23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA: KENYA INAKOSA WATU AINA YA NYERERE

WASHINGTON, MAREKANI


KINARA wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, amesema Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa na uwezo mkubwa katika utatuzi wa migogoro.

Alisema watu aina ya Nyerere wamekosekana serikalini nchini Kenya, ndiyo maana migogoro ya kisiasa imeshamiri.

Akihutubia katika Kituo cha Kimataifa cha Woodrow kuhusu Masuala ya Afrika, nchini Marekani, Odinga, alisisitiza kuwa mazungumzo pekee ndiyo yatatatua mgogoro inayoikabili Kenya kwa sasa.

Alisema mazungumzo yameibuka kama tiba kwa changamoto nyingi zilizozikumba nchi za Afrika, jambo linalopaswa kuigwa na Kenya.

“Kenya haina budi kukumbatia mazungumzo kama tiba kwa mgogoro wa kisiasa unaoikabili kwa sasa,” alisisitiza Odinga.

Kwenye hotuba yake, iliyoangazia changamoto za kisiasa zinazoikabili Afrika, Odinga alisema mazungumzo hayamaanishi uadui, mbali uwepo wa umoja katika ushughulikiaji wa matatizo yanayoikumba nchi husika.

Aliwatolea mfano Nyerere na Rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela kama mifano bora ya viongozi waliozingatia miito ya mazungumzo, hali iliyoziwezesha nchi zao kustawisha mifumo yao ya kidemokrasia.

“Nyerere alikubali mazungumzo ya pamoja baada ya kuhisi kwamba mfumo wa ujamaa haukufaulu, huku Mandela akifanya mazungunzo na viongozi wa Kizungu, hali iliyosababisha kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi,” alisema Odinga.

Kwa hayo, alisema nia yake ya mazungumzo ya pamoja na Rais Uhuru Kenyatta ni kuangazia mikakati ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi nchini, si kutafuta Serikali ya mseto kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya viongozi wa Muungano wa Jubilee.

Alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha Kenya si miongoni mwa nchi ambazo zimehatarisha mfumo wake wa kidemokrasia, kwa manufaa ya viongozi wachache.

“Tungali na nafasi ya kuhakikisha kuwa hatuingizwi katika kundi moja na nchi kama Zimbabwe ambazo haziheshimu demokrasia hata kidogo,” alisema.

Wiki iliyopita, Rais Kenyatta alisema amekubali miito ya kuandaa mazungumzo kati yake na Odinga, ila hilo litafanyika tu baada ya kupata mwelekeo wa iwapo ataapishwa au la, kulingana na uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya Juu.

Mahakama hiyo inatarajiwa kuanza kusikiza kesi kupinga ushindi wa Rais Kenyatta uliopatikana wakati wa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, ambao ulisuswa na Odinga kuanzia jana na itatoa uamuzi kufikia Novemba 20.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles