengi ambayo husaidia sana katika kujifunza tofauti na ilvyokuwa miaka 30 iliyopita.

Anasema ni wajibu wa kila mwanafunzi kuitumia vyema mitandao hiyo ya kijamii hususan simu za kijanja za kiganjani kujifunza na kupata maarifa

Anaongeza kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia mwanafunzi hatakiwi kukaa na kutegemea kufundishwa tu na waalimu na badala yake anatakiwa kujifunza kwa kutumia nyenzo mbalimbali zilizopo.

Profesa Jairo anasema kuwa utaratibu huo ndio unaotumika katika mfumo wa kujenga umahiri kwa mwanafunzi na kwamba wanatakiwa kuzingatia hilo.

Anasema wanafunzi wote waliojiunga na chuo hicho katika fani za Astashahada ya Uwakala wa Forodha ya Afrika Mashariki, Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi pamoja na Stashada ya Uzamili ya Kodi wanatakiwa kuzingatia masomo yao kutokana na kuwa ndio lengo lao la kujiunga na chuo hicho.

Anaongeza kuwa kwa upande wake chuo cha Kodi kimejipanga kuhakikisha kitatimiza wajibu wake wa kuwapa elimu wanayostahili katika mazingira yaliyo bora.

Anasema kwa wanafunzi watakaofaulu vizuri watapata ajira kutoka katika  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na kuwa mamlaka hiyo huchukua watumishi kutoka katika chuo hicho ambao watakuwa wamefaulu katika kiwango cha juu.

Anasema kila mwanafunzi aliyejiunga na chuo hicho anatakiwa kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na kufuata sheria ndogo ndogo na taratibu za chuo ili kuweza kumaliza masomo yake bila kupata na matatizo yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles